Hija ya Kitume ya Papa Francisko Malta: Nyayo Za Mtume Paulo: Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amepokea mwaliko kutoka kwa Serikali na Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Malta na ametia nia ya kutembelea nchini humo kuanzia Jumamosi tarehe 2 hadi Dominika tarehe 3 Aprili 2022. Itakumbukwa kwamba, hija hii ya kitume ilikuwa imepangwa kufanyika tarehe 31 Mei 2020 lakini kutokana na kuibuka kwa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 hija hii itasogezwa mbele hadi mwaka 2022. Hii ni hija ya kitume ya 36 Kimataifa kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko; na Malta inakuwa ni nchi ya 56 kutembelewa na Papa Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hija hii ya Kitume inanogeshwa na kauli mbiu “Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida.” Mdo 28: 2. Huu ni ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa baada ya kunusurika katika dhoruba kali na hatimaye kuwasili salama salimini Kisiwani Melita. Historia ya tangu kale inaonesha kwamba, ukarimu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa wananchi wa Malta kama hata lilivyo asili ya jina la nchi hii yenye amana, utajiri na urithi mkubwa wa: Kitamaduni, Kihistoria na Kibiblia. Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Malta kunako mwaka 1990 na Mwaka 2001. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alifanya hija ya kitume nchini Malta kunako mwaka 2010. Hiki ni kisiwa chenye kumbukumbu hai katika maisha na utume wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kama ilivyoandikwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume.
Kiini cha hija hii ya kitume inasimikwa katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa huruma, upendo na ukarimu kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Ni mwaliko wa kuendelea kusoma alama za nyakati hasa katika kipindi hiki cha vita kati ya Urussi na Ukraine na madhara yake kwa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 29 Machi 2022 amegusia kuhusu hija yake ya kitume nchini Malta, iliyoonesha ukarimu wa pekee sana kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa alipokumbwa na dhoruba akiwa njiani kuelekea Roma. Hii ni fursa ya kutembelea chemchemi ya uinjilishaji kwa kukutana na watu wa Mungu kwenye Kisiwa cha Malta kilichoko kwenye Bahari ya Mediterrania. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha.
Nchi ya Malta imekuwa mstari wa mbele katika kumwilisha upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu tangu wakati huu, anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maandalizi na hatimaye, wakati wa hija yake ya kitume nchini Malta. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika hija hii fupi, lakini yenye umuhimu wa pekee katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi ya Waraka wa Mtume Paulo Kwa Wagalatia alisema kwamba, Mtakatifu Paulo Mtume anaonesha jinsi ambavyo Ufunuo wa Neno la Mungu ulivyogusa undani wa maisha yake kiasi hata cha kuweka kando tamaduni na mapokeo yake ya zamani, ili kupokea upya na usafi wa Injili. Uhuru wa Wakristo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka unapyaisha tamaduni na mapokeo ya kidini mintarafu mwanga wa Injili. Uhuru wa wana wa Mungu walioupata kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo unawawezesha kupata hadhi ya kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu na wakati huo huo, kuiwezesha imani kupenya katika tamaduni mbalimbali na kutambua mbegu ya ukweli na hatimaye, kuiwezesha kufikia utimilifu wake!
Kwa njia ya wito wa uhuru, waamini wanagundua maana halisi ya utamadunisho wa Injili: Uwezo wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuheshimu na kuthamini kile kilicho kizuri na cha kweli katika tamaduni. Jambo hili si rahisi kwani kuna kishawishi cha “Kila mwamba ngoma, ngozi huivutia kwake.” Katika mchakato wa uinjilishaji, kumekuwepo na makosa yaliyotendeka, kiasi cha kulinyima Kanisa amana na utajiri kutoka katika tamaduni mahalia, kielelezo cha jamii ya watu husika. Huu ni mwelekeo ambao umekwenda kinyume kabisa na uhuru wa Kikristo! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Fumbo la Umwilisho limetangazwa na kufunuliwa na Kristo Yesu, chemchemi na kilele cha ufunuo wote. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho amewarejeshea wanadamu hadhi yao kuu, amejiunga kwa namna fulani na kila mwanadamu, akafanya kazi, akafikiri na kutenda kwa utashi na moyo wa kibinadamu, akazaliwa, na kufanana na binadamu katika yote isipokuwa katika dhambi! Rej. GS 22. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kuheshimu tamaduni za watu na kwamba, Kanisa Katoliki maana yake ni Kanisa ambalo liko wazi kwa ajili ya watu, tamaduni na nyakati zote, kwani Kristo Yesu ameteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya watu wote.
Tamaduni katika asili yake ni mchakato unaoendelea kubadilika, changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa nyakati hizi zenye mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia. Wakristo watambue kwamba, wamepokea zawadi ya uhuru ambayo wanapaswa kuilinda na kuendelea kujielekeza zaidi katika kuimwilisha, ili hatimaye, iweze kufikia utimilifu wake. Baada ya kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti, waamini wanapaswa kuendelea kusafiri kuelekeza utimilifu wa uhuru wa kweli! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtume Paulo alikuwa na ufahamu mkubwa wa Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu. Katika mawazo yake, anapaa zaidi na kuwaonesha waamini jinsi ya kufikiri na kutenda, wanapokabiliana na matatizo na changamoto za mipasuko ya kiimani ndani ya jumuiya. Mwishoni mwa Waraka huu, anazungumzia kuhusu Sheria na Msalaba wa Kristo na wale wote ambao wamekuwa ni viumbe wapya kwani wanachukua mwilini mwao chapa ya Kristo Yesu! Kutahiriwa kadiri ya mila na desturi za Kiyahudi lilikuwa ni jambo muhimu na utambulisho wao. Ni katika muktadha huu, Paulo Mtume aliamua kuzama zaidi ili kuubainisha ukweli wa Injili na uhuru wa Wakristo kama sehemu muhimu sana ya utambulisho wao. Mtume Paulo katika ufafanuzi wake, hakubaki juu juu tu, bali aliamua kuzama ndani zaidi ili hatimaye, kupata suluhisho la kudumu.