Papa Francisko: Kusanyeni Kodi kwa Kuzingatia: Sheria, Ukweli, Uwazi na Haki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu 31 Januari 2022 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Wakala wa Mapato Italia, “Agenzia delle Entrate”. Baba Mtakatifu ametumia mwanya huu kuweza kutoa katekesi mintarafu mwanga wa Injili kuhusu: Kodi, Sheria, Kutopendelea, Ukweli na Uwazi, mambo ambayo yanaongoza kila siku maisha ya watu wa Mungu. Watawala wote wa dunia, walianzisha kodi na kama ilivyokuwa hata nyakati za Kristo Yesu. Warumi katika utawala wa Kaisari waliwatoza watu kodi, kazi iliyotekelezwa na watoza ushuru na kati yao alikuwepo Zakayo, mkubwa mmoja kati ya watoza ushuru naye alikuwa tajiri. Rej. Lk 19:1-9. Zakayo alipata bahati ya kutembelewa na Kristo Yesu, akatubu na kumwongokea Mungu na wokovu ukaingia katika nyumba yake. Itakumbukwa kwamba, hata Mathayo alikuwa Mtoza ushuru na Kristo Yesu alimwita Mathayo akiwa forodhani, akaondoka akamfuata. Mathayo mtoza ushuru, akawa: Mfuasi, Mtume na Mwinjili. Itakumbukwa kwamba, Mathayo ndiye yule Mwinjili aliyetazamwa kwa jicho la huruma na upendo.
“Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo” ni maneno yaliyoko kwenye Nembo la Kiaskofu ya Baba Mtakatifu Francisko. Tangu wakati huo, maisha ya Mathayo yakabadilika na kupata mwanga na mwelekeo mpya uliong’arishwa kwa uwepo, huruma na upendo wa Kristo Yesu. Akageuka na kuwa ni shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na ukarimu kwa watu wa Mungu kama Kristo Yesu alivyokuwa anafundisha na kushuhudia. Katika Maandiko Matakatifu, rasilimali fedha inajitokeza sana tangu wakati wa Agano la Kale na inajulikana kama “Fungu la kumi”. Hii ni fedha, mazao ya nchi au mifugo iliyotolewa kwa Mfalme kama zaka, yaani alama ya shukrani, ukombozi na utakatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Rej. Law 27: 30-33. Watu wa Mungu walikumbushwa kwamba, kamwe hawawezi kujitosheleza wenyewe kwa sababu wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, wanapaswa pia kusumbuka na kuwajibikiana, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko baada ya katekesi kuhusu: kodi na rasilimali fedha kadiri ya Maandiko Matakatifu akajielekeza zaidi katika masuala ya: Kodi, Sheria, Kutopendelea, Ukweli na Uwazi; mambo msingi yanayopasa kuwaongoza wanapotekeleza dhamana na utume wao wa kukusanya kodi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu amewataka watoza kodi na ushuru kujenga urafiki, mahusiano na mafungamano mazuri na wananchi wanaotozwa kodi, ili kuwajengea utamaduni wa kupenda kulipa kodi na ushuru kwa moyo mweupe na kamwe wasichukuliwe kuwa ni wavunja sheria. Wananchi wawe tayari kutekeleza wajibu wao bila shuruti kama kielelezo cha ujenzi wa jamii inayosimikwa katika usawa. Faida kubwa kupita kiasi inaweza kujenga matabaka katika jamii. Sheria, taratibu na kanuni katika masuala ya kodi ni njia muafaka ya ujenzi wa usawa wa kijamii na hivyo kuepuka kashfa ya rushwa na ufisadi. Ili kuweza kufikia katika hatua kama hii, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika majiundo makini sanjari na kuwa na mwelekeo mpya wa mawazo. Kodi na ushuru ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwanyonya wananchi kama inavyoonekana na wengi nyakati hizi. Kimsingi kodi ni kielelezo cha utawala wa sheria na haki.
Rasimali na utajiri wa nchi hauna budi kutumiwa kikamilifu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wasinyonywe na wajanja wachache. Ikiwa kama kodi ni ya haki na halali ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja kwa Mamlaka za kodi, ushuru na mapato kujitahidi kuwajengea watu utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari kama inavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kanuni ya kutopendelea upande wowote, inawasaidia wananchi kutumia rasimali na utajiri wao binafsi kwa ajili ya kuchangia katika mustakabali wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wamejenga tabia ya kukwepa kodi na ushuru; tabia ya kuomba na kutoa rushwa; upendeleo katika kulipa kodi na mambo yote yanayokwenda kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za kodi. Watoza kodi na ushuru, wanapaswa kuonesha uaminifu, kwa kuhakikisha kwamba, wananchi wanalipa kodi halali na kwa wakati kwa ajili ya mafao ya wengi. Kutokupendelea mtu yoyote ni kielelezo cha ujenzi wa haki jamii na usawa, ili wananchi wengi waweze kuwa ni wajenzi wa ustawi na maendeleo ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka watoza kodi na ushuru kuwapatia watu wote haki zao: Mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru, astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. Rej. Rum 13:17. Baba Mtakatifu anakaza kusema “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.” Rej. Rum 12: 17. Baba Mtakatifu anasema, ukweli na uwazi, vilimsaidia Zakayo Mtoza ushuru kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kutambua udhaifu na makosa yake yaliyopelekea kuwanyonya maskini kutokana na tamaa ya mali na utajiri wa haraka haraka. Baada ya kutubu, kuongoka na kuguswa kutoka katika undani wa maisha yake, Zakayo Mtoza ushuru akawa mtu mpya na kuamua kuwapa maskini nusu ya mali yake, kurudisha mara nne mali ya watu aliyowanyang’anya kwa hila. Kodi na ushuru unaokusanywa usioongozwa na kanuni ya ukweli na uwazi, itazua minong’ono na mtazamo hasi kwa fedha inayokusanywa na Serikali. Watoza kodi wanao wajibu wa kisheria na kimaadili kutojitajirisha na kujinufaisha kwa kodi ya wavuja jasho na maskini wa nchi!
Padre “Don” Primo Mazzolari kunako mwaka 1948 aliwaandikia Wabunge Wakatoliki waliokuwa wamechaguliwa wakati huo kuwa waangalifu kwanza kwa mali zao wenyewe na wajitahidi kutenda wema ili kupunguza umaskini kwa jirani zao, kwa sababu huu ni wajibu wao msingi na ushuhuda wa tunu msingi za Kikristo. Mambo ya kuzingatia ni: Uaminifu, ukweli na uwazi; ushuhuda wa upendo na ukarimu; vitawasaidia wananchi kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kutoa ushuru kwa moyo mweupe. Kodi isaidie kuchangia ustawi na maendeleo fungamani ya watu, kwa kutengeneza fursa za kazi, kuboresha huduma za afya na elimu na ujenzi wa miundo mbinu ya kiuchumi na kijamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka Wakala wa Mapato Italia, “Agenzia delle Entrate” chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Mathayo Mwinjili ili aweze kuwasaidia kutembea katika njia ya: Sheria, Kutopendelea, Ukweli na Uwazi; mambo msingi yanayopasa kuwaongoza wanapotekeleza dhamana na utume wao wa kukusanya kodi na ushuru kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.