Tafuta

Papa Francisko amewaandikia barua wanandoa, vijana na wanandoa watarajiwa ili kuwatia shime katika kutangaza na kushuhudia furaha ya upendo ndani ya familia Papa Francisko amewaandikia barua wanandoa, vijana na wanandoa watarajiwa ili kuwatia shime katika kutangaza na kushuhudia furaha ya upendo ndani ya familia 

Barua ya Papa Francisko Kwa Wanandoa, Watarajiwa na Vijana: Upendo

Barua ya Papa Francisko kwa wanandoa anakazia: Umuhimu wa wito wa upendo, malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia, utambulisho na utume wa waamini walei. Wito wa ndoa unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ndoa, wema, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia na kwamba, Mtakatifu Yosefu awe ni mfano wa kuigwa katika ujasiri nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko alizindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: “Famiglia Amoris Laetitia.” Mwaka utakaohitimishwa kwa kudema wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.  Lengo kuu la Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni Mosi: Kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia wanandoa barua, akikazia umuhimu wa wito wa upendo kwa wanandoa, malezi na makuzi ya watoto ndani ya familia, utambulisho na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa. Wito wa ndoa unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ndoa, wema, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia na kwamba, Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa kuigwa katika ujasiri hasa katika kipindi hiki chenye mabadiliko makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu. Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu mkubwa, upendo, ukweli na uwazi anapenda kuchukua fursa hii kuwaandikia barua wanandoa katika hali na mazingira mbalimbali wanayokabiliana nayo, kwani hata haya ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.

Watoto wanahitaji huruma na upendo wa wazazi wao
Watoto wanahitaji huruma na upendo wa wazazi wao

Jambo la kukumbuka ni kwamba, katika mapito yote haya Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwaongoza na kuwashika mkono, kwani yupo pamoja nao katika familia, ujirani mwema, mahali pa kazi, shule na katika miji wanamoishi. Kama ilivyokuwa wito kwa Mzee Ibrahimu Baba wa imani, wanandoa nao wamejikuta, kila mmoja kwa wakati na mahali pake, akijibu wito wa ndoa takatifu, unaopitia hali mbalimbali za maisha. Hatimaye, hawa wawili si wawili tena bali wamekuwa wamoja katika ushirika na Kristo Yesu anayeendelea kutembea pamoja nao katika maisha yao na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yupo kandoni mwao na kamwe hawako pwekwe! Watoto wanapenda kuwaona wazazi wao wakipendana, kwa sababu hawa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watoto wana kiu na njaa ya upendo, shukrani, utambulisho pamoja na kuaminiwa. Mwaliko kwa wazazi kuhakikisha kwamba, wanarithisha ile furaha ya kwamba wao ni watoto wa Mungu ili wakue katika imani na kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Malezi na makuzi ya watoto ni changamoto pevu, kwani mahitaji ya kifamilia hayana budi kuzingatiwa katika medani mbalimbali za maisha. Wazazi ni walezi wa kwanza kwa watoto wao na kuendelea kusaidiwa na walimu. Watoto wanahitaji kuwa na uhakika wa usalama wao, kumbe, ni wajibu wa wazazi kuwajengea watoto wao imani na uzuri wa maisha ya ndoa na familia.

Mama Kanisa anatambua na kuthamini utambulisho na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, kwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mwanga wa mataifa na chumvi ya ulimwengu ili kuyatakatifuza malimwengu. Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika utume wa familia ndani ya Kanisa, kwa kushirikiana na wakleri ili kulinda na kutunza Kanisa la nyumbani. Ikumbukwe kwamba, familia ndiyo kiini cha msingi kabisa cha msingi wa jamii ambapo watu wanajifunza kuishi katika tofauti zao msingi lakini wakiwa wamoja. Maisha ya ndoa na familia ni mradi mkubwa wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana. Ndiyo maana familia zinapewa wito wa ujenzi madaraja ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kujenga ubinadamu wa kweli. Katika ulimwengu mamboleo kipaji cha ubunifu kinahitajika sana, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika jamii, Kanisa na miongoni mwa watu wa Mungu. Ndoa ni wito mtakatifu, unaohitaji mshikamano na mafungamano na Kristo Yesu. Kamwe, wanandoa wasidhani kwamba Kristo Yesu “anauchapa usingizi” wala haguswi na “kasheshe na vitimbwi vinavyoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya waamini. Uwepo endelevu na fungamani wa Kristo katika maisha ya wanandoa, uwasaidie kuyaangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali kwa mwanga wa imani. Ni fursa ya kutambua udhaifu na mapungufu ya kila mmoja wao na hivyo kuwa tayari kujiaminisha kwa Kristo Yesu.

Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, imekuwa ni fursa ya kuimarisha ushirika wa kifamilia, unaofumbatwa katika uvumilivu na upendo wa dhati kama unavyofafanuliwa na Mtume Paulo katika Nyaraka zake: Rum 8: 15; Gal 4:6. Wanandoa wajifunze kujenga na kudumisha upendo wa dhati wanapokuwa pamoja. Familia iwe ni mahali pa mtu kukubalika, kupokeleka na kufahamika. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wanandoa yale maneno makuu matatu: tafadhali, asante na samahani. Wanandoa wawe tayari kuombana msamaha, kila mara “wanapotibuana nyongo.” Wajitafutie nafasi ya kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kutafuta amani na utulivu wa ndani. Wanandoa wasindikizane kwa sala, toba na wongofu wa ndani. Kipindi cha maambukizi makubwa ya UVIKO-19 kimesababisha pia “kasheshe na patashika nguo kuchanika.” Kumekuwepo na matukio ya mateso, nyanyaso na ukatili mkubwa ndani ya familia, kiasi cha watu kuachana, na kila mmoja kushika “hamsini zake.” Wote hawa Baba Mtakatifu anapenda kuwaonjesha upendo wake wa dhati kabisa.

Vijana wasaidiwe kujiandaa kufunga ndoa takatifu
Vijana wasaidiwe kujiandaa kufunga ndoa takatifu

Ndoa inapovunjika waathirika wakuu ni watoto, kumbe, kuna haja kwa wanandoa kuhakikisha kwamba, wanamaliza kinzani na migogoro yao kwa amani na hivyo kusonga mbele na safari ya maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wajitahidi kuvumiliana na kuchukuliana, ili kuonja huruma na upendo wa Kristo Yesu katika maisha yao. Wawe ni watu wa msamaha ambao ni kielelezo cha ukomavu wa maisha ya sala, mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu awasaidie wanandoa kujenga familia zao katika msingi thabiti. Re. Mt. 7:24. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa wanandoa, anatoa nafasi kwa vijana wa kizazi kipya, hawa ndio wale wanandoa watarajiwa, wanaojiandaa kufunga pingu za maisha. Anatambua fika matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo vijana katika ulimwengu mamboleo. Ukosefu na uhakika wa fursa za ajira, visiwavunje moyo, bali wajitahidi kuwa na ujasiri wenye ubunifu.

Wanandoa waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Mwenyezi Mungu, familia zao, ndugu, jamaa na Kanisa katika ujumla wake. Wote hawa wasaidie mchakato wa maandalizi ya maisha ya ndoa na familia. Vijana wathubutu kujifunza kutoka kwa watu wenye uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya ndoa na familia. Wazee wakumbuke pia kwamba, wanao mchango mkubwa katika kuendeleza kumbukumbu kama sehemu ya ujenzi wa dunia inayosimikwa katika ukarimu na utu wema. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Yosefu awe ni mfano wa ujasiri wenye ugunduzi. Bikira Maria awasaidie wanandoa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Kristo Yesu, awe ni chemchemi ya furaha ya maisha ya ndoa yao, mwaliko wa kuishi wito wa ndoa na familia kwa ari na moyo mkuu! Watu wa ndoa, wawe na nyuso za tabasamu la kukata na shoka! Watoto wanataka kuona ushuhud waa upendo wa wazazi wao, ili kutiwa moyo. Kwa ujumla watu wa Mungu wanataka kuona uwepo na furaha ya watu wa ndoa inayo bubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanandoa wajifunze kudumu katika sala na katika kuumega mkate!

Barua kwa Wanandoa
13 February 2022, 16:11