Tafuta

Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, Jumamosi tarehe 22 Januari 2022, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Padre Rutilio Grande, SJ., na wenzake Mashahidi wametangwa kuwa ni Wenyeheri. Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, Jumamosi tarehe 22 Januari 2022, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Padre Rutilio Grande, SJ., na wenzake Mashahidi wametangwa kuwa ni Wenyeheri. 

Mwenyeheri Rutilio Grande na Wenzake: Imani, Msamaha & Upatanisho

Wenyeheri wapya walijisadaka kwa ajili ya huduma ya Injili kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mashuhuda wa Injili, Ukweli na Haki, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wao wa ujasiri, uamshe ndani ya waamini kiu ya kuwa wajasiri na vyombo vya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Rutilio Grande, SJ., na wenzake Mashahidi wawili walei: Manuel Solórzano pamoja na Nelson Rutilio Lemus, waliuwawa kikatili kunako mwaka1977. Na Padre Cosma Spessotto wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Wafrancisko wa Assisi aliuwawa kunako mwaka 1980. Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la San Salvador nchini El Salvador, Jumamosi tarehe 22 Januari 2022, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Padre Rutilio Grande, SJ., na wenzake Mashahidi wametangwa kuwa  ni Wenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya III ya Neno la Mungu, tarehe 23 Januari 2022, amewakumbuka na kuwataka waamini kuwa ni mashuhuda wa imani. Wenyeheri wapya walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mashuhuda wa Injili, Ukweli na Haki, kiasi hata cha kuweza kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wao wa ujasiri, uamshe ndani ya waamini kiu ya kuwa wajasiri na vyombo vya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki na amani.

Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la San Salvador nchini El Salvador, katika mahubiri yake, amesema kwamba, hawa ni “watoto wa nyumbani” walioandika historia ya maisha yao kwa furaha, matumaini, machungu na hali ya kukata tamaa. Ni Mashuhuda wa imani waliopitia dhuluma na nyanyaso nyingi hadi kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni ushuhuda ambao kamwe hautaweza kusahaulika kwa watu wa Mungu ndani na nje ya El Salvador. Ni mashuhuda wa imani walioitupa mkono dunia, huku wakitoa msamaha wa kweli katika maisha. Kardinali José Gregorio Rosa Chávez amesema ni kutokana na uvumilivu wa mateso, nyanyaso na dhuluma, leo hii, Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi utenzi wa sifa na shukrani,  kwa Mashuhuda hawa wa imani kutangazwa kuwa Wenyeheri. Hawa ni kati ya waamini 75, 000 waliouwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, hadi tarehe 16 Januari 1992 Mkataba wa Amani wa El Salvador ulipotiwa saini na hivyo kusitisha vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo ilisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kwa hakika kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa watu wa Mungu nchini El Salvador. Hii ni changamoto kwa viongozi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya majadiliano katika ukweli, uwazi, sanjari na upatanisho, daima wakijielekeza kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wenyeheri wa El Salvador
Wenyeheri wa El Salvador

Padre Rutilio Grande na Mashuhuda wenzake wa imani wamepitia mateso, nyanyaso na madhulumu. Wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo. Rej, Ufu 7:14. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilisababisha chuki, uhasama, uharibifu na vifo vya watu wasiokuwa na hatia. Mwenyezi Mungu amesikiliza na kujibu kilio cha watu wake, Mashuhuda wa imani wakayamimina maisha yao na sasa wameunganika na Kristo Yesu. Ni Mashuhuda waliouwawa kikatili mbele ya Altare na hivyo kupelekea Altare na Kanisa zima kunajisiwa kutokana na uchu wa madaraka; fedha, mali na umaarufu usiokua na tija wala mashiko. Lakini, damu ya Mashuhuda wa imani kwa sasa imekuwa ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Bro Cosimo Spessotto alikuwa na Ibada kubwa kwa Ekaristi Takatifu, maisha ya sala na huduma kwa wagonjwa.

Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, anakaza kusema, hawa ni mashuhuda wa imani ambao haitakuwa rahisi sana kuweza kusahauliwa, kwani kumbukumbu yao imekita mizizi katika akili na nyoyo za watu wa Mungu. Hii ni kumbukumbu inayoweza kumwilishwa tu katika maisha ya sala. Padre Rutilio Grande na wenzake, baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ni kipindi ambacho kimesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Kumbe, kwa hakika, Mashuhuda wa imani ni kumbukumbu ya matumaini, amani na upatanisho. Mashuhuda wa imani, waliitupa mkono dunia, huku wakiwa wanatoa msamaha na zaidi kwa kuombea: haki, amani na upatanisho wa kudumu.

Kardinali José Gregorio Rosa Chávez, Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la San Salvador nchini El Salvador, amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Mashuhuda wa imani ni kumbukumbu endelevu inayosimikwa katika matumaini, ili kuendelea kusimama kidete katika mchakato wa upatanisho; haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Huu ni muda wa kujikita katika uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama kielelezo cha imani tendaji. Kanisa likumbuke kwamba, ni sawa na uwanja wa mapambano, linalopaswa kutangaza na kushuhudia Uso wa huruma, upendo na wema wa Mungu. Kanisa halina budi kuwa maskini kwa ajili ya maskini.

Wenyeheri El Salvador
25 January 2022, 15:00