Papa Francisko tarehe 28 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Watu Asilia wa Canada. Muhimu: Ukweli, haki, uponyaji na upatanisho wa kitaifa. Papa Francisko tarehe 28 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Watu Asilia wa Canada. Muhimu: Ukweli, haki, uponyaji na upatanisho wa kitaifa. 

Papa Francisko Akutana na Baraza La Watu Asilia Wa Canada: Ukweli

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 28 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa watu 10 kutoka Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” Kikundi cha “Inuit” waliokuwa wamesindikizwa na baadhi ya Maaskofu Katoliki kutoka nchini Canada. Mambo muhimu: Ukweli, haki, uponyaji na mchakato wa upatanisho wa kitaifa ili kukuza haki msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” liliundwa kunako mwaka 1983 kwa lengo la kuragibisha haki msingi za watu asilia ndani na nje ya Canada. Hili ni Baraza ambalo limekuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kuragibisha haki msingi za Watu Asilia wa Canada mintarafu sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu pamoja na kuweza kujiendeleza wenyewe kama raia wa Canada. Hawa ni watu ambao wamekumbana na changamoto nyingi katika maisha yao nchini Canada hasa kutokana na sera za ubaguzi wa rangi katika sekta mbalimbali za maisha. Lakini hawa ni watu ambao wanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa mintarafu misingi ya haki, huku wakiwa na utambulisho wao wa kitamaduni, mapokeo na urithi wao. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 28 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa watu 10 kutoka Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” Kikundi cha “Inuit” waliokuwa wamesindikizwa na baadhi ya Maaskofu Katoliki kutoka nchini Canada. Baba Mtakatifu ametenga muda maalum wa kuwasikiliza wahanga wa ubaguzi wa rangi ili kutambua ukweli na hivyo kuanza mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, uponyaji na upatanisho wa kitaifa. Si rahisi sana kuweza kufuta mateso, machungu na changamoto walizokutana nazo katika historia na maisha yao. Jumuiya ya Watu Asilia nchini Canada inasema kwamba, ina uthibitisho wa makaburi ya wanafunzi 215 waliozikwa kwenye shule ya “British Columbia School”, moja ya shule zilizokuwa zimetengwa ili kutoa nafasi kwa wazawa kuweza kushiriki katika maisha ya jamii nzima.

Baraza la Watu Asilia wa Canada: Ukweli, haki, uponyaji na upatanisho
Baraza la Watu Asilia wa Canada: Ukweli, haki, uponyaji na upatanisho

Makaburi haya yamegunduliwa kwenye eneo la “Kamloops Indian Residential School” iliyofanya kazi zake kuanzia mwaka 1890 hadi mwaka 1970. Hawa ni wanafunzi waliopotea katika mazingira ya kutatanisha na wazazi na walezi wao hawakupatiwa maelezo ya kutosha. Shule kama hizi zilikuwa zinaongozwa na kuendeshwa na Makanisa nchini Canada. Tume ya Haki na Upatanisho wa Kitaifa nchini Canada inasema kuna zaidi ya wanafunzi 4, 100 waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. “Kamloops Indian Residential School” ni kati ya shule kubwa nchini Canada iliyokuwa inaongozwa na Kanisa Katoliki, ikiwa na wanafunzi zaidi ya 500 kabla ya Serikali kuanza kuingoza kunako mwaka 1969. Shule hizi kwa ajili ya wazawa nchini Canada zilipelekea mauaji ya kimbari. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”, 6 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema kwamba, alikuwa anafuatilia kwa uchungu mkubwa habari zilizokuwa zinamfikia kutoka Nchini Canada. Hii ni baada ya kugunduliwa kwa masalia ya wanafunzi 215 kutoka katika shule ya “Kamloops Indian Residential School” waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. Baba Mtakatifu ametia nia ya kutembelea Nchini Canada, lakini tarehe rasmi bado haijapangwa na kutangazwa rasmi.

Wajumbe wa Baraza la Watu Asilia wa Canada wakiwa mjini Vatican.
Wajumbe wa Baraza la Watu Asilia wa Canada wakiwa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu alipenda kuchukua fursa hii, kujiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada na watu wa Mungu nchini Canada katika ujumla wao, kuonesha uwepo wake wa karibu kutokana na habari hizi zinazohuzunisha na kutia simanzi moyoni. Baba Mtakatifu aliwahamasisha viongozi wa Serikali na Kidini nchini Canada kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili hatimaye, ukweli uweze kufahamika, na huo uwe ni mwanzo wa mchakato wa upatanisho na uponyaji wa kitaifa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na tabia ya ukoloni na hata ukoloni wa kiitikadi, kwa kutambua na kuthamini haki msingi za binadamu, tunu na amana za kitamaduni kwa watu wote wa Mungu nchini Canada. Baba Mtakatifu aliziweka nyoyo za marehemu watoto hao 215 chini ya huruma ya Mungu. Anaendelea kuiombea Jumuiya ya Watu Asilia nchini Canada ili iweze kupokea changamoto hii kwa moyo wa utulivu. Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” lina mshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutenga muda wake ili kusikiliza kilio chao cha ndani, ili kuanza hija ya ukweli, haki, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, dhamana inayopaswa pia kutekelezwa kwa makini katika ngazi ya mtu binafsi.

Canada
29 March 2022, 14:55