Pongezi Kwa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama Mjini Vatican: Huduma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 3 Februari 2022 amekutana na kuzungumza na vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican na kwa namna ya pekee, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia kwa ushirikiano mwema na Vatican katika ari na moyo wa huduma. Amevishukuru vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza majukumu yake mjini Vatican kwa kuzingatia taaluma, weledi na maadili ya kazi, kiasi kwamba, shughuli mbalimbali za Ibada na Utalii mjini Vatican zimeendelea kwa amani na utulivu. Hawa ni waamini na mahujaji wanaotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya Sala na Ibada bila kuwasahau wageni wanaokwenda kuonana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vyombo ambavyo vimetoa ulinzi na usalama hata kwa waamini wanaofanya maandamano yao kuzunguka Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni kazi nyeti na tete inayohitaji uelewa makini, uvumilivu na uwepo wao karibu. Hivi ni vikosi vinavyoshughulikia safari na hija mbalimbali zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro Jijini Roma na Italia katika ujumla wake. Anawashukuru kwa umoja na ushirikiano kati yao na Vikosi vya Ulinzi wa Papa mjini Vatican maarufu kama “Swiss Guards.” Baba Mtakatifu baada ya kuwapongeza, amewashukuru kwa huduma wanayoitoa kwa kusukumwa na utashi wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao; sanjari na utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mambo muhimu sana kwa Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni ambayo imeadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 2 Februari 2022, kwamba, ni Sikukuu ya watu kukutana.
Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na Mtoto Yesu wanakutana na Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli. Hawa ni watu wa vizazi tofauti wanaokutana na kati kati yao yuko Kristo Yesu. Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama katika kutekeleza dhamana na wajibu wao, wanatoa nafasi kwa watu kuja mjini Vatican wakiwa na lengo la kukutana na Kristo Yesu ambaye alipokelewa kwa mikono miwili na wazee hao wanaotajwa katika Maandiko Matakatifu. Kwa huduma yao makini, wanawawezesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumpokea Kristo Yesu katika maisha yao. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko, amewaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, waliompeleka Mtoto Yesu hekaluni. Ameweka pia matumaini, wasiwasi na hofu zao zinazofichama nyoyoni mwao kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu na kwamba, anachukua fursa hii kuwahakikishia sala zake kwa wao wenyewe, familia pamoja na marafiki zao.
Kwa upande wake, Kamanda Lamberto Giannini, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican ameelezea historia ya Vikosi hivi vilivyoanzishwa na Papa Pio XII kunako mwaka 1945, ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, waamini na watu wenye mapenzi mema wanapotembelea mjini Vatican, kiini cha imani na Ukristo. Katika kipindi cha miaka miwili, tangu kuibuka kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, mazingira ya kazi yamekuwa ni magumu sana kutokana na changamoto mpya zilizoibuka. Kazi hii kwa sasa inahitaji upyaisho shirikishi kihali na katika maisha ya kiroho. Kwa watu kufungiwa kwenye karantini, Maaskari walijikuta wakiwa pweke kulinda maeneo matakatifu ya Sala na Ibada.
Umekuwa wakati wa kuomba huruma na upendo wa Mungu kwa ajili ya walimwengu. Askari hawa ni mashuhuda wa umaskini wa hali na kipato unaowazunguka watu wengi ambao wengi wao ni wagonjwa na wenye kuhitaji ulinzi na usalama, matumaini na faraja katika mahangaiko yao. UVIKO-19 umepelekea madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya jamii, lakini mbaya zaidi ni katika masuala ya kiuchumi na kijamii; ongezeko kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Huduma hii yote imetekelezwa kwa kulipa gharama kubwa kwa kuwa mbali na familia zao. Lakini, daima wako tayari kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na hasa wale maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.