Tafuta

Papa Francisko:Bwana anataka tuaminiane na kutembea pamoja

Baba Mtakatifu katika masifu ya pili ya Jioni katika siku ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo,pamoja na kufunga Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo amelezea safari ya Mamajusi kwa hatua tatu kuanzia Mashariki,kupitia Yerusalemu hadi Bethlemu.Bwana atupatie ujasiri wa kubadili njia,kuongoka,kufuata mapenzi yake na kwenda pamoja kuelekea Yeye.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican.

Hija ya Mamajusi na njia ya uekumene ni mapito yaliyotenganishwa na zaidi ya milenia mbili ya historia, lakini yanaelekezwa na nyota ile ile ya nuru ya Yesu. Katika madhimisho masifu ya Pili ya jioni, katika Katika Kuu la Mtakatifu Paulo mtume,  Nje ya Ukuta Roma, Jumanne tarehe 25 Januari 2022, Jioni  Papa Francisko ameongoza masifu hayo na kuonesha njia ya umoja kamili kuanzia ratiba ya Mamajusi. Walioshiriki maadhimisho hayo ni pamoja na  Askofu Mkuu Polykarpos, mwakilishi wa Upatriaki wa Kiekumene, Ian Ernest, mwakilishi binafsi wa Askofu Mkuu wa Canterbury huko Roma, na wawakilishi wa jumuiya nyingine za Kikristo. Papa katika tafakari yake amekumbusha kwamba safari ya Mamajusi inaanzia Mashariki kwa sababu ni kutoka huko waliona nyota ikitokea. Baadaye wakapitia Yerusalemu, ambapo walipata upinzani wa nguvu za giza za ulimwengu, na kuishia Bethlehemu: ambapo huko waliweza kusujudu na kumwabudu Mtoto.

Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta
Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta

Hata kwenye njia yetu ndefu kuelekea umoja, inaweza kutokea kwamba tunajifunga wenyewe kwa sababu ile ile iliyowapooza watu hao: wasi wasi na hofu. Hofu ya mambo mapya ndiyo inayotikisa mazoea na uhakika uliopatikana; ni hofu kwamba mapya mengine yatavuruga tamaduni yangu na mipango yangu iliyounganishwa. Lakini, katika mizizi yake, ni hofu inayokaa ndani ya moyo wa mwanadamu, ambayo Bwana Mfufuka anataka kutuweka huru. Hebu turuhusu himizo lake la Pasaka lisikike katika safari yetu ya umoja: “Msiogope” (Mt 28,5.10), Papa amesisitiza, Tusiogope kumweka ndugu yetu mbele ya hofu zetu! Bwana anataka tuaminiane na kutembea pamoja, licha ya udhaifu na dhambi zetu, licha ya makosa ya zamani na majeraha ya kila mmoja.

Historia ya Mamajusi pia inatutia moyo katika hili. Huko Yerusalemu, mahali pa kukatisha tamaa na upinzani, ndipo pale ambapo njia iliyooneshwa kutoka Mbingu, utafikiri inataka kupasuka dhidi ya kuta zilizosimamishwa na mwanadamu, na wakagundua njia ya kwenda Bethlehemu. Ni makuhani na waandishi waliotoa maelekezo, baada ya kuyachunguza Maandiko (Mt 2:4). Mamajusi walimkuta Yesu, sio tu shukrani kwa nyota, ambayo ilikuwa imetoweka wakati huo huo; bali wanahitaji Neno la Mungu. Na sisi Wakristo pia hatuwezi kumfikia Bwana bila Neno lake lililo hai na lenye ufanisi (Eb 4:12). Neno lilitolewa kwa Watu wote wa Mungu,  likaribishwe, kuombwa, kutafakariwa pamoja na Watu wote wa Mungu. Papa ameomba kwamba “tumkaribie Yesu kwa Neno lake, lakini pia tuwakaribishe ndugu zetu kwa njia ya Neno la Yesu na kwa kufanya hivyo nyota itatokea tena kwenye njia yetu na itatupatia furaha”.

Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta
Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mamajusi, waliofikia hatua ya mwisho huko Bethlehemu. Humo waliingia ndani ya nyumba, wakiabudu na kumsujudia Mtoto (Mt 2:11). Kwa maana hiyo safari yao iliisha pamoja, katika nyumba moja, kwa kuabudu. Kwa maana hiyo mamajusi walitazamia kama wanafunzi wa Yesu, ambao ni tofauti lakini wakiwa wameungana, mwishoni mwa Injili wanamsujudia Yeye Aliyefufuka kwenye mlima wa Galilaya (Mt 28:17). Hivyo kwa kuwa ishara ya unabii kwa ajili yetu, tunaomtaka Bwana, wenzi wasafirio katika njia ndefu za ulimwengu, watafutaji katika Maandiko Matakatifu ya ishara za Mungu katika historia. Baba Mtakatifu amesema, hata kwa ajili yetu umoja kamili katika nyumba moja, unaweza kuja tu kwa njia ya kumwabudu Bwana. Hatua ya maamuzi ya safari ya kuelekea muungano kamili inahitaji maombi ya kina zaidi, inahitaji kuabudu, inahitaji ibada ya kuabudu Mungu.

Mamajusi, hata hivyo, wanatukumbusha kwamba ili kuabudu kuna hatua ya kuchukua: ni lazima kwanza tusujudu. Hii ndiyo njia, ya kuinama, kuweka kando madai yetu ili kumweka Bwana peke yake katikati. Ni mara ngapi kiburi kimekuwa kikwazo cha kweli kwa ajili ya umoja! Mamajusi walikuwa na ujasiri wa kuacha ufahari na sifa nyumbani, kujishusha kwenye nyumba ndogo ya maskini huko Bethlehemu; hivyo waligundua “furaha kuu sana” (Mt 2:10). Kujishusha, kuacha, kuwa rahisi, ndiyo Baba Mtakatifu ameshauri  usiku wa leo kumwomba Mungu ujasiri huo, ujasiri wa unyenyekevu, njia pekee ya kupata kumwabudu Mungu katika nyumba moja, karibu na altare moja.

Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta
Masifu ya jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta

Huko Bethlehemu, baada ya kusujudu kwa kuabudu, Mamajusi walifungua masanduku yao na dhahabu, ubani na manemane. Hii inatukumbusha kwamba, ni baada tu ya kuomba pamoja, mbele ya Mungu katika nuru yake tu ndipo tunatambua hazina ambayo kila mmoja anayo. Lakini ni hazina ambazo ni za kila mtu, ambazo lazima zitolewe na kushirikishwa. Kwa hakika ni karama ambazo Roho huwagawia watu wote walio wema, kwa ajili ya kuwajenga na kuwaunganisha watu wake. Na tunatambua hilo kwa kuomba, lakini pia kwa kuhudumia: tunapowapatia wale wanaohitaji, tunamtolea Yesu, ambaye anajitambulisha na wale walio maskini na walio pembezoni (Mt 25:34-40); na Anatuunganisha sisi.

Zawadi za Mamajusi zinaashiria kile ambacho Bwana anataka kupokea kutoka kwetu. Dhahabu, kitu cha thamani zaidi, lazima apewe Mungu, kwa sababu Mungu yuko nafasi ya kwanza. Ni kwake yeye tunapaswa kumwangalia, na sio sisi; kwa mapenzi yake, si mapenzi yetu; kwa njia zake si njia zetu. Ikiwa Bwana kweli yuko mahali pa kwanza, chaguzi zetu, hata za kikanisa, haziwezi tena kuegemea kwenye siasa za ulimwengu, bali juu ya matakwa ya Mungu. Na baadaye kuna uvumba, wa kukumbuka umuhimu wa maombi, ambayo Mungu kama manukato yanayokubalika (Zab 141:2). Tusichoke kuomba na kuombeana mmoja na mwingine. Hatimaye, manemane, ambayo yalikuwa yatumike kuheshimu mwili wa Yesu ulioshushwa kutoka msalabani (Yn 19:39), inatuelekeza kwenye utunzaji wa mwili unaoteseka wa Bwana, uliopasuliwa katika viungo vya maskini. Tuwatumikie wahitaji, tumtumikie Yesu anayeteseka pamoja! Papa ameshauri.

Baba Mtakatifu Francisko ameshuri kukaribisha maelekezo kwa ajili ya safari yetu kutoka kwa Mamajusi; nasi tufanye kama wao, waliorudi nyumbani “kwa njia nyingine” (Mt 2:12). Ndiyo, kama Sauli kabla ya kukutana na Kristo, tunahitaji kubadili njia yetu, kuibadilisha dira ya mwenendo wa mazoea yetu na manufaa yetu ili kutafuta njia ambayo Bwana anatuonesha, njia ya unyenyekevu, njia ya udugu, na ya kuabudu. Bwana utupatie ujasiri wa kubadili njia, kuongoka, kufuata mapenzi yako na si fursa zetu; kwenda mbele pamoja, kuelekea Wewe, ambaye kwa Roho wako unataka kutufanya kitu kimoja, amina amehitimisha.

25 January 2022, 19:28