Tafuta

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mama Kanisa pia anatumia fursa hii kutangaza Pasaka ya Bwana itakayoadhimishwa tarehe 17 Aprili 2022 Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mama Kanisa pia anatumia fursa hii kutangaza Pasaka ya Bwana itakayoadhimishwa tarehe 17 Aprili 2022  (Vatican Media)

Mbiu ya Pasaka ya Bwana Kwa Mwaka 2022: Sherehe na Sikukuu za Kanisa

Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi yaani Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu; Yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 17 Aprili 2022.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 17 Aprili 2022.

Kila Dominika, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Sikukuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 2 Mwezi Machi 2022 kwa kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 29 Mei 2022 na Pentekoste, Sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei itaadhimishwa hapo tarehe 5 Juni 2022.

Jumapili ya kwanza ya Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo itaadhimishwa hapo tarehe 27 Novemba 2022. Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Sherehe na Sikukuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Sikukuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake, ni Alfa na Omega. Amina.

Pasaka ya Bwana 2022

 

06 January 2022, 14:56