Tafuta

Papa Francisko amempongeza Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa kuchaguliwa tena kuongoza Italia kwa miaka saba. Papa Francisko amempongeza Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa kuchaguliwa tena kuongoza Italia kwa miaka saba. 

Papa Francisko Ampongeza Rais Sergio wa Italia Kwa Kuchaguliwa

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumhakikishia Rais Sergio Mattarella sala na sadaka yake, ili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kwa watu wa Mungu nchini Italia katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, waweze kukabiliana kwa ujasiri na changamoto mamboleo. Maaskofu pia wamempongeza Rais Sergio.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za heri na pongezi nyingi Rais Sergio Mattarella kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Italia kwa kipindi cha miaka mingine saba hapo Jumamosi tarehe 29 Januari 2022. Anampongeza Rais Mattarella kwa kukubali kujitoa na kuwajibika kwa ukarimu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kumeibuka majanga makubwa, hofu na wasi wasi hasa katika ulimwengu wa kazi, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la umaskini, hali inayowafanya wananchi wengi kujifungia katika ubinafsi wao. Baba Mtakatifu anapenda kumhakikishia Rais Sergio Mattarella kwamba, uongozi na huduma yake kwa watu wa Mungu nchini Italia bado ni muhimu na inahitajika sana ili kuimarisha umoja wa Kitaifa na utulivu nchini Italia. Baba Mtakatifu anapenda kumhakikishia Rais Sergio Mattarella sala na sadaka yake, ili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kwa watu wa Mungu nchini Italia katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, waweze kukabiliana kwa ujasiri na changamoto mamboleo. Watakatifu walinzi na waombezi wa Italia, wamsindikize na kumwombea Rais Sergio Mattarella anapoanza uongozi wake kwa awamu ya pili.

Rais Sergio Mattarella wa Italia amechaguliwa tena kuongoza kwa miaka saba.
Rais Sergio Mattarella wa Italia amechaguliwa tena kuongoza kwa miaka saba.

Kwa upande wake, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, amempongeza Rais Sergio Mattarella kwa kutangaza na kushuhudia umoja wa Kitaifa; akasimamia kikamilifu Katiba ya nchi, ambayo kimsingi ni sheria mama na kwamba, kwa sasa aendelee kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za uhuru na mshikamano wa kidugu kama zinavyobainishwa kwenye Katiba ya nchi ya Italia. Katika kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi wake, amejipambanua kuwa ni mtu wa haki, kiongozi mahiri anayependa kujisadaka kwa ajili ya huduma na rejea kwa watu wa Mungu nchini Italia. Awamu ya pili ya uongozi wake, aendelee kujikita katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa usawa wa kijamii; awaunganishe wananchi wote wa Italia licha ya tofauti zao za kisiasa na kuendelea kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo bado linapukutisha sana maisha ya watu. Kanisa Katoliki nchini Italia, litaendelea kumuunga mkono kwa ajili ya kudumisha utu, heshima; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Makardinali wa Italia wakiwa na Rais Mattarella
Makardinali wa Italia wakiwa na Rais Mattarella

Wakati huo huo, Rais mteule Sergio Mattarella baada ya kutangazwa na Bunge kwamba, amechaguliwa kuwa Rais, amewashukuru viongozi wakuu wa Serikali, Wabunge na wawakilishi wa mikoa mbalimbali ya Italia, waliomwamini na hatimaye, wakaridhia kumpatia kura ili aendelee kuwaongoza wananchi wa Italia. Amesema kwamba, anatambua changamoto zilizojitokeza katika kipindi chote cha uchaguzi wa Rais, bila kusahau wimbi kubwa la maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kuchechemea kwa uchumi pamoja na changamoto pevu zinazoendelea kujitokeza kijamii. Mazingira yote haya yanahitaji kwa namna ya pekee kabisa uwajibikaji na utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa na Bunge. Kila mtu anapaswa kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake, ili kujibu matamanio halali ya wananchi wa Italia. Wananchi wengi wamefurahia Rais Sergio Mattarella kuendelea kuongoza Italia, lakini moto unawaka katika vyama vya kisiasa kwa kushindwa kusoma alama za nyakati! Huu ni ushindi wa kishindo “Tsunami kutoka kwa wananchi wa Italia” waliosimama kidete na kukataa kuyumbishwa yumbishwa na wanasiasa kwa ajili ya masilahi ya vyama vyao na watu binafsi.

Rais Italia

 

30 January 2022, 14:57