Askofu Mkuu Mstaafu J. Lebulu: Umoja, Ushiriki na Utume wa Watawa Kwa Makanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa Watakatifu amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 2 Februari, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, changamoto na mwaliko kwa Wakristo wote kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na upendo wa huduma kwa jirani. Hii ni sikukuu ya mwanga na watu kukutana na Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Kimsingi Kristo Yesu anakutana na watu wake, wanaowakilishwa na Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli. Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu kujenga utamaduni wa wazee na vijana kukutana katika upendo, ili kuimarisha nguvu ya kuweza kusonga mbele. Kumbukumbu, historia, mang’amuzi na maisha ya wazee ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya wanaoendeleza ndoto ya matumaini. Ni siku maalum ya kuwakumbuka na kuwaombea watawa wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu, Kanisa na jirani zao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Watawa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma ya afya, elimu, ustawi wa jamii pamoja na shughuli za kichungaji kama vile katekesi na elimu ya dini shuleni. Huu ni mwaliko kwa waamini kusali na kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ili kweli Kanisa liweze kupata watawa watakatifu, wachamungu na wenye bidii, juhudi na maarifa.
Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 alianzisha Siku ya Watawa Ulimwenguni inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari sanjari na Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Na kwa mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 26 ya Watawa Ulimwenguni. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, lengo kuu la Siku ya Watawa Ulimwenguni ni kumshukuru Mungu kwa watawa ambao wameamua kumfuasa Kristo Yesu kwa kuishi mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili. Ni fursa kwa watawa kurudia tena maagano yao, ili kupyaisha maisha na utume wao mintarafu karama za mashirika yao. Watafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Maisha ya kitawa ni kiini cha utume wa Kanisa, kinacholitajirisha Kanisa kwa karama mbalimbali za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Pili ni nafasi ya kuragibisha maisha na utume wa watawa kwa ajili ya mafao ya Kanisa zima pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao pamoja na kukoleza utakatifu wa maisha. Rej. LG 44. Hii ni siku ambayo watawa wanapaswa kumshangilia Mungu kwa ari na moyo mkuu kwa zawadi hii kubwa ambayo haina mbadala katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kurejea kwenye chemchemi ya miito yao, kutafakari kwa kina na mapana na hivyo kujiwekea malengo kwa siku za usoni.
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema lengo ni kuonesha uaminifu na furaha ya watawa wanaoishi katika mifumo mbalimbali ya maisha na utume wao. Mwaka 2021 mwaliko ulikuwa ni kutangaza na kushuhudia tasaufi ya ushirika, ili watawa waweze kuwa ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu, mwangwi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Huu ni mwaliko kwa watawa wote kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana katika ngazi zote za maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia ushirika wa upendo unaokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu chemchemi ya wema na uzuri unaoweza kuleta nguvu mpya, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Wito wa maisha na utume wao wa kitawa, uwawezeshe kujisikia kuwa ni washiriki wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu unaowafungamanisha na kuwaunganisha wote ili kuwa wamoja. Watambue kwamba, kila mmoja wao anashiriki kikamilifu katika kutekeleza mradi huu kwa ajili ya mafao ya wengi kwa njia ya mshangao wa historia ya miito yao.
Ni muda muafaka wa kuishi na kuendelea kupyaisha ushiriki katika mashirika yao kwani kuna hatari kubwa ya kuweza kumezwa na ubinafsi na hivyo kufyekelea mbali ushirika wa kijumuiya. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kuna ushiriki mkamilifu kwa kutambua kwamba, kila mtawa ni sehemu ya mradi huu mkubwa, ili kuweza kuiishi zawadi hii kuna umuhimu wa kujenga umoja unaovuka kinzani za kitawa! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania, anawataka watawa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Wanayo haki na nyajibu zao wanazopaswa kutekeleza kwa kushirikiana na kushikamana na watu wa Mungu katika ujumla wao. Wawe mstari wa mbele katika: utume, maisha na ujenzi wa Makanisa mahalia kwa njia ya karama na mapaji yao, lengo likiwa ni kushiriki kikamilifu katika utume wa Makanisa mahalia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni wakati wa kuondokana na ubinafsi kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Kanisa la nyumbani, ili kuzamisha ndani mwao dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Ni muda muafaka wa kujipambanua katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa mahalia. Askofu mkuu mstaafu Lebulu anawataka watawa kuzamisha mashauri ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao katika ufukara na utii wa Kiinjili na usafi kamili. Wakazie daima maisha ya kijumuiya ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Wajitahidi kushiriki na kunogesha utume wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo hususan katika Nchi za Afrika na kwa namna ya pekee katika Ukanda wa Nchi za AMECEA ambako dhana ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinapewa kipaumbele cha pekee kama sehemu muhimu sana ya shughuli za kichungaji.