Tafuta

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya waathirika wakuu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni maskini. Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya waathirika wakuu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni maskini. 

Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Waathirika Wakuu ni Maskini: Hili Ni Janga!

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni matokeo ya kukengeuka kwa jamii, kumong’onyoka kwa kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; utupu wa maisha katika mambo msingi pamoja na kuporomoka kwa mahusiano na mafungamano ya kijamii. Yote haya ni madonda wazi yanayowaandama walimwengu, kiasi cha waathirika kuzamishwa katika janga hili

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamechochea kasi ya kuongezeka kwa matumizi haramu. Ni dhamana na wajibu wa Mama Kanisa kuwasaidia waathirika ili watambue utu, heshima na kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na utegemezi unaoendelea kujitokeza nyakati hizi, ni kikwazo kikuu cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Haya ni matokeo ya kukengeuka kwa jamii, ulaji wa kupindukia; tabia ya kutaka kujitosheleza; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; utupu wa maisha katika mambo msingi pamoja na kuporomoka kwa mahusiano na mafungamano ya kijamii. Yote haya ni madonda wazi yanayowaandama walimwengu, kiasi cha waathirika kukosa uhuru wao kutokana na kuzamishwa katika janga hili ambalo limekuwa ni mwiba kwa utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbalimbali za dunia. Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona dhidi ya biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo miongoni mwa vijana! Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha.

Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji.

Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbalimbali za dunia katika mchakato wa: kuragibisha, kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake. Kumekuwepo na dhana ya kutaka kuruhusu matumizi haramu ya dawa za kulevya, lakini wachunguzi wa mambo wanasema, hii ni hatari kubwa kwani wanyonge ndio waathirika wakuu kama anavyosimulia Malenga Hassan wa Garashi kutoka Tanzania anayesema, waathirika wakuu ni maskini wanaotumiwa na watu wenye fedha zao. 

Dawa za Kulevya

 

03 January 2022, 15:02