Papa:Familia na walimu wakuze ufahamu kwa vizazi ukurasa mweusi wa historia!
Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican.
Yalikuwa ni maangamizi makubwa dhidi ya Wayahudi wa Ulaya, Holocaust, na kwa lugha ya Kiebrania Shoah ambayo ni mauaji ya kimbari. Inasadikika kuwa watu milioni 5-6 kutoka Barani Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya miaka 1940 na 1945 walikufa. Mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na serikali ya Ujerumani chini ya kiongozi wa wakati huo Adolf Hitler kwa msaada wa serikali za nchi zilizofungamana na Ujerumani au zilizokuwa chini ya jeshi la Ujerumani. Kwa maana hiyo kumbu kumbu ya Shoah, inakumbusha mnamo tarehe 27 Januari 1945, tarehe ambayo kila mwaka imewekwa na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kuikumbuka na ili ili mauaji ya kimbari yasijirudie tena na hasa hata kuondoa fikira nyingi potofu kwa wale ambao wanakataa kuwa jambo hili halikutokea.
Katike mkesha wa siku hiyo, Jumatano tarehe 26 Januari 2022, Baba Mtakatifu mara baada ya tafakari na salamu kwa waamini na mahujaji waliokuwa katika Ukumbi wa Paulo VI, Vatican, alikumbusha juu ya siku ya kumbu kumbu ya miaka 77 kimataifa kwa ajili ya waathirika wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi. Papa alisema ni lazima kukumbusha maangamizi ya milioni za wayahudi na watu tofauti wa mataifa na imani za kidini. Hali hii isirudiwe kamwe ya ukatili usiolelezeka. Alitoa wito kwa wote hasa walimu na familia ili waweze kukuza katika vizazi vipya utambuzi wa tishio baya sana katika ukurasa mweusi wa historia. Hiyo haipaswi kusahaulika ili kuweza kujenga wakati ujao mahali ambapo hadhi ya binadamu haikanyagwi tena, alisisitiza Papa. Hii ni kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yalotekelezwa dhidi ya Wayahudi, yaani ‘Holocaust’, ambayo hufanyika kila mwaka kwa kukumbuka siku ya kufunguliwa kwa kambi ya mauaji ya kimbari ya Auschwitz- Birkenau na kumbukumbu kwa wahanga wa mauaji hayo.