Siku ya 56 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni Kwa Mwaka 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 56 ya Upashanaji Habari Ulimwengu kwa mwaka 2022 sanjari na maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni hapo tarehe 29 Mei 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Kusikiliza kwa Sikio la Moyo.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia umuhimu wa kusikiliza kama tunu na amana katika tasnia ya mawasiliano ya jamii na kama njia ya kunogesha majadiliano katika ukweli na uwazi; majadiliano kati ya Mungu na waja wake kama kielelezo cha neema, ingawa mwanadamu ana tabia ya kutaka kuziba masikio yake. Baba Mtakatifu anasema, kusikiliza ni kielelezo cha mawasiliano bora zaidi yanayosimikwa katika: ukweli na uwazi; imani na uaminifu. Kumbe, kusikiliza ni kati ya sifa kuu za majadiliano na mawasiliano bora yanayofumbatwa katika uvumilivu ili kugundua ukweli wa mambo katika ukuaji wa uchumi, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, ili kuondokana na maamuzi mbele na ugumu wa mioyo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa halina budi kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza hasa pale Mwenyezi Mungu anapozungumza na waja wake kwa njia ya Neno lake, katika sala na waamimini wanaposikilizana wao kwa wao, watambue kwamba, hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na karimu, mwanzo wa mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.
Lengo kuu ni Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina”. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Wafuasi hawa baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, walirejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yanapania kuchochea: Umoja, Ushiriki na Utume mambo yanayokolezwa na usikilizaji mzuri na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Ujumbe wa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni hutolewa wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, tarehe 24 Januari 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii mkoa wa Lazio nchini Italia, katika Kanisa la “Santa Maria in Montesanto” hili kimsingi ni Kanisa la wasanii. Maadhimisho haya ni kumbukumbu ya miaka 400 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Sale. Kardinali Angelo De Donatis amewashukuru na kuwapongeza wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa kuwajibika, kwa ushupavu, ukarimu na ushujaa wa kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii na hasa wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Kardinali Angelo De Donatis, amewataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, kuendelea kumwilisha ndani mwao, changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021. Baba Mtakatifu anawaalika Waandishi wa Habari “kuchanja mbuga” ili kupata habari nzuri zaidi. Kuna upashanaji habari ambao umekuwa ukitumia sauti. Lakini uandishi wa habari za uchunguzi wa kina kwa ajili ya magazeti, luninga, radio na wavuti zinaanza kupungua makali na viwango vyake, kiasi cha kushindwa kutoa ukweli na uhalisia wa maisha ya watu; ni habari ambazo hazina uzito kwa sababu hazipati chimbuko lake kutoka katika maisha ya watu, matatizo na changamoto zao.
Matokeo yake ni habari nyingi kutengenezwa kwenye “Vyumba vya habari” kwenye Komputer, mitandao ya kijamii, bila “kuchakarika” kutaka kukutana na watu mubashara katika shughuli zao na kuzifanyia uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa mambo kutoka kwa wahusika. Bila ya kujenga utamaduni wa watu kukutana, tasnia hii itabaki kama watazamaji kwa maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano na hivyo kushindwa kuzama katika uhalisia wa maisha ya watu. Vyombo vinaweza kutumika na kuwa na thamani, ikiwa kama vitawasukuma watu kutoka nje na kwenda kujionea ukweli wa mambo ulivyo. Wadau wa tasnia ya mawasiliano waendelee kushirikiana na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Tasnia ya mawasiliano ya jamii, itekeleze dhamana na wajibu huu kwa upendo na sadaka kuu kama alivyokuwa anashauri Mtakatifu Francisko wa Sale, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.