Tafuta

Papa Francisko na Patriaki wa Kiekumene Bartholomew I  (Vatican Media) Papa Francisko na Patriaki wa Kiekumene Bartholomew I (Vatican Media) 

Papa Francisko ampongeza Patriaki wa Bartolomeo I wa Constantinople

Papa Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video akimpongeza Patriaki wa Kiekumene Bartholomew wa Kwanza,kwa maadhimisho ya miaka thelathini ya huduma kama Askofu Mkuu wa Constantinople na kumtakia miaka mingi:"Chrónia pollos! Ad multos annos!"

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Alhamisi tarehe 10 Februari 2022, Papa Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kumpongeza Patriaki wa Kiekumene Bartholomeo wa Kwanza, katika fursa ya kuadhimisho miaka thelathini tangu achaguliwe kuwa kama Askofu Mkuu wa Constantinople na kumtakia miakamingi kwa kutumia maneno ya Kigiriki na kilatino: “Chrónia pollos! Ad multos annos! Papa Francisko akianza ujumbe wake amesema “Ninafurahi sana kwamba maadhimisho ya miaka thelathini ya kuchaguliwa kwa rafiki yangu na kaka Bartholomeo kuwa Patriaki wa Jimbo la kale na tukufu la Constantinople inaadhimishwa na wengi ambao wametaka kumshukuru Bwana kwa ajili ya maisha na huduma yake”.

Urafiki ulizaliwa yangu kuanza kwa upapa 

Papa Francisko ameelezea uelewa mzuri wa kibinafasi kati yao kwamba ulizaliwa tangu siku ile ya Papa kuanza huduma yake ya kipapa, alipofanya heshima ya uwepo wake jijini Roma, na baadaye kuendelea kukomaa katika urafiki huo wa kidugu katika makabiliano mengi ambayo, kwa miaka mingi, wamekuwa nayo, si hapa Roma tu, bali pia huko Constantinople, Yerusalemu, Assisi, Cairo, Lesvos na Bari. Papa Francisko amebainisha kwamba kinachowaunganisha na Patriaki Bartholomeo ni ufahamu wa pamoja wa wajibu wao wa pamoja kichungaji kuelekea changamoto za dharura ambazo familia nzima ya binadamu inapaswa kukabiliana nazo leo hii. 

Shukrani wa jitihada za Patriaki kilinda kazi ya Uumbaji

Papa Francisko ameongeza kusema kwamba “Ninashukuru kwa dhati kwa juhudi za Patriaki wa Kiekumene katika kulinda kazi ya uumbaji na kwa tafakari yake juu ya somo hilo, ambalo nimejifunza na ninaendelea kujifunza mengi. Pamoja na kuzuka kwa janga linaloendela na kuenea kwa athari zake za kiafya, kijamii na kiuchumi, ushuhuda wake na mafundisho yake juu ya uongofu muhimu wa kiroho wa mwanadamu umepata umuhimu zaidi”.

Mazungumzo kama njia pekee ya upendo kufikia upatanisho kati ya waamini katika Kristo

Baba Mtakatifu Francisko aidha amesema zaidi ya hayo, Patriaki Bartholomeo ameonesha bila kukoma mazungumzo, katika upendo na kweli, kama njia pekee iwezekanayo ya upatanisho kati ya waamini wote katika Kristo na kwa ajili ya kuanzishwa tena kwa umoja wao kamili. Papa ameongeza: “Katika njia hii hakika tunataka kuendelea kutembea pamoja. Ni imani yetu sote kwamba ukaribu na mshikamano kati yetu Wakristo na kati ya Makanisa yetu ni mchango wa lazima kwa ajili ya udugu wa kidunia na urafiki wa kijamii, ambapoubinadamu unahitaji kwa haraka ”.

χρόνια πολλά! Ad multos annos!

Hatimaye Papa Francisko kwa lugha ya Kigiriki na Kilatini katika utamadauni wa kuakiana matashi mema amesema: “Kwa hisia hizi, ninapenda kueleza mashi yangu ya dhati kwa ajili ya kumbukumbu yako Patriaki Bartolomeo, nikimwomba Mungu akupe afya, utulivu, na furaha ya kiroho na uniruhusu nisema kwa maana ya ucheshi: zaidi! Utakatifu wako, ndugu mpendwa katika Kristo, χρόνια πολλά! [Chrònia Pollà!]"Ad multos annos!

UJUMBE WA PAPA KWA PATRIAKI BARTOLOMEO I
10 February 2022, 17:47