Tafuta

Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jarida la "Terra Sana" ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Tano inajikita katika: Nchi Takatifu, Historia, Jiografia na Maisha ya Watu. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jarida la "Terra Sana" ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Tano inajikita katika: Nchi Takatifu, Historia, Jiografia na Maisha ya Watu. 

Injili ya Tano Ni Nchi Takatifu, Historia na Mazingira ya Yesu

Injili ya tano ni Ufunuo wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, yaani Kristo Yesu, katika mazingira ya kihistoria na kijiografia, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hizi ni juhudi za kuwatambulisha watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu, Maisha ya Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali bila kuwasahau Wayahudi na Waislam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jarida la “Terra Santa” linaloratibiwa na Mfuko wa Nchi Takatifu “Fondazione Terra Santa”, yaani kunako mwaka 1921, Jumatatu, tarehe 17 Januari 2022 viongozi na wafanyakazi wa Jarida hili wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa jitihada zao za kuhakikisha kwamba, habari za Nchi Takatifu zinapata nafasi katika vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Huu ni mchakato wa kuhakikisha kwamba, Nchi Takatifu, Mahali alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, Chimbuko la Ukristo, mahali penye Madhabahu yanayoonesha historia ya Ukombozi wa mwanadamu mahali yalipo zinawafikia watu wengi zaidi. Kwa maneno mengine, hizi ni jitihada za kutangaza na kushuhudia Injili ya tano, yaani: Ufunuo wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, yaani Kristo Yesu, katika mazingira ya kihistoria na kijiografia, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hizi ni juhudi za kuwatambulisha watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu, Maisha ya Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali bila kuwasahau Wayahudi na Waislam. Zote hizi ni jitihada za ujenzi wa majadiliano ya kiekumene na kidini huko Mashariki ya kati kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa jamii inayofumbatwa katika udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika ulimwengu wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, kuna haja ya kujenga na kudumisha Jumuiya, lakini zaidi udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuimarisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Juhudi hizi ziwasaidie waamini wa dini mbalimbali kutambuana na kuheshimiana kama watoto wa Mzee Ibrahimu, Baba wa imani ambaye ni chimbuko la Wayahudi, Waislam na Wakristo. Udugu wa kibinadamu uwe ni nyenzo ya huduma makini kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, ili hata wao waweze kupata nafasi ya kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Tano, Jarida hili limeweza kukutana na watu jinsi walivyo katika hali na mazingira yao. Huduma ya upashanaji na mawasiliano, imewawezesha hata kutembelea katika maeneo tete kama Siria, Lebanon, Palestina na Ukanda wa Gaza. Wamekuwa ni mashuhuda wa Habari Njema inayotangaza amani, kwa kuonesha ubaya wa vita na kukazia umuhimu wa upatanisho wa kweli ili kuwarejeshea tena watoto ambao wamepokwa utu, heshima na haki zao msingi; mahangaiko na mateso ya wakimbizi na wahamiaji bila kusahau matumaini na ndoto yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi na kwa njia hii, waandishi hao, wamethubutu hata kuhatarisha usalama na maisha yao, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Tano!

Baba Mtakatifu anasema, Jarida hili limekita mang’amuzi yake katika uzoefu wa watu wanaokutana na Neno la Mungu, Ujumbe wa Wokovu wa walimwengu na kwa njia hii, wameweza kukutana na Kristo Yesu katika mazingira mbalimbali ya watu wake. Kristo Yesu alikuwa anahubiri, aliwaangalia watu kwa jicho la upendo na huruma; alikaa kimya, kiasi cha watu kusutwa kutoka katika undani wa maisha yao. Kwa hakika, Kristo Yesu ni ufuo wa Uso wa Mungu: unaongalia, sikiliza, kugusa na kuzungumza. Neno la Mungu lina nguvu ya kuona na kushirikisha mang’amuzi ya maisha, ili hatimaye, kujenga majadiliano ya kina. Jarida la “Terra Santa” linalo wajibu wa kuhakikisha kwamba, Injili ya Tano kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI inafahamika kwa wengi. Injili ya Tano kwa ufupi ni Nchi Takatifu inayoonesha historia na jiografia ya kazi ya wokovu na hivyo kuwasaidia watu wa Mungu kugusa tena ukweli wa historia ambayo imetekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa kuanzia katika ardhi ya Ibrahimu Baba wa imani, maeneo alimozaliwa, maisha na utume wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Ni kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu ameweza kuingia ulimwenguni na hivyo kumshirikisha mwanadamu katika kazi ya ukombozi. Fumbo la Pasaka ni mwanga angavu hata katika historia ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Leo hii bado kuna madonda makubwa ya vita na kinzani, lakini pia kuna neema na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anafungua matumaini ya udugu wa kibinadamu na amani. Na haya ndiyo masimulizi ya Injili ya Tano, ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kuandika katika historia na maisha ya mwanadamu. Kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, wanaweza kusaidia kuboresha imani ya watu hata wale ambao bado hawajawahi kufanya hija ya kiroho katika Nchi Takatifu. Mwishoni mwa hotuba yake Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, huu ni utume unaotekelezwa kwa kuzingatia weledi, umahiri na umakini mkubwa katika huduma ya Injili ya Tano. Hii ni hazina na amana kwa waamini wote duniani na msaada mkubwa kwa Wakristo wanaishi katika Nchi Takatifu. Baba Mtakatifu amependa kutumia fursa hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu. Anawakumbuka katika sala na sadaka yake na watakaporejea makwao, wamsaidie kumfikishia salam na baraka zake za kitume. Wote anawakumbuka katika sala zake!

Terra Santa
17 January 2022, 15:09