Tafuta

Papa ameomba kushiriki sala na kufunga Machi 2 kwa ajili ya Ukraine

Jumatano 23 Februari 2022 mara baada ya Katekesi Papa Francisko aliwaalika waamini wajitolee kwa pamoja ili katika siku ya kwanza ya Kwaresima kusali na kufunga kwa ajili ya amani barani Ulaya kwa namna ya pekee nchini Ukraine.Papa alisema:“Mungu ni baba wa wote,si mtu tu,anatutaka tuwe ndugu na si maadui”.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Februari 2022 kwa waamini na mahujaji waliokuwa wameunganika katika ukumbi wa Paulo VI, jijini Vatican alionesha uchungu moyoni kwa ajili ya hali halisi kuongezeka kwa mivutano  huko Ukraine.  Katika salamu zake, alotoa wito mpana kwa ajili ya amani ulimwenguni  ambapo hakuweza kuficha wasi wasi wake na kujutia matokeo mabaya ya mazungumzo ya kimataifa ambayo hadi wakati huo yalikuwa  yamefanyika bila kuleta mafanikio.

Mazungumzo ya Kidiplomasia

“Licha ya juhudi za kidiplomasia za wiki chache zilizopita hali zinazozidi kutisha zinafunguka. Kama mimi, watu wengi duniani wanakabiliwa na uchungu na wasiwasi. Kwa mara nyingine tena, amani ya kila mtu inatishiwa na maslahi ya upande”. Papa Francisko ameendelea: “Nitoe wito kwa wale wenye majukumu ya kisiasa wachunguze kwa kina dhamiri mbele za Mungu, ambaye ni Mungu wa amani na si wa vita, Baba wa wote, sio tu wa mtu anayetaka tuwe ndugu na si maadui. Ninaomba pande zote zinazohusika zijiepushe na kitendo chochote kinachosababisha mateso zaidi kwa watu, kudhoofisha kuishi pamoja kati ya mataifa na kudharau sheria za kimataifa”.

Waamini wajitoe kusali na kufunga siku ya majivu, tarehe 2 Machi 2022  

Papa Francisko anaelewa wazi kuwa siasa haitoshi kubadili mioyo,ni Mungu peke yake ambaye anaweza kufanya hivyo na hivyo amewaalika waamini na wasio waamini kuunga katika maombi ya pamoja kwa ajili ya amani. Kwa maana hiyo amesema:  “Yesu alitufundisha kwamba upumbavu wa kishetani wa vurugu unajibiwa kwa silaha za Mungu, kwa maombi na kufunga. Ninawaalika kila mtu kuifanya hiyo tarehe 2 Machi ijayo, ambayo ni Jumatano ya Majivu, iwe siku ya kufunga kwa ajili ya amani. Ninawatia moyo  hasa waamini kujitolea sana kwa ajili ya maombi na kufunga siku hiyo. Malkia wa Amani alinde ulimwengu dhidi ya wazimu wa vita”, alisisitiza Papa.

Kile ambacho alikuwa amesema, na sasa kimekuwa, hivyo kuna haja ya kusali na kama Kardinali Pietro parolin alivyosema kuwa “Mbele ya kuongezeka kwa  mgogoro wa Ukraine, maneno ya Baba Mtakatifu aliyotamka jana baada ya Katesi yake, yanasikika kabisa kwa dhati”.  Papa alionesha “uchungu mkubwa, huzuni na wasiwasi”. Na aliwaalika sehemu zote husika zijiepushe na kitendo chochote kinachosababisha mateso zaidi kwa watu, kudhoofisha kuishi pamoja kati ya mataifa na kudharau sheria za kimataifa”. Na kuongeza kuthibitisha kuwa: “Sisi waamini hatupotezi matumaini juu ya mwanga wa dhamiri ya wale ambao wana hatima za ulimwengu mikononi mwao. Na tunaendelea kuomba na kufunga Jumatano ijayo ya Majivu kwa ajili ya amani nchini Ukraine na ulimwenguni kote”.

25 February 2022, 09:25