Tafuta

Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre 17-19 Februari 2022. Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre 17-19 Februari 2022. 

Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre 2022

Mapokeo ya Kanisa yawasaidie watu wa Mungu kung’amua mapenzi ya Mungu katika maisha yao bila woga wala wasi wasi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuzingatia misingi mikuu minne itakayowasaidia kujenga ujirani mwema na Mwenyezi Mungu, Askofu mahalia, Urika wa Mapadre pamoja na Watu wa Mungu katika ujumla wao, ili kukoleza miito ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 17 Februari 2022 amefungua Kongamano la Kimataifa Kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre. Katika hotuba yake elekezi amewashirikisha wadau wa kongamano ushuhuda wa maisha na utume wake wa Kipadre kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Anasema Mapokeo ya Kanisa yawasaidie watu wa Mungu kung’amua mapenzi ya Mungu katika maisha yao bila woga wala wasi wasi. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuzingatia misingi mikuu minne itakayowasaidia kujenga ujirani mwema na Mwenyezi Mungu, Askofu mahalia, Mapadre pamoja na Watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hotuba yake inafumbata uzoefu na mang’amuzi ya maisha na wito wake wa Kipadre kwa zaidi ya miaka 50 kwa kupitia hali na mazingira mbalimbali, lengo likiwa ni kuwasaidia Mapadre kuishi katika amani na utulivu ili waweze kuzaa matunda kadiri ya uwezo wa Roho Mtakatifu. Hiki ni kipindi cha kihistoria ambacho, kinawataka watu wa Mungu kukubali na kupokea mabadiliko katika maisha kama inavyojitokeza katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, daima kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati, ili kukubali na kupokea mabadiliko yanayokita mizizi yake katika tunu msingi za Kiinjili, bila kukumbatia sana mambo yasiyokuwa na mvuto wala mashiko.

Kamwe Mapadre wasiwe na matumaini wala ndoto kubwa zinazoelea kwenye ombwe. Mitazamo hii miwili, kamwe haiwezi kuwapatia suluhu ya matatizo na changamoto zinazowaandama katika maisha na wito wao wa Kipadre. Baba Mtakatifu anasema, Mapokeo ya Kanisa yawawezeshe Mapadre kufanya mang’amuzi ya mapenzi ya Mungu katika maisha yao bila woga wala wasi wasi kwani historia ya Kanisa imetukuka hasa kwa sababu ni historia ya kujisadaka, matumaini na mapambano ya kila siku sanjari na maisha ya sadaka katika huduma na uaminifu katika utume ingawa yataka moyo kweli kweli. Rej. Evangelii gaudium, 96. Mapadre katika maisha na utume wao wanakabiliwa na changamoto pevu, inayowataka Mapadre kujisadaka kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko ili kuchochea miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Watu wanataka kuona ushuhuda wa sadaka, furaha na maisha ya udugu katika jumuiya, ili kuwafanya Wakleri na Watawa kujisadaka zaidi kwa Mungu na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ushuhuda wa jumuiya inayosali na kuwajibikiana ni mfano mzuri kwa vijana wanaotamani kuingia katika wito wa Upadre. Wito wa kwanza wa kila mbatizwa ni utakatifu wa maisha, kwa kumpenda Kristo Yesu na kuendelea kuinjilishwa.

Wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha
Wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha

Kila wito unapaswa kufanyiwa mang’amuzi ya kina, chemchemi ya matumaini katika kipeo hiki cha ukavu wa miito ya Kipadre na Kitawa ndani ya Kanisa. Hii ni changamoto inayopata chimbuko lake hata katika maisha na utume wa familia. Ikumbukwe kwamba, miito yote ndani ya Kanisa inapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Katika ulimwengu mamboleo kuna fursa, changamoto na vishawishi vingi katika maisha na utume wa Kipadre. Kumbe, watu wa Mungu wajitahidi kujijenga na kujiimarisha kwa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu, huku wakitambua kwamba, wao ni mahekalu matakatifu ya Mungu yanayosimikwa katika nguzo kuu nne zinazojenga ujirani mwema, msingi wa mahusiano ya ujirani na Mwenyezi Mungu, Askofu mahalia, urika wa Mapadre pamoja na ujirani mwema na watu wa Mungu katika ujumla wao.

