Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 30 ya Wagonjwa Duniani 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa na sala za Makuhani, Mama Kanisa huwakabidhi wagonjwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Mama Kanisa anawaalika wagonjwa na wazee kujiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo Yesu, ili kutoa mchango wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Rej. KKK. 1499. Mpako wa wagonjwa hutimiliza kufananishwa kwa waamini kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama Sakramenti ya Ubatizo inavyoanza. Siku ya Wagonjwa Duniani, ni wakati wa kusali na kuwaombea wagonjwa na familia zao; kwa kuwaenzi wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wanaojitolea usiku na mchana, kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wazee sehemu mbalimbali za dunia. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa huduma ya afya, ili kuweza kuwasindikiza wagonjwa na wanaoteseka katika shida na mahangaiko yao. Ni fursa kwa Kanisa kupyaisha tena na tena huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee.
Itakumbukwa kwamba, Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Hii ni siku maalum ambayo Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa wagonjwa bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali. Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee sehemu mbalimbali za dunia! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 30 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa tarehe 11 Februari 2022, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes unaongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Lk. 6:36: Kusimama karibu na wale wanaoteseka ni njia ya upendo.” Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Baba wa milele, mwaliko wa kugusa mahangaiko ya Kristo Yesu kwa njia ya wagonjwa.
Taasisi za huduma ya afya ni “nyumba za huruma” na kwamba kuna haja ya kujikita katika mpango mkakati wa uchungaji wa huruma, kwa uwepo na ujirani mwema. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sayansi ya tiba ya mwanadamu, lakini bado kuna changamoto kubwa kwa watu wanaoishi katika umaskini pamoja na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Wote hawa wanapaswa kusaidiwa ili kuunganisha magonjwa na mateso yao na yale ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mwanzoni maadhimisho ya Mwaka 2022 yalipangwa yaadhimishwe Kimataifa Jimbo Katoliki la Arequipa nchini Peru, lakini sasa maadhimisho haya yatafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama hamasa ya kujenga ujirani mwema na huduma kwa wagonjwa pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma.
Huruma ni jina na asili ya Mungu, inayo onesha nguvu na upendo; ulinzi na tunza ya Mungu inayowawezesha waamini kupata maisha mapya katika Roho Mtakatifu. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, uliomwezesha kutangaza, kushuhudia na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Akawatuma wafuasi wake kutangaza Ufalme wa Mungu na kupoza wagonjwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema uchungu mzito unamfanya mtu kujitenga na wengine, hali inayohitaji faraja kutoka kwa wengine. Wagonjwa mara nyingi ni watu wenye mioyo mizito, woga na wasi wasi kutaka kufahamu kwa haraka maana ya mambo yanayoendelea kujiri katika maisha yao. Haya ndiyo yanayowakumba hata leo hii waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambao wameonja huruma na upendo kutoka kwa wafanyakazi wa sekta ya afya mbali kabisa na uwepo wa ndugu na jamaa zao. Changamoto ni kuwa watu wenye huruma na divai ya faraja kwa madonda yanayowasibu wagonjwa.
Baba Mtakatifu anawakumbusha wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea kwamba, huduma yao kwa wagonjwa inavuka mipaka ya taaluma na kugeuka kuwa ni utume, unaoendeleza ile kazi ya Kristo Yesu, yaani wanawakuwa ni alama ya mikono ya huruma ya Baba wa milele, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanalinda sifa kubwa ya taaluma na wajibu wake. Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sayansi ya tiba ya binadamu, lakini jambo la msingi kuzingatia ni utu, heshima na haki msingi za wagonjwa. Wasikilizwe na kupatiwa tiba makini, pale inaposhindikana wafarijiwe kama kielelezo cha ujirani mwema. Wanafunzi katika sekta ya afya waelimishwe kusikiliza wagonjwa kwa makini sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano na wengine. Nyumba za huduma kwa wagonjwa na wazee, ziwe ni kielelezo cha “Nyumba za Msamaria mwema” na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wamisionari ambao wanatangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kutoa tiba kwa wagonjwa na tunza kwa wazee, watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo yenye mvuto na mashiko. Bado huduma ya afya kwa wengi ni safari ambayo itachukua muda mrefu na kwa baadhi ya watu, huduma ya afya kwa sasa imegeuka na kuwa kama anasa. Haya ndiyo yanayojitokeza hata katika ulimwengu mamboleo, kipindi hiki cha kutoa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna baadhi ya nchi maskini, bado zinaendelea kusuasua kupata chanjo. Nyumba za Msamaria mwema, ziwe ni mahali pa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia bado maskini na wagonjwa wanaendelea kunyanyasika na kubaguliwa. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika sera na uchungaji wa huruma, kama kielelezo cha uwepo katika huduma na ujenzi wa ujirani mwema.
Ubaguzi mbaya kabisa dhidi ya maskini ni ukosefu wa huduma za maisha ya kiroho yaani: baraka, Neno lake na Sakramenti za Kanisa. Rej. Evangelii gaudium, 200. Kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa ni sehemu muhimu sana ya huduma kwa wagonjwa na huu ni mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe. Huduma ya faraja ni dhamana na wajibu wa kila Mbatizwa, anayekumbushwa maneno ya Kristo Yesu aliyesema “Nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama.” Mt 25:36. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 30 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa tarehe 11 Februari 2022, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, kwa kuwaweka wagonjwa wote na familia zao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa. Anawakumbuka pia na kuwaombea wafanyakazi wote katika sekta ya afya, ili wakiwa wamesheheni utajiri wa huruma, waweze kuwahudumia wagonjwa kikamilifu, huku wakiwaonesha ujirani mwema unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu.