Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Cosenza Jimbo kuu la Cosenza-Bisignano: Ujumbe: toba na wongofu; utume na dhana ya sinodi Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Cosenza Jimbo kuu la Cosenza-Bisignano: Ujumbe: toba na wongofu; utume na dhana ya sinodi 

Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Cosenza: Wongofu wa Ndani

Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa kuu la Cosenza ni fursa ya toba tayari kushiriki kikamilifu maisha na utume wa Kanisa ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Watoe kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika maisha ya kiroho na kiutu na hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo kuu la Cosenza-Bisignano, lililoko Kusini mwa Italia tarehe 30 Januari 2022 limezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Cosenza hapo tarehe 30 Januari 1222, Ibada iliyoongozwa na Kardinali Niccolò de Chiaramonti, kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jubilei itafungwa rasmi tarehe 12 Februari 2023. Kanisa hili lilijengwa na hatimaye kutabarukiwa upya kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea kunako mwaka 1184. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa kuu la Cosenza yamezinduliwa rasmi na Askofu Emil Paul Tscherrig, Balozi wa Vatican nchini Italia. Katika maadhimisho haya waamini wanaweza kujipatia rehema kamili. Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa Katoliki yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi.

Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa kuu la Cosenza, Italia
Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa kuu la Cosenza, Italia

Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa Rehema Kamili. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa kuu la Cosenza anapenda kuungana na watu wa Mungu Jimbo kuu la Cosenza-Bisignano kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na amana na utajiri wa sanaa na historia inayohifadhiwa kwenye Kanisa hili. Hii ni fursa ya toba, wongofu wa ndani, tayari kutoka kimasomaso kushiriki kikamilifu maisha na utume wa Kanisa ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu juu ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Watoe kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi katika maisha ya kiroho na kiutu na hasa kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Waamini watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye jiwe kuu la msingi, mwaliko wa kutafakari uzuri, ukuu na utakatifu wa Kanisa la Mungu, ili kuamsha na kupyaisha ile kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika Sala, Neno, Sakramenti, maisha na utume wa Kanisa. Jubilei kiwe ni kipindi cha kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu, kwa kutembea pamoja kama Kanisa la Kisinodi, ili kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika umoja, ushiriki na utume. Ni wakati wa kupyaisha shughuli za kichungaji kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wakati muafaka wa kudumisha haki jamii, utawala wa sheria, amani na utulivu. Jubilei ni fursa ya kumwendea Mwenyezi Mungu kwa moyo wa uchaji na ibada sanjari na kuwaelekea jirani kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Jubilei Miaka 800

 

01 February 2022, 15:12