Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Watu wa Mungu Kisiwa cha La Palma: Athari za Volkano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na kundi la tatu la Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kama sehemu ya hija ya kitume ya Maaskofu mjini Vatican inayoadhimishwa walau kila baada ya miaka mitano yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.”. Maaskofu Katoliki Hispania wametumia nafasi hii kumwelezea Baba Mtakatifu madhara makubwa yaliyosababishwa na mlipuko wa Volkano uliotokea huko Cumbre Vieja, katika Kisiwa cha La Palma nchini Hispania tarehe 19 Septemba 2021. Serikali ilibidi kuwahamisha watu zaidi ya 7, 000 ili kuwapatia hifadhi kwenye maeneo salama zaidi. Majengo zaidi 3, 000 pamoja na miundombinu ya barabara viliharibiwa sana. Hasara yote inakadiriwa kufikia Euro millioni 843. Huu ni mlipuko wa Volkano ambao umewahi kudumu kwa muda wa siku 85 hadi tarehe 25 Desemba 2021. Ni katika hali na mazingira haya, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, amewatumia watu wa Mungu wanaoishi katika Kisiwa cha La Palma, nchini Hispania ujumbe wa matumaini, wakati huu wa mchakato wa ujenzi mpya wa makazi yao. Hawa ni watu licha ya kupoteza makazi, lakini pia wengi wao wamepoteza fursa za ajira, kumbe wanaishi katika hali na mazingira magumu sana.
Hali ni tete, lakini hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kufanya ukarabati na ujenzi ni hatua kubwa katika kujikwamua na hali yao ya sasa. Watambue kwamba, majanga asilia yapo, lakini si hatima ya maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, kusimama kidete na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu bila kuvunjika moyo. Baba Mtakatifu amewakumbuka pia watu wa Mungu kutoka katika Kisiwa cha Tonga ambao pia wameathirika kutona na mlipuko wa Volkano uliotokea hivi karibuni. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka yake na kwamba, anawaombea. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 26 Septemba 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliwakumbuka na kuwaombea watu walioathirika kutokana na mlipuko wa Volkano ya Teneguía iliyoko kwenye kisiwa cha La Palma katika Visiwa vya Canary, nchini Hispania janga lililotokea tarehe 19 Septemba 2021.
Watu zaidi ya 500 walihamishwa kutoka Kisiwani hapo kama sehemu ya hatua za mwanzo za usalama wa maisha yao. Viongozi wa Serikali ya Hispania wametembelea eneo hili ili kujionea maafa yaliyojitokeza. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano wa kidugu kwa watu wote walioathirika na mlipuko huo. Baba Mtakatifu aliwaombea pia wale wote wanaoendelea kutoa msaada kwa waathirika hawa, ili Bikira Maria, Mama Yetu wa Las Nieves, aweze kuwalinda na kuwapatia tunza yake ya Kimama. Kwa mara ya mwisho, Volkano ya Teneguía iliyoko kwenye Kisiwa cha La Palma katika Visiwa vya Canary ililipuka kunako mwaka 1971. Na takwimu zinaonesha kwamba, kabla ya hapo, mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 1430, kadiri ya Takwimu zilizotolewa na Taasisi ya “National Geographical Institute, ING, nchini Hispania.