Hija za Kitume Mjini Vatican Zinapania Kuimarisha Urika wa Maaskofu na Papa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Ni katika hali na mazingira kama haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linasema, hija yao ya Kitume mjini Vatican imekuwa ni ya manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Wamejadiliana kuhusu maisha ya Sakramenti za Kanisa na changamoto zake nchini Hispania; umuhimu wa uinjilishaji na urithishaji wa imani unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; huduma ya kiroho na kimwili kwa wakimbizi na wahamiaji; malezi na majiundo makini kama sehemu muhimu ya kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.
Maaskofu Katoliki Hispania wanasema, yote haya ni katika utekelezaji wa dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Hispania. Kumbe, urika wa Maaskofu ni sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana, dhana inayofanyiwa kazi wakati huu wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Wimbi kubwa la maambukizi la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limekuwa ni tishio katika maisha ya kiroho kwa waamini wengi kutokana na madhara yake: kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata katika maisha ya kiroho. Kuna wimbi kubwa la ukoloni wa kiitikadi linalotishia Injili ya uhai sanjari na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kuna haja ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanatangaziwa na kurithishwa imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Hili ni jukumu linaloweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi kwa njia ya waamini walei, waliofundwa barabara katika: Imani, Katekesi, Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Kwa maneno mafupi, ni waamini wanaoifahamu vyema Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Maaskofu wanaendelea kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa waamini walei kwa kutambua kwamba, wanao wajibu na dhamana ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Leo hii kuna changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini Hispania. Hawa ni watu wanaohitaji huduma mbalimbali: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, watawa wa Mashirika mbalimbali wamepewa dhamana ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, huku wakiendelea kushirikiana na kushikamana na Maaskofu mahalia pamoja na Mapadre wa Majimbo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania limejielekeza zaidi katika mchakato wa malezi na majiundo makini kama sehemu muhimu ya kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa nchini Hispania. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wanapenda kutumia vyombo vya mawasiliano ya kijamii pamoja na majukwaa ya kisiasa kulishambulia Kanisa na kusahau kwamba, hili ni janga la kijamii linapaswa kushughulikiwa na wote, ili kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Desemba 2021 alikutana na kuzungumza na Kundi la kwanza la Maaskofu Katoliki Hispania katika hija yao ya kitume, “Ad Limina.” Kati ya mambo ambayo wamejadiliana na Baba Mtakatifu Francisko ni kuhusu: Hali na maisha ya utume wa Kanisa nchini Hispania; athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Mwaka Mtakatifu Yakobo Mkuu pamoja na mwenendo wa mahujaji huko Compostela kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maaskofu Katoliki kutoka Hispania baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wameendelea pia kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusikilizana, ili hatimaye, kufanya maamuzi na utekelezaji wa pamoja. Kwa njia hii, Maaskofu wanasema, Kanisa litaweza kusimama kidete ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika umoja, ushiriki na utume.