Jumatano ya Majivu: Kufunga, Kusali na Kuombea Amani Ukraine!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tarehe 2 Machi 2022 ni Jumatano ya Majivu. Huu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na machungu pamoja na masikitiko makubwa sana moyoni mwake kutokana na Urussi kuivamia kijeshi Ukraine, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine ambayo kwa sasa inateseka sana baada ya kuvamiwa kijeshi na Urussi, Alhamisi tarehe 24 Februari 2022.
Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2021 aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtafakari Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kunogesha majadiliano na hatimaye, kujenga ushirika wa upendo na maisha. Kristo Yesu ni kiini cha amani ya kweli, lakini bado vita inaendelea kurindima sehemu mbalimbali za dunia; bado kuna kinzani na mipasuko ya kijamii. Lakini pamoja na mambo yote haya Mama Kanisa bado anathubutu kutangaza ujumbe wa matumaini unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Kristo Yesu ni chemchemi ya amani inayotangazwa kwanza kabisa katika sakafu ya nyoyo za watu na hatimaye, kuenea sehemu mbalimbali za dunia. Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wanaendelea kushuhudia ongezeko la vita, dharura na watu wa Mataifa kusigana na kuanza kupambana kwa silaha mambo ambayo yanaonekana kana kwamba, sasa yanaanza kuzoeleka na wala si habari tena.
Kuna maafa makubwa yanayotendeka sehemu mbalimbali za dunia, lakini yanapita katika hali ya ukimya. Kuna hatari kwamba, watu wakashindwa kusikiliza kilio cha mateso na kukata tamaa kinachotolewa na watu wengi duniani. Juhudi za kidiplomasia katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita hazikuweza kufua dafu na kuzaa matunda yaliyokusudiwa na matokeo yake ni Urussi kuivamia kijeshi Ukraine na hivyo kusababisha maafa kwa watu na mali zao. Wapenda haki, amani na maridhiano duniani wanapinga vikali uvamizi huu na kumtaka Rais Vladimir Putin wa Urussi kuondoa majeshi yake nchini Ukraine bila masharti, wito ambao unaonekana kugonga mwamba! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika ujumla wao, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kufunga na kusali, ili kuombea amani na utulivu nchini Ukraine. Hizi ni silaha madhubuti dhidi ya hali tete inayoendelea kwa sasa nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ni Mungu wa amani na wala si Mungu wa vita; ni Baba wa wote na wala si kwa baadhi ya watu. Mwenyezi Mungu anataka watu wajenge umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu na wala si kujiundia maadui.
Jumatano ya Majivu waamini wanapakwa majivu yanayowakumbusha kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi, changamoto kubwa ni kupyaisha maisha ya kiroho kwa njia ya: Sala na sadaka. Ni wakati wa kujichimbia katika tafakari ya Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ni njia muafaka ya kujiandaa kikamilifu ili kukutana na Kristo Mfufuka aliye hai katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa na kwa njia ya huduma makini kwa jirani sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Waamini wajitahidi kufunga ili kuratibu vilema vyao na kwa kuepuka dhambi za mazoea na hatimaye, wamwombe na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia toba na wongofu wa ndani unaowaletea upya wa maisha, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka baada ya siku 40 za maisha ya kiroho jangwani! Kipindi cha Kwaresima yaani Siku 40 ni safari ya maisha ya kiroho inayojikita katika: imani, matumaini na mapendo.