Dominika ya III ya Neno la Mungu: Usomaji, Utumishi na Makatekista
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kwa Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu Proprio ya “Spiritus Domini” yaani “Roho wa Bwana”: Utume wa Waamini Walei kutoka katika Ubatizo”, anasema, kuanzia sasa wanawake wenye sifa wanaweza kupewa daraja dogo la usomaji na utumishi Altareni. Hii ina maana kwamba, wanawake wanaweza kusaidia kugawa Ekaristi Takatifu. Madaraja haya yatatolewa katika Ibada maalum. Uamuzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Utume huu wa waamini walei unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na unatofautiana na huduma ya Daraja Takatifu ya Upadre. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya III ya Neno la Mungu, tarehe 23 Januari 2022, atatoa kwa waamini walei Daraja dogo la usomaji na utumishi Altareni kwa waamini walei walioandaliwa vyema. Hawa ni waamini walei kutoka Korea ya Kusini, Pakistan, Ghana na Majimbo mbalimbali ya Italia. Roho Mtakatifu ni kiunganishi cha mapendo kati ya Baba na Mwana. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini ambao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa wanampokea Roho Mtakatifu kadiri ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa.
Hizi ni zawadi na karama za Roho Mtakatifu zinazowawezesha kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mtakatifu Paulo, Mtume, anatofautisha kati ya karama “charismata” na huduma “diakonia”. Kumbe, ndani ya Kanisa kuna karama na huduma. Daraja Takatifu ni Sakramenti ya Huduma ambayo imegawanyika katika madaraja makuu matatu yaani: Daraja ya Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Baadhi ya huduma zinazotolewa na Mama Kanisa zinatekelezwa na waamini walei kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa hata pengine bila ya kutambuliwa rasmi. Kuna utume unaotekelezwa na waamini walei pamoja na huduma inayofanywa na waamini waliodarajiwa yaani: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Verbum Domini” alisema kwamba, Daraja dogo la Usomaji ni huduma ya waamini walei.Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, pamoja na mabadiliko yote haya, lakini Mama Kanisa hana nia ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa wanawake, kama alivyowahi kutamka Mtakatifu Yohane Paulo II. Mama Kanisa anapenda kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu pamoja na kuendelea kutia nia ya kuishi, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyotangazwa na Mitume pamoja na waandamizi wao, ili kweli, Kanisa liweze: kulisikiliza, kulihifadhi kitakatifu na kulitangaza kiaminifu. Mama Kanisa anataka kumtumikia Mungu na watu wake kwa uaminifu mkubwa.
Mabadiliko haya yanapania pamoja na mambo mengine, kuwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; kwa kushiriki kinagaubaga katika kutoa maoni na maamuzi muhimu katika maisha ya jamii wanamoishi. Ukuhani wa Ubatizo na Ukuhani wa Daraja ni muhimu kwa ajili ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kwa muda wa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitoa huduma ya usomaji wa Neno la Mungu na Utumishi Altareni kwani yote haya yanapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko kwa Barua yake Binafsi "Motu Proprio", "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” ameanzisha Huduma ya Katekista ambayo kimsingi ni huduma kale. Maandiko Matakatifu yanataja huduma mbalimbali zinazotolewa na Mama Kanisa. Mwenyezi Mungu katika Kanisa ameweka: Mitume, Manabii, Walimu, watenda miujiza pamoja na watu waliokirimiwa karama mbalimbali za Roho Mtakatifu. Rej. 1Kor. 12:28-31.
Mwinjili Luka katika utangulizi wa Kitabu cha Matendo ya Mitume anaelezea umuhimu wa mafundisho yake kwa Wakristo na kwamba, kuna haja ya kushirikishana tunu msingi za maisha kama alama na matunda ya Katekesi ya kweli. Karama mbalimbali ndani ya Kanisa zilipania kutoa huduma kwa ajili ya Jumuiya yaani “Diakonia”. Mtakatifu Paulo Mtume, anatambua Karama za Roho Mtakatifu na tofauti zake, lakini zote zinapata chanzo na asili yake kutoka kwa Roho Mtakatifu anayemgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye! Rej. 1Kor. 12: 4-11. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwamba, kuna mafundisho ambayo Mitume waliwarithisha baadhi ya waamini na kuwasihi kuyahifadhi Mapokeo waliyopokea, wapiganie imani, ili Kanisa liweze kuishi katika utakatifu na kukuza imani. Mama Kanisa anakiri kwa dhati kabisa kwamba, huduma hii imesaidia katika utume wa uinjilishaji na kwamba, Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapongeza njia mbalimbali zinazoendelea kujitokeza ili kuliwezesha Kanisa lenyewe liendelee kuwa aminifu kwa Neno la Mungu, ili kwamba, Injili Takatifu iweze kuhubiriwa kwa kila kiumbe.
Katika kipindi cha miaka elfu mbili iliyopita, watawa wameonesha ufanisi mkubwa katika maisha na utume wao. Wakleri na watawa wameendelea kujisadaka kwa ajili ya kufundisha Katekesi, ili kwamba katekesi iweze kuwa ni chombo madhubuti cha kuimarisha imani kwa watu wote. Kuna baadhi ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ambayo yameendelea kujipambanua kwa ajili ya kufundisha Katekesi. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Dominika ya III ya Neno la Mungu, tarehe 23 Januari 2022 Baba Mtakatifu Francisko atatoa Huduma kwa Makatekista walei kutoka katika Vikarieti ya Yurimaguas, huko nchini Perù na wengine wawili kutoka nchini Brazil, wanaojihusisha na malezi na majiundo endelevu ya Makatekista nchini Brazil. Kanisa Barani Afrika linawakilishwa na Mama mmoja kutoka, Kumasi, nchini Ghana, waamini wawili walei kutoka Hispania na Italia. Kwa bahati mbaya, waamini wawili kutoka Congo DRC hawataweza kuhudhuria tukio hili la kihistoria kutokana na changamoto za kiafya hususan kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Mama Kanisa anawakumbuka kwa heshima na taadhima waamini walei waliojisadaka usiku na mchana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa njia ya mafundisho ya Katekesi. Hawa ni watu waliokuwa na imani thabiti na mashuhuda wa utakatifu wa maisha, baadhi yao wakaanzisha Makanisa na wengine kuitupa mkono dunia kwa njia ya ushuhuda wa kifodini. Hata leo hii, kuna Makatekista mashuhuri ambao ni viongozi wa Jumuiya zao na wanasaidia pia kurithisha na ukuzaji wa imani. Kuna jeshi kubwa la wenyeheri, watakatifu na mashuhuda ambao ni Makatekista waliolisongesha mbele Kanisa na kwa hakika wanahitaji kutambuliwa, kwa sababu wao ni utajiri mkubwa na amana ya Katekesi pamoja na historia nzima ya tasaufi ya Kikristo.