Tafuta

Papa anaomba zipatikane suluhishi za mivutano nchini Ukraine kwa njia ya mazungumzo. Papa anaomba zipatikane suluhishi za mivutano nchini Ukraine kwa njia ya mazungumzo. 

Papa Francisko atoa wito kwa siku ya maombi kwa ajili ya amani

Wakati wa kuhitimisha sala ya Malaika wa Bwana katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican,Papa Francisko ameelezea wasiwasi wake juu ya mvutano unaoongezeka na unaotishia amani nchini Ukraine,kwa njia hiyo ametoa wito kuwa Jumatano tarehe 26 Januari 2022 iwe siku ya maombi kwa ajili ya amani.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika hitimisho la sala ya Malaika wa Bwana, kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Dominika, tarehe 23 Januar 2022, Papa Francisko ameelezea wasiwasi wake juu ya mvutano unaoongezeka na ambao unatishia kupindua nafasi ya amani huko Ukraine na usalama katika bara la Ulaya kwa ujumla, kutokana na athari kubwa za migogoro yoyote ile inayojitokeza. Katika kutafuta jibu, Papa  Francisko amependekeza kuwa Jumatano ijayo tarehe 26 Januari 2022 iwe ni siku ya maombi kwa ajili ya amani. Papa Francisko amesema: “Ninatoa wito wa dhati kwa watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa Mwenyezi Mungu ili vitendo na mipango yote ya kisiasa iwe kwa ajili ya udugu wa kibinadamu badala ya masilahi binafsi ya kisiasa”.

Papa Francisko wakati wa tafakari na sala ya Malaika wa Bwana 23 Januari 2022
Papa Francisko wakati wa tafakari na sala ya Malaika wa Bwana 23 Januari 2022

Papa akiendelea amesema kwamba wale wanaofuata malengo yao wenyewe kwa madhara ya wengine, wanaonesha kudharau wito wao kama wanadamu, kwani sisi sote tumeumbwa kuwa kaka na dada. Kwa maana hiyo kufuatia na mivutano hiyo ya mara kwa mara nchini Ukraine , Papa amehimiza kila mtu kuombea amani na kwamba ni mazungumzo ambayo yanaweza kutawala katika kutatua hali kama  hizo.

Waamini wakiudhuria  sala ya Malaika wa Bwana 23 Januari 2022 katika uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini wakiudhuria sala ya Malaika wa Bwana 23 Januari 2022 katika uwanja wa Mtakatifu Petro

Wenye heri wapya huko San Salvador

Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kuwa Jumamosi tarehe 22 Januari huko San Salvador,  Padre mmoja Mjesuit , Rutilio Grande García na walei wawili walitangazwa Wenyeheri, pamoja na Padre Mfransiskani Cosme Spessotto, mashuhuda wa imani. Wao walisimama kidete na kuwa karibu na maskini, wakitoa ushuhuda wa Injili, ukweli na haki hadi kumwaga damu. Mfano wao wa kishujaa na uamshe  shauku yote ya kuwa wakala shupavu wa udugu na amani. Papa Francisko kwa maana hiyo amewaomba watu wote waliokuwa kwenye uwanja kuwapigia makofi Wenyeheri wapya…

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo:kutangazwa kwa Mt Ireneus

Katika muktadha wa Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, Papa Francisko amesema kwamba, alikubali pendekezo kutoka sehemu mbalimbali la kumtangaza Mtakatifu Ireneus wa Lyons, kuwa Mwalimu wa Kanisa la Ulimwengu. Mafundisho ya Mchungaji Mtakatifu huyo na Mwalimu ni kama daraja kati ya Mashariki na Magharibi na ndiyo sababu amesema wanamtaja kama Mwalimu wa Umoja, Doctor Unitatis . “Bwana atujalie, kwa maombezi yake, ili sisi sote tufanye kazi kwa ajili ya umoja kamili wa Wakristo. Kwa kuhitimisha, PFrancisko amewasalimia wapendwa waamini wa Roma,  mahujaji kutoka Italia na sehemu nyingine za Ulimwengu. Kwa namna ya pekee familia ya Kiroho ya Watumishi wa Mateso na Skauti wa Agesci wa Mkoa wa Lazio, Italia. Na pia amewaona kundi  kutoka nchini kwake na kuwasalimia waargentina waliokuwapo hapo. Kwa wote amewatakia Dominika njema na mlo mwema, lakini wasisahau kusali kwa ajili yake.

23 January 2022, 15:29