Hija ya Kitume ya Papa Francisko Malta: Ratiba Elekezi Aprili, 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Malta kuanzia Jumamosi tarehe 2 hadi Dominika tarehe 3 Aprili 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida.” Mdo 28: 2. Huu ni ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa baada ya kunusurika katika dhoruba kali na hatimaye kuwasili salama salimini Kisiwani Melita. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu ataondoka mjini Roma majira ya saa 2: 30 kwa Saa za Ulaya. Baada ya kuwasili na kukaribishwa rasmi, atamtembelea Bwana George William Vella Rais wa Malta na kufanya naye mazungumzo ya faragha. Atakutana na kuzungumza na Bwana Robert Abela Waziri mkuu aliyechaguliwa tena na baadaye atawahutubia viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia na wawakilishi. Baba Mtakatifu anatarajia kutembelea Bandari ya Mgarr. Ataongoza Sala katika Madhabahu ya Kitaifa ya “Ta Pinu” huko Gozo. Baadaye atarejea kwenye Bandari ya Cirkewwa na kuelekea kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Malta.
Dominika tarehe 3 Aprili 2022, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Wayesuit wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Malta kwenye Ubalozi wa Vatican huko Rabat. Atatembelea Pango la Mtakatifu Paulo na kuongoza Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Sala ya Malaika wa Bwana. Jioni atakutana na kuzungumza na wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa katika Kituo cha “John XXIII Peace Lab” kilichoko mjini Hal Far. Hapa ni mahali muhimu sana panapomwilishwa Injili ya upendo na ukarimu. Ni mahali pa majiundo makini ya: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mahali ambapo haki jamii inamwilishwa katika mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu pamoja na huduma ya afya kwa wakimbizi na wahamiaji. Takribani wakimbizi na wahamiaji 200 wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baadaye jioni ataagana na wenyeji wake, tayari kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha pamoja na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kwa upande wake, Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ni kati ya viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican wanaoandamana na Baba Mtakatifu Francisko katika Hija yake ya kitume nchini Malta. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Mario Grech kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Gozo tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2019. Anasema, hija hii ya kitume inapania pamoja na mambo mengine kuwaimarisha watu wa Mungu Kisiwani Malta katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Licha ya Malta kuwa ni kiini na chimbuko la Mapokeo ya Kanisa, lakini wao pia ni sehemu ya utandawazi wenye fursa na changamoto zake katika maisha. Hija hii ya kitume, itasaidia kupyaisha, mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Watu wa Mungu nchini Malta wanayo matumaini makubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro hasa kwa kipaumbele chake cha pekee katika kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapaswa kushiriki kikamilifu katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji badala ya mwelekeo wa sasa unaoitwisha Malta mzigo mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji. Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, kuna haja kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, kuendelea kuwekeza katika tunu bora za maisha na utume wa familia. Nchini Malta, bado familia zinapewa umuhimu wa pekee katika maisha ya watu. Lakini inapaswa kukumbukwa kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.