Tafuta

Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa ni Baba na Mlezi kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya vijana. Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa ni Baba na Mlezi kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kuendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya vijana. 

Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco: Baba na Mlezi wa Vijana

Katika maisha na utume wake miongoni mwa vijana, Mtakatifu Yohane Bosco aliwataka vijana kuhakikisha kwamba, wanafuata kanuni ifuatayo kama sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha! Aliwataka vijana wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili; wasome kwa bidii, juhudi na maarifa; wasali kwa Ibada na uchaji na mwisho wa yote haya wayamwilishe katika matendo mema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Bosco, Padre, Baba na Mwalimu wa vijana wa kizazi kipya, anakumbukwa na kuadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari. Ni Padre aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa vijana waliokimbilia mjini Torino, Kaskazini mwa Italia kutafuta fursa za ajira baada ya kutokea kwa Mapinduzi ya Viwanda wakati huo. Kwa kusoma alama za nyakati, akaanzisha mahali pa kuwakutanisha vijana, akawapatia malezi, makuzi na majiundo makini ya kitaaluma na huo ukawa ni mwanzo wa Vituo vya michezo na malezi ya vijana Parokiani “Oratorio”. Mtindo wake wa elimu na makuzi kwa vijana ukawa ni dira na mwongozo wa Mtakatifu Francisko wa Sale, Muasisi wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika, tarehe 30 Januari 2022 ametumia fursa hii, kutoa salam na matashi mema kwa Wasalesian wa Don Bosco katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu mwanzilishi wa Shirika lao. Amewashukuru na kuwapongeza kwa maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Amesema, amefuatilia kwa makini Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, iliyokuwa inaongozwa na Padre Ángel Fernández Artime, Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Baba Mtakatifu anasema, ameungana nao pamoja na kuwaombea. Mtakatifu Yohane Bosco alijisadaka sana kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, akatoka kimasomaso kwenda mitaani kuwatafuta na kuwaonjesha kipaji cha ubunifu.

Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa Baba na Mlezi wa Vijana
Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa Baba na Mlezi wa Vijana

Mtakatifu Yohane Bosco katika maisha na utume wake miongoni mwa vijana, aliwataka vijana kuhakikisha kwamba, wanafuata kanuni ifuatayo kama sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha! Aliwataka vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili; wasome kwa bidii, juhudi na maarifa; wasali kwa Ibada na uchaji na mwisho wa yote haya wayamwilishe katika matendo mema. Mtakatifu Yohane Bosco hakuwa na Katekesimu ya Kanisa Katoliki, bali mikononi mwake alibeba Msalaba, kielelezo cha hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Alithubutu kuandamana na vijana wa kizazi kipya katika Njia ya Msalaba wa maisha yao, kiasi kwamba, kwa vijana hawa akawa ni Baba, Mwalimu na Mlezi, sifa kuu za Padre mwema na Mkristo bora. Maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco yalijikita katika huduma kwa vijana, hususan: maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa wakafundishwa imani inayojikita katika kanuni ya maisha ya Wasalesiani yaani, “Kuinjilisha kwa njia ya kuelimisha na kuelimisha ili Kuinjilisha.”

Mtakatifu Yohane Bosco aliwataka vijana kuwa wabunifu
Mtakatifu Yohane Bosco aliwataka vijana kuwa wabunifu

Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, Familia ya Wasalesiani haina budi kuendelea kujikita katika ukarimu na imani; tunu msingi zinazopaswa kuambata mikakati na shughuli mbalimbali za kitume zinazotekelezwa na Wasalesiani sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya. Ni mikakati inayomwilishwa katika vituo vya michezo, vituo vya vijana, taasisi za kitaaluma, shule, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Yote haya yafanyike bila kuwasahau vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Hawa ni vijana ambao wanahitaji kwa namna ya pekee kuonjeshwa: matumaini na kufundwa katika furaha inayobubujika kutoka katika kisima cha maisha ya Kikristo. Mtakatifu Yohane Bosco alikuwa ni mnyenyekevu na mwaminifu kwa Kristo Yesu na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alikuwa tayari kufuata maelekezo aliyopewa na viongozi wa Kanisa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto wa kiroho wa Mtakatifu Yohane Bosco kutoka ili kwenda kukutana na vijana huko waliko kwenye maskani yao; pembezoni mwa miji mikuu; katika maeneo ambamo kuna hatari za maisha ya kiroho na kimwili; katika mazingira ya kijamii ambako kuna uhaba na ukata wa mambo msingi katika maisha. Haya ni maeneo ambayo kimsingi yanakosa: upendo, uelewa, wema na matumaini.

Papa: Yohane Bosco
31 January 2022, 15:38