Tafuta

Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 ili kutambua mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Siku ya Watawa Ulimwenguni ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 ili kutambua mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. 

Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Watawa Ulimwenguni 2 Feb. 2022

Lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mungu kwa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena maagano yao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao. Pili ni kuragibisha maisha na utume wa watawa kwa ajili ya ustawi wa Kanisa zima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, tangu mwanzoni mwa maisha na utume wa Kanisa walikuwepo watu, wanaume na wanawake, ambao kwa kutekeleza mashauri ya kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Usafi kamili walinuia kumfuata Kristo kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, na walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu. Wengi miongoni mwao, kwa kufuata msukumo wa Roho Mtakatifu, waliishi maisha ya upweke, au walianzisha familia na jumuiya za kitawa, ambazo Kanisa kwa mamlaka yake lilizikubali kwa moyo wa upendo na kuziidhinisha. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 akaanzisha Siku ya Watawa Ulimwenguni inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari sanjari na Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Na kwa mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 26 ya Watawa Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 2 Februari 2022 majira ya Saa 11: 30 za Jioni kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 1: 30 kwa Saa za Afrika Mashariki, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 26 ya Watawa Ulimwenguni.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mungu kwa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena maagano yao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao. Watafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa mtumaini. Maisha ya kitawa ni kiini cha utume wa Kanisa, kinacholitajirisha Kanisa kwa karama mbalimbali za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Pili ni nafasi ya kuragibisha maisha na utume wa watawa kwa ajili ya mafao ya Kanisa zima pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao pamoja na kukoleza utakatifu wa maisha. Rej. LG 44. Hii ni siku ambayo watawa wanapaswa kumshangilia Mungu kwa ari na moyo mkuu kwa zawadi hii kubwa ambayo haina mbadala katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kurejea kwenye chemchemi ya miito yao, kutafakari kwa kina na mapana na hivyo kujiwekea malengo kwa siku za usoni.

Watawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Watawa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe Mosi, Februari 2015 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Watawa Duniani sanjari na hitimisho la Mwaka wa Watawa Ulimwenguni ambao uliliwezesha Kanisa kuonesha mn’gao wa uzuri na utakatifu wa maisha ya kitawa; majitoleo na furaha ya majibu ya wito wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watawa wameng’amua kwa uwazi zaidi utambulisho wao, tayari kusonga mbele huku wakiwa wamejikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha, ili kuandika kurasa safi zinazofuata nyayo za waanzilishi wa mashirika yao. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2021 kuna Mashirika 1, 900 ya Watawa wa Kike sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni changamoto ya kuendelea kuwa waminifu kwa wito na maisha ya kitawa; kukua na kukomaa katika upendo; sadaka na ugunduzi. Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu anapenda kuwaachia watawa zawadi ya maneno matatu muhimu: Unabii, Ujirani na Matumaini.

Baba Mtakatifu anasema Unabii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa watawa. Anawataka watawa kushuhudia ukweli wa Kimungu kwa njia ya maisha yao yanayoonesha mng’ao wa sura ya Mungu Baba mwingi wa huruma na mapendo na wala si mwepesi wa hasira. Ikiwa kama watawa watashindwa kukubalika na kupokelewa na watu wanaowahudumia, watambue kwamba, wameonesha sura yao na kuificha Sura ya huruma ya Mungu. Watawa wajenge na kuimarisha mahusiano na urafiki mwema na Mwenyezi Mungu; kwa kumwabudu katika ukimya, sala, tafakari ya kina na huduma ya upendo kwa maskini na wale wote ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa katika jamii. Baba Mtakatifu anawakabidhi watawa Ushuhuda wa udugu na ujirani mwema ambao umejidhihirisha kwa namna ya pekee kwa Mungu kujifunua kwa Kristo Yesu, akawa karibu na watu wote, akashiriki furaha na machungu ya watu wake; akabeba mabegani mwake magonjwa na mateso ya mwanadamu, ili kuwa ni fidia kwa wengi.

Watawa wanalitegemeza Kanisa kwa sala na sadaka zao.
Watawa wanalitegemeza Kanisa kwa sala na sadaka zao.

Kumfuasa Kristo ni kujitahidi kufuata nyayo zake kama Msamaria mwema, tayari kuwaganga na kuwaponya waliojeruhiwa; kuonesha ujirani mwema ili kushiriki furaha na mahangaiko ya watu ili hatimaye, kuwaonjesha upendo na sura ya huruma ya Baba wa milele pamoja na upendo wa Mama Kanisa. Asiwepo mtu anayewaona kuwa ni watu wa kuja, wageni, wapita njia, au: “Vyasaka” “Wanyamahanga”, au “watu pori.” Kila mtawa anaitwa kuhudumia mintarafu karama ya shirika lake: katika sala, katekesi, elimu, afya na matendo ya huruma; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ili kuishi kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu anawahimiza watawa kuwa ni mashuhuda wa Matumaini ya huruma ya upendo wa Mungu, ili kuwaonjesha walimwengu matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaoogelea katika kinzani, woga, wasi wasi na hali ya kukata tamaa. Watawa wawaonjeshe heri za mlimani, uaminifu na huruma; wema, kiasi na kujikita katika mambo msingi na yenye maana katika maisha ya watu.

Watawa wawe ni chachu ya matumaini ndani ya Kanisa, kwa kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene hata na watawa wa Makanisa mengine ya Kikristo. Watawa washuhudie na kumwilisha karama za mashirika yao katika mitindo mbali mbali ya maisha, huku wakikuza na kudumisha umoja, ushiriki na utume, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, katika utume wao kamwe wasiongozwe na umri au idadi yao, bali wawe na ujasiri wa kuitikia wito wao kila siku ya maisha, ili kuweza kupyaisha matumaini yao. Unabii, ujirani na matumaini ni mambo yatakayojaza furaha mioyo yao, kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo, mvuto na mashiko kwa watu wengi zaidi kwa ajili ya utukufu wa Mungu na uzuri wa Kanisa, mchumba wa Kristo.

Siku ya 26 Watawa
01 February 2022, 09:06