Mshikamano wa Papa Francisko Kwa Watu wa Mungu Nchini Brazil
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Brazil imekumbwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo na hivyo kupelekea watu zaidi ya 270 kupoteza maisha. Zaidi ya watu 28, 000 hawana makazi ya kudumu baada ya nyumba zao kubomoka kutokana na mvua kubwa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 16 Januari 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa watu wa Mungu nchini Brazil, walioguswa na kutikiswa na maafa haya makubwa, licha ya maambukizi na madhara makubwa yanayosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Baba Mtakatifu anawaombea kwa namna ya pekee waathirika pamoja na familia zao pamoja na wote waliopoteza makazi yao. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awatie shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika na maafa haya makubwa! Wakati huo huo, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Brazil, Caritas Brazil, yanaendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa waathirika huko nchini Brazil.