Boresheni Mazingira ya Wafungwa Magerezani Kwa Kudumisha Utu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 19 Januari 2022 kuhusu Mtakatifu Yosefu Baba Mwenye huruma, amewataka watu wa Mungu kuguswa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili hata wao waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, vinginevyo, watabaki wamefungwa bila kuwa na fursa ya kuweza kusimama tena na kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa amewakumbuka na kuwaombea wafungwa na mahabusu magerezani. Ni haki kabisa kwa mkosaji kupewa adhabu kadiri ya makosa yake. Lakini pia ni haki kwa mkosaji kupewa nafasi ya kutubu makosa yake, tayari kuanza kutembea upya katika mwanga wa matumaini. Watu wa Mungu wajitahidi kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na haki ya Mungu, kwa kuwajengea jirani zao matumaini, yatakayosaidia kuboresha maisha yao, kuwa watu bora zaidi, baada ya kumaliza adhabu zao magerezani.
Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu, jamii inapashwa kuboresha hali ya magereza ili kuwawezesha wafungwa wanapomaliza kutumikia adhabu zao, waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida na kwamba, kifungo si laana ya maisha! Wafungwa magerezani wajengewe mazingira mazuri yatakayowawezesha kujifunza stadi za maisha; kuboresha mahusiano na mafungamano yao ya kijamii, ili kuondokana na kishawishi cha kuwatenga watu waliomaliza kutumikia adhabu zao. Hali kama hii itawaongezea machungu. Baba Mtakatifu anawaalika watu kuonja udhaifu wa binadamu badala ya kuwagawa watu katika makundi ya wema na wabaya. Waone ubaya wa dhambi, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umesababisha madhara makubwa katika maisha ya watu, kwani watu wengi wamefariki dunia bila ya kuonja faraja kutoka kwa ndugu, jirani na rafiki zao na hasa wafungwa na mahabusu magerezani. Magereza mengi yamefurika kiasi cha kuhatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Hata wafungwa anasema Baba Mtakatifu wanapaswa kupewa matumaini ya maisha mapya baada ya kumaliza kutumikia adhabu yao. Anasema, waamini wamwombe Mtakatifu Yosefu Baba Mwenye Huruma, awaombee ili Mwenyezi Mungu awajalie: toba na wongofu wa ndani; ari na moyo wa kukimbilia huruma na upendo wake, unaobubujika kwa namna ya pekee, kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho, ili awasamehe dhambi zao. Wakishakusamehewa dhambi zao, na wao pia wawe na uwezo wa kuwapenda na kuwasamehe jirani zao katika umaskini na udhaifu wao wa kibinadamu. Wawe karibu na wote waliotenda makosa, ili kuwafundisha umuhimu wa kuomba na kutoa msamaha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kimsingi mwanadamu ana kiu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.