Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Babu, Bibi, Wajukuu na Wazee kwa Mwaka 2022 yanaongozwa na kauli mbiu: “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee” Zab 92:14. Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Babu, Bibi, Wajukuu na Wazee kwa Mwaka 2022 yanaongozwa na kauli mbiu: “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee” Zab 92:14.  

Maadhimisho Siku ya Pili ya Babu, Bibi na Wajukuu 24 Julai 2022

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Wazee Duniani anasema yananogeshwa na kauli mbiu: “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee” Zab 92:14. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria. Ni siku ya kuenzi utu na heshima

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Dominika ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu, Siku ya Pili ya Wazee Duniani inaadhimishwa Dominika tarehe 24 Julai 2022. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni: imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahaulika sana na hatimaye, kusukumizwa pembezoni mwa jamii utadhani kana kwamba, wao wamekuwa ni “daladala bovu.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Pili ya Wazee Duniani anasema yananogeshwa na kauli mbiu: “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee” Zab 92:14. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria.

Madhumuni ya ujumbe huu anasema Baba Mtakatifu ni kukoleza mchakato wa majadiliano kati ya vizazi, lakini kwa namna ya pekee kati ya mababu, mabibi, wazee na wajukuu wao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wazee wanapaswa kupata matibabu muafaka kwa kutambua kwamba, wao ni hazina, amana na utajiri wa ubinadamu. Hawa ni chemchemi ya hekima na kumbukumbu hai kwa jamii na Kanisa katika ujumla wake. Tema hii ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuwalinda, kuwatunza na kuwathamini wazee, ambao kutokana na sababu mbalimbali wanaendelea kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kifamilia, jumuiya pengine na hata katika Kanisa. Uzoefu, ujuzi na mang’amuzi yao ya maisha na imani yanaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii, kwa kutambua mizizi yake sanjari na ujenzi wa jamii inayosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Siku ya babu, bibi, wazee na wajukuu wao ni muhimu kukoleza majadiliano
Siku ya babu, bibi, wazee na wajukuu wao ni muhimu kukoleza majadiliano

Ni muhimu sana ikiwa kama wajukuu wataendelea kushikamana na kufungamana na babu pamoja na bibi zao, ili waweze kujichotea tunu msingi za maisha ya kiutu, kitamaduni na kiroho. Jamii haina budi kuhakikisha kwamba, inatoa fursa kwa vijana wa kizazi kipya kukutana na kujadiliana na “vijana wa zamani.”  Yaani hawa ni wazee, kwani hapa ari na mwamko wa hekima ya wazee inakutana na mwamko wa vijana wa kizazi kipya, hasa katika nyakati hizi za athari kubwa za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa sanjari na mmong’onyoko wa tunu msingi za kijamii, unaoendelea kujionesha kila kukicha katika maisha ya binadamu. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linawaalika watu wa Mungu kuadhimisha siku hii kwa kuwa na mwelekeo wa Kanisa la Kisinodi linalojikita katika: Umoja, Ushiriki na Utume. Linawaalika viongozi wa Makanisa mahalia: kitaifa, kijimbo na kiparokia pamoja na vyama vya kitume, kuhakikisha kwamba, vinaadhimisha Siku ya Wazee Duniani katika muktadha wa shughuli za kichungaji katika maeneo yao.

Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi kieleweke kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wazee na vijana wanahitajiana, ili kukamilishana katika hija ya maisha yao na hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono” Yoe 2: 28-32.

Ni siku ya kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Ni siku ya kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Wazee wanahamasishwa kutumia ujuzi, uzoefu na mang’amuzi yao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu anasema, wazee wengi wana kumbukumbu ya machungu katika maisha, lakini ikumbukwe kwamba, kumbukumbu ni sehemu ya maisha na kama ikutumiwa vyema inaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki na ukarimu na kwamba, msingi wa maisha ya kweli ni kumbukumbu! Sala ya wazee ina nguvu kiasi hata cha kuweza kuulinda ulimwengu. Ni maneno yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, hata katika uzee wake anaendelea kusali na kuliombea Kanisa. Huu ni msukumo mpya katika mchakato wa uinjilishaji. Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Tafakari ya Neno la Mungu ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika huduma.

Siku ya Wazee Duniani
15 February 2022, 15:45