Tafuta

Kumbukizi la Miaka 90 la Jarida la "Famiglia Cristiana" ni hazina na amana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kumbukizi la Miaka 90 la Jarida la "Famiglia Cristiana" ni hazina na amana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. 

Jarida la "Famiglia Cristiana" Kumbukizi la Miaka 90 ya Utume!

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia waandishi wa habari wa Jarida hili pamoja na wasomaji wake, akiwatakia heri na mafanikio katika utume huu wa uinjilishaji unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na Tunu msingi za maisha ya kifamilia. Wanahabari wawe na ujasiri wa kuomba ruhusa na kuangalia mambo kwa jicho la kuvutia na si macho ya kengeza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jarida la “Famiglia Cristiana” lililoanzishwa na Mwenyeheri Giacomo Alberione kunako tarehe 25 Desemba 1931 – 25 Desemba 2021 linaadhimisha Kumbukizi la Miaka 90 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni Jarida ambalo limeendelea kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni Jarida ambalo limejipambanua kwa kutofungamana na upande wowote wa kisiasa, daima limejielekeza zaidi kwa ajili ya tunu msingi za kifamilia na masilahi ya watu wa Mungu katika ujumla wake mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Kumbukizi la Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Jarida la “Famiglia Cristiana” anapenda kuwatia shime kutumia ukweli kwa wema kwa kupitia “Uandishi wa Habari Makini” usiotoa nafasi kwa “wambea, kwani hawa hawana Bunge na wala umbea si mtaji, kama ungekuwa mtaji wangetajirika wengi.”

Jarida la Famiglia Cristiana ni limesheheni utajiri wa Mafundisho Jamii ya Kanisa
Jarida la Famiglia Cristiana ni limesheheni utajiri wa Mafundisho Jamii ya Kanisa

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, huu ndio ukweli wa mambo kwamba, kuna umbea unaozagaa kwenye mitandao ya kijamii. Lakini Jarida la “Famiglia Cristiana” liendelee kujikita katika ukweli! “Famiglia Cristiana” huchapishwa kila juma nchini Italia ili kunogesha pia mchakato wa udugu na mshikamano wa kibinadamu. Ni jarida ambalo limejijengea sifa njema ya kujadiliana na wasomaji wake katika makundi mbalimbali. Ni Jarida linalozungumzia tunu msingi za maisha ya familia, elimu, malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya. Linagusia mahusiano na mafungamano ya watoto na wazazi wao, bila kusahau masuala mtambuka ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayowagusa kwa ukaribu sana watu wa Mungu nchini Italia. Jarida la “Famiglia Cristiana” katika kipindi cha mwaka 2020-2021 limepitia kipindi kigumu cha myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa; maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, lakini wakati wote huu, limeendelea kuwa ni chemchemi ya imani na matumaini. Ni Jarida ambalo linaendelea kutanua kwenye mitandao ya kijamii.

Kumbukizi la Miaka 50 tangu Mwenyeheri Giacomo Alberione afariki dunia
Kumbukizi la Miaka 50 tangu Mwenyeheri Giacomo Alberione afariki dunia

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kumbukizi la Miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Jarida la “Famiglia Cristiana”, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia waandishi wa habari wa Jarida hili pamoja na wasomaji wake, akiwatakia heri na mafanikio katika utume huu wa uinjilishaji unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na Tunu msingi za maisha ya kifamilia. Baba Mtakatifu anawaalika waandishi wa habari wawe na ujasiri wa kuomba ruhusa, pili kuangalia mambo kwa jicho la kuvutia kama mtu anavyoangaliwa na rafiki kama alivyopenda kusema Mwenyeheri Giacomo Alberione, Mwanzilishi wa Shirika la Wapaulini aliyezaliwa tarehe 4 Aprili 1884 na kufariki duniani tarehe 26 Novemba 1971. Shirika la Wapaulini linaadhimisha pia kumbukizi la Miaka 50 tangu alipofariki dunia Mwenyeheri Giacomo Alberione.

Mwenyeheri Giacomo Albertione, katika maisha na utume wake, alitambua kwa namna ya pekee mchango wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Alitaka kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu aliye: Njia, Ukweli na Uzima anafahamika sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Mtumishi wa Mungu Giacomo Alberione kuwa ni Mwenyeheri hapo tarehe 27 Aprili 2003. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Jarida la “Famiglia Cristiana”, viongozi, waandishi wa habari sanjari na wasomaji wake wote kwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Jarida la “Famiglia Cristiana.” Hili ni Jarida ambalo limewasindikiza na kuviongoza vizazi vingi kwa kujipambanua kama rafiki na mwenza wa safari ya maisha. Hili ni Jarida kwa ajili ya watu pamoja na watu, tayari kutoa kipaumbele cha pekee kwa watu wasiokuwa na sauti na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa Famiglia Cristiana
27 January 2022, 15:07