Papa Francisko Wahudumieni Vipofu kwa Wema Na Upendo Wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni mwaka 1927, huko mjini Lione, nchini Ufaransa, Padre Yves Mollat, S.J. aliyekuwa kipofu alipoanzisha vuguvugu la wanaharakati waliogeuka baadaye na kuanzisha Chama cha Kitume cha “Voir Ensemble” yaani “Kuona kwa Pamoja” kunako mwaka 1947. Chama hiki kikajielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Jina la “Voir Ensemble” lilianza kutumika rasmi kunako mwaka 2003 kwa lengo la kusimamia haki msingi, utu, heshima, maendeleo, ustawi na mafao ya vipofu. Ni Chama cha kitume kinachopania kuwaendeleza vipofu: Kiakili, kijamii, kiutu, kitamaduni, kihali na kielimu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata pia fursa za ajira ili kuweza kuboresha maisha yao ndani na nje ya Ufaransa. Ni katika muktadha wa kumbukizi la Miaka 90 ya huduma ya mshikamano na upendo unaowasukuma wanachama hawa “kuona kwa pamoja”, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican tarehe 19 Februari 2022.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewashukuru na kuwapongeza kwa kujenga na kuimarisha udugu wa mshikamano ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga, kwa kutoa nafasi kwa Kristo Yesu, ili aweze kuwaganga na kuwaponya, ili hatimaye, waweze kuona kwa jicho la moyo! Baba Mtakatifu amechota ujumbe wa tafakari yake kutoka katika sehemu ya Injili ya Yohane kwa Kristo Yesu kumponya mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Yn 9:1-41. Kristo Yesu alimwangalia kipofu huyu kwa jicho la huruma, upendo na udugu wa kibinadamu. Kuna watu wengi waliokutana na kipofu yule tangu kuzaliwa kwake, lakini hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kumwonea huruma, badala ya kuanza kumhukumu kwamba, upofu wake ni matokeo ya kuzaliwa katika dhambi, kielelezo cha adhabu ya Mungu na mtazamo finyu unaowatenga, kuwabeza na hatimaye kuwasukumizia pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.
Huu ni utamaduni unaojikita katika maamuzi mbele, lakini Kristo Yesu anaupatia mwelekeo mpya kwa kusema kwamba kipofu huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake, bali haya ni maradhi tu yamemkuta katika maisha yake. Ni maneno yanayobeba ndani mwake, uhuru, ukarimu na ukombozi kamili. Kwa bahati mbaya watu wengi wanavutika kuangalia mambo ya nje tu, lakini kwa kukutana na Kristo Yesu, waamini wanapata fursa ya kuwa na mwanga mpya wa maisha na imani, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu msingi wa udugu wa kibinadamu ndani ya Kanisa na katika jamii. Mchakato wa uponyaji unaotendwa na Kristo Yesu ni kielelezo cha matendo makuu ya Mungu yanayosimikwa katika huruma na mapendo, chemchemi ya faraja, tiba na uponyaji, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa vyombo na mashuhuda wa huduma ya puponyaji na afya bora, kwa wale wote wanaohitaji msaada wao wa hali na mali.
Kipofu tangu kuzaliwa kwake, alibahatika kukutana na Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa, akapewa zawadi ya kuweza kuona, lakini wale waliomzunguka wakatumbukia katika upofu kiasi cha kushindwa kuona matendo makuu ya Mungu katika maisha ya huyu mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi kuwaangalia watu wanaoteseka kwa jicho la huruma na upendo wa Kimungu. Huu ni mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya na mpana zaidi kwa watu na vitu, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika familia na ubinadamu huu unaokabiliwa sana na magonjwa pamoja na kifo. Imani iwasaidie waamini kutembea katika mwanga wa Kristo, kwa kuwa na jicho la huruma na upendo, ili hatimaye, waamini wote waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, mwanga wa Mataifa kama alivyotangaza na kushuhudia yule mtu aliyezaliwa kipofu baada ya kuzongwa zongwa na watu, akawaondolea uvivu na hivyo kuungama imani yake kwa kusema “Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona” Yn 9:25. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa, kwa kujikita katika ukarimu na udugu wa kibinadamu, ili kuwakirimia wagonjwa na maskini mwanga mpya wa maisha na matumaini.