Kuhusu msingi wa ujirani mwema na Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu anasema, Padre anahitaji nyenzo msingi ili aweze kutekeleza dhamana na wito wake wa kila siku kwa kupiga vita kiaminifu kwa ajili ya Injili. Silaha hizi ni nguvu ya upendo na moyo wa kiasi. Rej. 2 Tim 1:6-7. Watambue kwamba, wao ni matawi na Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli, kumbe wanapaswa kuzama katika Neno la Mungu na maisha ya sala na kwa njia hii kamwe Padre hataweza kujisikia kuwa mpweke katika maisha na utume wake. Wajenge na kuimarisha imani na upendo wao kwa Kristo Yesu na kuendelea kupambana, ili kupata baraka zake, chemchemi ya maisha kwa wengi. Ukavu wa maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni chanzo cha Mapadre wengi kutumbukia katika upweke hasi na migogoro ya miito ya Kipadre. Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu ni mambo yanayojenga ujirani mwema na Mwenyezi Mungu. Padre anayesali anaguswa na shida, mahangaiko na changamoto za watu wake na hivyo kumwezesha kuwa karibu zaidi na watu wake, kiasi cha kujifungamanisha na watu wake kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mapadre wajenge ujirani mwema na Maaskofu mahalia, kwa njia ya utii na ushirika; kwa kusikiliza na kutenda kwa uaminifu na uadilifu, ukweli, uwazi na maisha, badala ya Mapadre kujifungia katika ubinafsi wao. Kwa njia hii, Mapadre watakuwa na uwezo wa kufanya mang’amuzi kuhusu mapenzi ya Mungu katika maisha yao na kwamba, Askofu mahalia ni chombo cha mang’amuzi haya. Baba Mtakatifu anasema katika mawasiliano, wajitahidi kujenga utamaduni wa kusikiliza, ili kujenga ukaribu, ili kupata maneno sahihi na ushiriki mkamilifu. Hii ni sanaa inayojengwa kwenye heshima na huruma, ili kukua kiukweli na hivyo kuamsha shauku ya mfano bora wa Kikristo, tamaa ya kuuitikia kikamilifu upendo wa Mungu, ili kuzaa matunda ya kweli katika maisha. Rej. Evangelii gaudium, 171. Askofu mahalia ajitahidi kujenga na kudumisha ushirika kati ya Padre na Jimbo husika. Utii kwa Kanisa ni kielelezo halisi cha Kanisa kama Sakramenti ya wokovu kwa watu wote. Utii inaweza kuwa ni fursa ya kuweza kukabiliana uso kwa uso, kusikiliza na hata wakati mwingine kuna kuwepo na kinzani. Maaskofu wanapaswa pia kuonesha unyenyekevu, uwezo wa kusikiliza, kujikosoa na kujiruhusu kusaidiwa na wengine.

Kongamano la Kimataifa kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre
Kongamano la Kimataifa kuhusu Taalimungu Msingi ya Upadre

Mapadre wajenge ujirani mwema katika urika wa Mapadre, kwa kudumisha udugu wa kibinadamu, ili kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja. Mapadre wajifunze kuwa na saburi na uvumilivu kwa kusaidiana na kutaabikiana; kwa kushirikiana na kushikamana, bila kugeuziana “kisogo”, hali inayoweza kuwatumbukiza baadhi ya Mapadre katika upweke hasi. Wajenge tabia ya wema na kuepukana na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Kila mtu ajisikie kuwa ni sehemu ya Jumuiya na kamwe asiwepo ambaye anatengwa kwa sababu yoyote ile; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja wanaojipambanua kwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Wajitahidi kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na wala si masilahi binafsi. Wawe wepesi kusamehe na kusahau na kamwe wasitumbukie katika kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi. Wawe ni watu wenye upendo unaosimikwa katika ukweli na haki.

Jumuiya iwe ni mahali pa kupambana na maisha ya kiroho, kwa kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Upendo wa kidugu uwe ni utambulisho wao kwamba, kweli ni wafuasi wa Kristo Yesu. Upendo huu unapaswa kumwilishwa katika shughuli za kichungaji, ili kukuza urafiki wa kweli. Useja ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa la Kilatini, zawadi inayopaswa kuchukuliwa kuwa ni chachu ya utakatifu kwa kujikita katika mahusiano bora, kwa kuheshimiana na kutakiana mema yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Bila sala na marafiki wa kweli useja, utakuwa ni “zigo zito” lisiloweza kubebeka hata na “Wanyamwezi” na hivyo kuwa ni kinyume kabisa cha ushuhuda, utakatifu na uzuri wa maisha na wito wa Kipadre.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kujenga ujirani mwema na watu wa Mungu, ili kukoleza utamu wa kiroho wa kuwa Taifa la Mungu, ili kuwa kweli ni chemchemi ya furaha. Utume ni uchu kwa ajili ya Kristo Yesu na waja wake kwa wakati mmoja. Upendo wa Kristo Yesu unawainua na kuwategemeza Mapadre, ili kuwakumbatia na kuwaambata watu wote wa Mungu. Kristo Yesu anawatumia ili kuwavuta wote kwake. Anawateuwa kutoka katikati ya watu na kuwatuma kwa waja wake ili kujenga familia moja ya watu wa Mungu kama utambulisho wao wa ndani kabisa. Rej. Evangelii gaudium, 268. Ujirani mwema na watu wa Mungu, uwasaidie Mapadre kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu miongoni mwa waja wake, kwa kujitahidi kuwa ni Wasamaria wema, tayari kuwaganga watu wa Mungu kwa mafuta ya faraja na divai ya upendo. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mtandao wa upendo na mshikamano wa watu wa Mungu kwa kutambua nafasi ya Kanisa katika historia, kwa kuendelea kujitamadunisha, kuinjilisha kwa kusikiliza kwa makini na kuzifafanua sauti mbalimbali zinazosikika katika nyakati hizi katika mwanga na kweli za Kiinjili. Kanisa linapaswa kutambua kwamba, lina utume maalum ambao linapaswa kuutekeleza hapa duniani. Huu ni wakati wa kupima misingi ya ujirani mwema, katika sala, tafakari, Sakramenti za Kanisa na huduma makini kwa watu wa Mungu. Ujirani mwema ni zawadi bora sana katika mchakato wa kukuza na kustawisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Mapadre wajifunze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na wema wa Mungu kwa waja wake.

Papa Wito wa Upadre

 

 

17 February 2022, 15:13