Tafuta

Wajumbe wa Shirikisho la Wajenzi Kitaifa nchini Italia,  ANCE tarehe 20 Januari 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wajumbe wa Shirikisho la Wajenzi Kitaifa nchini Italia, ANCE tarehe 20 Januari 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  

Wajenzi Zingatieni: Ushindani na Uwazi; Kanuni Maadili na Usalama

Baba Mtakatifu Francisko amewaosia wajumbe Shirikisho la Wajenzi Kitaifa nchini Italia, kujikita katika tunu msingi za Kikristo wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu: Waongozwe na kanuni zifuatazo: ushindani na uwazi; uwajibikaji na maisha fungamani; kanuni maadili na usalama kazini kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Wajenzi Kitaifa nchini Italia “L'Associazione nazionale costruttori edili, ANCE” lilianzishwa kunako tarehe 15 Mei 1946, mara tu baada ya Vita ya Pili ya Dunia, na hivyo kuyaunganisha Makampuni 20, 000 na Mashirika 89 ya Ujenzi nchini Italia. Shirikisho hili kwa sasa linaadimisha kumbukizi la Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake na kuendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa majengo mbalimbali nchini Italia. Ni katika muktadha huu, wajumbe wa Shirikisho la Wajenzi Kitaifa nchini Italia, tarehe 20 Januari 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaosia wajumbe hawa kujikita katika tunu msingi za Kikristo wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu: Waongozwe na kanuni zifuatazo: ushindani na uwazi; uwajibikaji na fungamani; kanuni maadili na usalama.  Kristo Yesu katika mafundisho yake alikazia umuhimu wa wafuasi wake halisi kusikiliza na kutenda maneno yake kwani kwa njia hii “Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.” Lk 6: 46-49.

Katika mfano huu, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa wajenzi kujenga msingi imara na thabiti utakaoweza kushindana na changamoto mamboleo kwa kuhakikisha kwamba, shughuli zao zote zinasimikwa katika msingi imara kwani hata leo hii kuna majanga makubwa yanayoendelea kutokea kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumbe, kuna haja kwa wajenzi kusimama imara katika tunu msingi za Kiinjili katika mchakato wa kufikiri na kutenda, ili hatimaye, waweze kusimama imara wakati wa maisha ya kawaida, lakini zaidi wakati shida na magumu ya maisha, kwa kuongozwa na imani inayomwilishwa katika matendo. Tunu zilizobainishwa na Shirikisho la Wajenzi Kitaifa, zipewe kipaumbele cha pekee katika utendaji wao wa kila siku. Kuhusu ushindani na uwazi katika muktadha wa soko huria: kuna hatari ya watu kuanza kujikita katika mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko, kiasi hata cha kuweza kuwaengua wengine kwa njia zisizo halali na madhara yake yataonekana katika uchumi na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushindani uyachochee makampuni kufanya vyema na kwa haki na wala si katika tamaa ya kutaka kuwaengua wengine kutoka katika soko au kuwatawala na kuwakandamiza.

Kumbe, kuna haja ya kudumisha ushindani unaozingatia ukweli na uwazi katika mchakato wa maamuzi na sera za kiuchumi. Kusiwepo na ushindani tenge katika sekta ya uchumi kwani hali hii inaweza kusababisha ukosefu wa fursa za ajira na matokeo yake ni kuibuka kwa kazi za suluba na mshahara “kiduchu.” Na huu ndio mwanzo wa rushwa na ufisadi, unaorutubishwa na ukosefu wa haki na uvunjaji wa sheria. Baba Mtakatifu Francisko anasema, dhana ya uwajibikaji na fungamani ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee kwa wakati huu, ili kudumisha ikolojia fungamani. Katika ujenzi kuna haja ya kutumia vifaa vinavyowahakikishia watu usalama wa maisha na mali zao. Ni vyema kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani kuna maeneo ambayo yameharibiwa sana kutokana na shughuli za ujenzi. Kila kampuni inaweza kuchangia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, ili kweli kazi iweze kuwa fungamani. Kwa kuzingatia uhusiano uliopo kati ya makazi ya watu na tabia ya mwanadamu, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wale wanaosanifu majengo, ujirani, maendeleo ya umma na mipango miji wanapaswa kujifunza kutoka kwa taaluma mbalimbali zinazowasaidia kuelewa fikra za watu, lugha za picha na namna yao ya utendaji. Haitoshi kutafuta uzuri wa usanifu peke yake. Jambo jingine msingi ni huduma ya uzuri wa aina yake, yaani mchakato wa maisha bora ya watu, jinsi wanavyomudu mazingira yao, wanavyohusiana na kusaidiana. Hapa kuna haja ya kukazia mipango miji kwa kuzingatia maoni ya watu watakao kaaa katika maeneo hayo. Rej. Laudato si 150.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, kazi ya wajenzi hawa itazisaidia jumuiya mbalimbali kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii yanayosimikwa katika mshikamano, ushirikiano pamoja na kusaidiana kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu amekazia pia kanuni maadili na usalama kazini na kusikitika kusema kwamba, kumekuwepo na vifo vya wafanyakazi wengi mahali pa kazi. Hapa izingitiwe kwamba, ni watu wanaopoteza maisha na wala si tu idadi inayokumbukwa. Wajenzi pia wameguswa na kutikiswa katika shughuli zao. Ulinzi na usalama kazini vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wala si kwa kuangalia gharama zake, kwani huo utakuwa ni mwanzo wa mawazo potofu. Amana na utajiri wa kweli ni rasilimali watu, wanaojenga na kudumisha jumuiya ya wafanyakazi, wanaoongeza pato la makampuni pamoja na ukuaji wa uchumi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu maboresho ya ulinzi na usalama maeneo ya kazi maana yake ni kulinda na kutunza rasilimali watu ambao wana thamani kubwa sana machoni pa mwenyezi Mungu, kama ilivyo kwa wafanya biashara wa kweli. Usalama kazini ni mchakato unaopania kulinda rasilimali watu na hivyo kuwawezesha kupara riziki yao ya kila siku. Kumbe, kuna haja ya kuboresha ulinzi na usalama kazini, ili kunogesha zaidi ubora na uzuri wa kazi zinazotekelezwa. Mtakatifu Yosefu, Mlinzi na Mwombezi wa wafanyakazi awasimamie na kuwaongoza katika shughuli na utendaji wao wa kazi.  

Wajenzi

 

20 January 2022, 14:56