Tafuta

Papa Francisko amewataka wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kusimama kidete kulinda: Imani, maadili na utu wema. Papa Francisko amewataka wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kusimama kidete kulinda: Imani, maadili na utu wema.  

Papa Francisko: Tunzeni Imani, Dumisheni Utu Na Maadili Mema

Utu wa binadamu, mang’amuzi, imani na maadili ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuyafafanua kwa kina na mapana Ijumaa tarehe 21 Januari 2022, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa mwaka. Utu na heshima ya binadamu vinapaswa kudumishwa na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ndilo lililokabidhiwa dhamana na utume wa kulinda na kudumisha mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki kuhusu imani na kanuni maadili. Utu wa binadamu, mang’amuzi, imani na maadili ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuyafafanua kwa kina na mapana Ijumaa tarehe 21 Januari 2022, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa mwaka. Baba Mtakatifu anasema, katika muda huu ambao binadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu nafasi ya kuishi kuna haja ya kukiri na kutambua utu na heshima ya binadamu, ili kujenga udugu wa kibinadamu ulimwengu. Hii ni kiu ya Mwenyezi Mungu Muumbaji inayotekelezwa katika hija ya maisha ya mwanadamu ambaye utu wake unapaswa kutambuliwa. Katika ulimwengu mamboleo ambako kuna kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na hata kiafya, kumezuka tabia ya baadhi ya watu kuanza kuangaliana “kwa jicho pembe”, kwa kuwaona wengine kuwa kama ni “watu wa kuja”, wageni na adui bila kuwapatia utu na heshima yao.

Baba Mtakatifu amewataka wajumbe wa Baraza kuwa makini na tayari wakati ufaao na wakati usiofaa, wakaripie, wakemee na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Rej. 2Tim 4:2. Wawe makini na waaminifu kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa kuhusu utu wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni katika muktadha huu, huduma inapaswa kutolewa kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake kama mambo msingi yanayoweza kunogesha udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kati ya watu wa Mataifa. Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Mama Kanisa amesimama kidete kutangaza na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kimsingi binadamu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha kazi ya Uumbaji, kiasi hata cha kuteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa mwenza katika mipango yake ya milele na kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, Kristo Yesu, ameteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Baraza ambao katika mkutano wao mkuu kwa mwaka 2022 wamejadili kuhusu utu wa binadamu sanjari na changamoto mamboleo zinazomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu amegusia pia dhana ya “Mang’amuzi.” Leo hii, waamini wanatakiwa kujikita katika mchakato wa mang’amuzi kutokana na ukweli kwamba, waamini wanakabiliana na mawimbi ya maswali mazito na changamani; hali inayohitaji tasaufi ambayo wakati mwingine si rahisi sana kuweza kuipata kwa kufuata Maandiko Matakatifu. Leo hii kuna matukio ambayo si ya kawaida, kiasi cha kuwafanya watu wa Mungu kudai maelezo na ufafanuzi wa kina na wenye uhakika. Dhana ya mang’amuzi ni silaha makini inayoweza kupambana na changamoto zote zinatokana na kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Mama Kanisa anataka kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ili kutoa haki kwa watu walionyanyaswa na kudhulumiwa kijinsia, kwa kufuata na kutekeleza kanuni, sheria na taratibu ambazo zimebainishwa. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu kwamba, amesasisha kanuni za uhalifu zilizotengwa kwa ajili ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, akipania kuleta ufanisi mzuri zaidi katika hatua za Kimahakama. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, jambo hili peke yake haliwezi kukomesha kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa, lakini hii ni hatua muhimu ya kurejesha tena haki, kurekebisha kashfa sanjari na kumrekebisha mkosaji.

Dhana hii inapaswa pia kumwilishwa katika kutengua maagano ya ndoa kwa kutoa upendeleo wa imani “in favorem fidei.” Kwa mamlaka aliyopewa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mama Kanisa ya kuvunja maagano ya ndoa isiyo ya Kisakramenti, sio tu ni kwa ajili ya kusitisha ndoa kisheria, ambayo tayari inaonesha kushindwa, lakini kiukweli hii ni njia kwa tendo hili kuu la shughuli za kichungaji linalotoa upendeleo wa Imani Katoliki “In favorem fidei”, ili muungano mpya na katika familia, ambayo ndoa hii mpya itakuwa ni kiini chake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika changamoto hii, kuna haja ya kumwilisha dhana ya mang’amuzi kama yanavyobainishwa kwenye mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Lengo ni kuwasikiliza watu wa Mungu, kuchambua yaliyozungumzwa na hatimaye, kutoa matokeo yake. Kuna haja ya kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu mawazo binafsi, mielekeo na tafakari makini, huku wakisaidiwa na Roho Mtakatifu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limepewa dhamana na wajibu wa kulinda na kuendeleza Imani Katoliki, ili imani ya Kanisa igeuzwe na kuwa kama wakala wa udugu. Imani inapaswa kuwa ni kiini na mwongozo wa maisha wa kila Mbatizwa.

Hii inapaswa kuwa ni imani thabiti anayoitaka Kristo Yesu mwenyewe anapowaambia Mitume wake kama wangekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, wangeweza kuuambia mkutu huu, “Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii. Rej. Lk 17:6. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuwa na imani thabiti, itakayowasaidia kukua sanjari na kuwapatia jukwaa la kuulizana maswali, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kwamba, imani yao inapaswa kuwashirikisha wote. Waogope imani na kutenda mambo kwa mazoea. Huu ni mwaliko wa kuendelea kushirikiana na Roho Mtakatifu pamoja na wale wote wanaofanya nao kazi, ili kuendelea kuwasha moto wa imani kwa watu wote.

Papa: Imani na Maadili

 

21 January 2022, 15:27