Mwenyeheri Padre Gaetano Giménez Martín na Wenzake 15: Mashuhuda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 26 Februari, huko Granada, Hispania, amemtangaza Padre Gaetano Giménez Martín, na wenzake kumi na tano waliouwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani (Odium fidei) wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania kati ya mwaka 1936 hadi mwaka 1939 kuwa wenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 27 Februari 2022 amewakumbuka, mashuhuda hawa wa imani kwa uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamshe ndani ya waamini ile ari na mwamko wa kuhudumia Injili kwa uaminifu na ujasiri.
Kwa upande wake, Kardinali Marcello Semeraro, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema akisema, “Kwa moyo safi, na tuimbe sifa za mashuhuda watakatifu, ambao shauku iliyobarikiwa imewafanya kuwa sawa na Kristo Yesu Mfufuka. “Laudes sanctorum martyrum – quos sacra fecit passio – Christi conformes gloriae – puris canamus cordibus” (PL 86, 1003). Hawa ni Wakristo walioonesha ushupavu, wakasimama kidete kuhusu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kiasi hata cha kuthubutu kuyamimina maisha yao, kiasi kwamba, damu yao imekuwa ni mbegu ya Ukristo. Walikipokea kifo kama zawadi na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni kifo na mateso ambayo yamewastahilisha ushindi na maisha ya uzima wa milele. Wamekuwa kama chembe ya ngano iliyoanguka katika nchi, ikafa, ili iweze kutoa mazao mengi.Rej. Yn 12: 24. Mababa wa Kanisa wanasema,damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo “Semen est sanguis christianorum.”
Kardinali Marcello Semeraro anakaza kusema, utakatifu wa mashuhuda wa imani si jambo lililopitwa na wakati, bali ni neema na baraka kwa Kanisa la Kristo Yesu; msingi na nguzo thabiti katika hija ya maisha ya uzima wa milele. Mashuhuda hawa wametakaswa dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu kwa mateso na hatimaye, kifodini na sasa ni waombezi wakuu wa Kanisa linaloendelea kusafiri huku bondeni kwenye machozi. Wanawasaidia na kuwaongoza waamini katika safari ya maisha yao, mwaliko kwa waamini kuwakimbilia kwa maombezi yao, ili hata wao waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu anaendelea kuishi kati ya Mashuhuda wake wa imani. “Christus in martyres est.”