Hija ya Kitume ya Papa Francisko Barani Afrika: DRC Na S. Kusini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2021 alilitazama Bara la Afrika na kuyaelekeza mawazo yake nchini Ethiopia, ili waweze kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kweli, kwa kuguswa zaidi na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kuliko mambo mengine yote. Mtoto Yesu asikilize na kujibu kilio cha watu wa Mungu Ukanda wa Sahara wanaoteseka kutokana na vitendo vya kigaidi kimataifa. Kwa uso wake wenye huruma na mapendo, awaangalie watu wa Mungu, Kaskazini mwa Afrika, wanaoteseka kutokana na mipasuko, ukosefu wa fursa za ajira sanjari na ukosefu wa usawa kiuchumi. Mtoto Yesu, Mfalme wa amani, awaondolee mateso watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini na Sudan Kongwe. Awasaidie kukoleza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kukuza amali za kijamii zinazofumbatwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, maridhiano na amani katika nyoyo za watu wa Mungu Barani Afrika.
Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Noeli ni ukumbusho endelevu wa Fumbo la Umwilisho, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni muda muafaka kwa watu wote kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ukomavu wa imani na mshikamano wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Mchungaji John Chalmers, ambaye aliwahi kuwa Mchungaji mkuu wa Kanisa la Presibiterian huko nchini Scotland, walitoa salam na matashi mema ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 pamoja na Mwaka Mpya 2020 kwa viongozi wa kisiasa nchini Sudan ya Kusini.
Viongozi hawa wa kiroho waliwatakia wananchi wa Sudan ya Kusini amani ya kweli, ustawi na maendeleo na kwamba wako pamoja nao katika kipindi hiki cha mpito, kuelekea katika mchakato wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama sehemu ya utekelezaji wa Makubaliano ya Amani. Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wenzake, walimtolea sala na maombi yao Kristo Yesu, ili awasaidie kuendelea kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na udugu wa kibinadamu. Waliwaombea watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, heri, baraka na neema tele. Kristo Yesu, Mfalme wa amani, awaangazie na kuongoza hatua zao katika njia ya wema na ukweli, ili hatimaye, waweze kuzima ile kiu ya kutaka kutembelea Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko na Askofu mkuu Justin Welby walionesha nia ya kutembelea Sudan ya Kusini kwa pamoja, Mwenyezi Mungu akiweka mkono wake kunako mwaka 2020. Haikuwezekana!
Baba Mtakatifu aliendelea kuvuta subira, daima akiwa na matumaini kwamba, siku moja, ataweza kwenda Sudan ya Kusini, ili kuwaimarisha watu wa Mungu katika hija ya haki, amani na maridhiano, ili wote watambue kwamba, licha ya tofauti zao msingi, lakini ni watoto wa Baba mmoja, Mungu Baba Muumbaji. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kutembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, mjini Kinshasa na Goma tarehe 2-5 Julai 2022. Baba Mtakatifu anatarajia kutembelea Juba, Sudan ya Kusini tarehe 5-7 Julai 2022, matendo makuu ya Mungu. Ratiba nzima, itachapishwa kwa wakati muafaka lakini kwa sasa hii ndiyo habari ya “Mujini." Kwa hakika subira yavuta heri! Tumejipanga vizuri kukushirikisha awamu ya pili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika! Wajulishe na wengine, tuanze mchakato wa sala!