Papa Francisko: Mauaji ya Padre Richard Kasereka Ni Ukatili Mkubwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Padre Richard Masivi Kasereka, wa Shirika la Mapadre wa Adorno “Order of the Clerics Regular Minor” aliyekuwa anajiandaa kuadhimisha kumbukizi la miaka 36 ya kuzaliwa kwake, tarehe 2 Februari 2022 aliuwawa kikatili huko Kivu Kaskazini, nchini DRC na majambazi waliokuwa na silaha. Padre Richard Masivi Kasereka alikuwa anarejea Parokiani kwake, baada ya kuadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya 26 ya Watawa Ulimwenguni, iliyosherehekewa huko Kanyabayonga, Jimbo Katoliki la Butembo Beni, nchini DRC. Padre Richard Masivi Kasereka baada ya majiundo yake ya kitawa na masomo kwenye Chuo Kikuu cha Tangaza, Nairobi hadi mwaka 2018, mwezi Februari 2019 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre. Na tangu tarehe 31 Oktoba 2021 alikuwa akitoa huduma za kichungaji kwenye Parokia ya Malaika mkuu Mikael.
Padre Richard Masivi Kasereka, anakumbukwa na wengi kutokana na ucheshi na huduma zake kwa watu wa Mungu Parokiani hapo, bila kusahau majitoleo yake kwa kuambata mashauri ya Kiinjili kama mtawa. Tarehe 5 Februari 2022, ikaadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Padre Richard Masivi Kasereka, wa Shirika la Mapadre wa Adorno, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kumstahilisha kufika mbinguni na hatimaye kushiriki maisha na uzima wa milele. Damu ya mashuhuda wa imani inayoendelea kumwagika sehemu mbalimbali za dunia, iwe ni mbegu kwa ajili ya kukua na kukomaa kwa Kanisa la Mungu. Itakumbukwa kwamba, tarehe 1 Februari 2022 wanamgambo wenye silaha walivamia Kambi ya Wakimbizi na Wahamiaji ya Ipuri na kupelekea watu 62 kupoteza maisha yao.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhitimisha Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Mwombezi wa Kanisa la Kiulimwengu, amewasalimia Mapadre wa Shirika la Adorno na kuyaelekeza mawazo yake kwa Padre Richard Masivi Kasereka aliyeuwawa kikatili tarehe 2 Februari 2022 huko Kivu ya Kaskazini. Huu ni ukatili wa hali ya juu na unaosikitisha. Lakini, kifo chake kisiwakatishe tamaa ndugu, jamaa, jumuiya ya Kikristo na watu wa Mungu katika ujumla wao nchini DRC. Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto kubwa kwa sasa ni kwa watu wote wa Mungu kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa wema na udugu wa kibinadamu, licha ya matatizo na changamoto wanazokumbana nazo. Wajitahidi kumuiga Kristo Yesu, Mchungaji mwema.