Tafuta

Safari ya Majadiliano ya Kiekumene: Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtafuso wa Nicea: 2025 na Ungamo la Augusta, Miaka 500 kunako mwaka 2030: Lengo ni umoja wa Wakristo. Safari ya Majadiliano ya Kiekumene: Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtafuso wa Nicea: 2025 na Ungamo la Augusta, Miaka 500 kunako mwaka 2030: Lengo ni umoja wa Wakristo. 

Majadiliano ya Kiekumene: Miaka 1700 ya Nicea na 500 ya Ungamo la Augusta.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Hija ya pamoja katika majadiliano ya kiekumene, Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 pamoja na Jubilei ya Miaka 500 tangu kutokea kwa "Ungamo la Augusta.” Lengo ni kudumisha upatanisho, kuganga na kuponya utengano miongoni mwa Wakristo duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Tafakari ya kuombea umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2022 imeandaliwa na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati na linahitimishwa kwa Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa hapo tarehe 25 Januari 2022. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Januari 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa kiekumene kutoka nchini Finland wanaohiji mjini Roma kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Henrik, Mlinzi na Mwombezi wa nchi ya Finland. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Hija ya pamoja katika majadiliano ya kiekumene, Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 pamoja na Jubilei ya Miaka 500 tangu kutokea kwa "Ungamo la Augusta.” Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa kiekumene kwa kuendeleza hija ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayopania kudumisha upatanisho, kuganga na kuponya utengano miongoni mwa Wakristo, ili kwa kuwa huru waweze kujikita katika kutafuta ukweli; wanapoteleza, wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele na safari.

Kama ilivyokuwa kwa Mamajusi waliweza kuhitimisha hija ya maisha yao ya kiroho kwa kumwona Mtoto Yesu, wakamwangukia na kumwabudu. Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa aliyejitaabisha kuwatafuta kwanza waja wake, kwa njia ya neema azidi zaidi kuwavuta kwake na wao kazi yao kubwa iwe ni kumfuasa kama walivyofanya Mamajusi, safari inayopaswa kutekelezwa katika umoja. Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu walioguswa na neema ya Mungu, wanahimizwa kutembea kwa pamoja, huku wakisonga mbele kwa ari na moyo mkuu, kama wajumbe wa kiekumene walivyofanya hapa mjini Roma. Haya ni mapokeo ambayo yamedumu kwa takribani miaka 37, changamoto endelevu, ili kuondokana na giza la utengano na kuanza kujielekeza katika umoja wa Kanisa kama ndugu wamoja, ili kujenga umoja wa Kanisa unaoonekana. Katika hija ya kiekumene, Wakristo wasaidiane, ili kuwa karibu zaidi na Mungu “magis et magis at Deum” kama anavyosema Mtakatifu Benedikto Abate. Ulimwengu unahitaji mwanga wa Mungu unaong’ara katika upendo, ushirika na udugu wa kibinadamu. Safari ya upendo inawawezesha kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, maskini na wahitaji na wao wenyewe kushikamana kwa dhati. Kuna wakati hija hii inakuwa ni ngumu, kiasi cha kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa, hali inayoweza kuwatumbukiza katika kishawishi cha kujikatia tamaa.

Katika hali na mazingira kama haya, Wakristo wajitambulishe na wale wanaomtafuta Mungu, katika unyenyekevu, uvumilivu na mshikamano wa kidugu. Wakristo wote wasaidiane katika shida na kama wanahitaji kusimama kidogo wasimame ili kujichotoea nguvu sanjari na kupambanua malengo waliyojiwekea. Kuna matukio makubwa mawili ambayo yako mbele ya Wakristo wote. Mosi, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua.

Kuna matukio mbalimbali yanayoadhimishwa na Kanisa katika Kipindi cha Miaka 10 kuanzia mwaka 2021 na kilele chake ni hapo mwaka 2030, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kutokea kwa "Ungamo la Augusta": linalojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Confessio Augustana" lililosaidia kurejesha umoja wa Kanisa, wakati ambapo Makanisa yalikuwa yameanza kusambaratika, kila Kanisa katika njia yake. Makanisa yanataka kuanza kwa umoja, ili kuendelea kujizatiti katika mambo yale yanayowaunganisha zaidi, ili kufanya kazi kwa pamoja, kwa kushinda kiburi na hali ya kutoaminiana. Hija ya majadiliano ya kiekumene inajielekeza zaidi katika mchakato wa upatanisho, kwa kutambua na kukiri machungu ya historia ya utengano kati ya Makanisa. Hii ni hija ya ushirika kwa kujinyenyekesha mbele ya Mungu ili kutekeleza mapenzi yake na wala si mikakati ya kibinadamu, daima wakipania kupata ya mbinguni. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza kwa hija hii ya kiekumene, ili kwa pamoja waendelee kumtafuta Mwenyezi Mungu, huku wakimtazama Kristo Yesu, Rej. Ebr 12:2 pamoja na kujenga ukaribu kati yao kwa njia ya sala.

Ujumbe wa Kiekumene

 

17 January 2022, 14:49