Tafuta

Papa Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia mjini Vatican amekazia umuhimu wa majadiliano unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Papa Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia mjini Vatican amekazia umuhimu wa majadiliano unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. 

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Wanadiplomasia Kwa Mwaka 2022

Papa Francisko amekazia: Ujenzi wa familia ya binadamu ili kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu UVIKO-19 na umuhimu wa chanjo kwa watu wote; hali tete ya Lebanon; hija za kitume; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi; athari za mabadiliko ya tabianchi; diplomasia shirikishi inayosimikwa katika majadiliano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa Mwaka 2022, tarehe 10 Januari amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu ili kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu UVIKO-19 na umuhimu wa chanjo kwa watu wote; hali tete ya Lebanon; hija za kitume nchini Iraq, Hungaria, Slovakia, Cyprus na Ugiriki. Amezungumzia kuhusu changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; athari za mabadiliko ya tabianchi; umuhimu wa kuendeleza diplomasia shirikishi inayosimikwa katika majadiliano na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kukuza msingi wa haki jamii dhidi ya rushwa na umaskini wa hali na kipato. Biashara haramu ya silaha duniani inaendelea kusababisha majanga na maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha: elimu, kazi na majadiliano Kati ya vizazi: nyenzo za ujenzi wa amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu Francisko amewaambia wanadiplomasia kwamba, wanakutana kama wanafamilia, ili kutakiana heri na baraka kwa mwaka 2022 na hatimaye, kupembua kwa makini yale yaliyojiri katika kipindi cha mwaka 2021 na kuyaangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini. Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yanahitaji nguvu ya ziada kutokana na madhara yake. Baba Mtakatifu amemkumbuka Hayati Askofu mkuu Aldo Giordano, ambaye kwa miaka mingi amekuwa Balozi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia. UVIKO-19 unahitaji kwanza kabisa juhudi binafsi za kulinda na kutunza afya kwa kuwalinda pia jirani. Huduma ya afya ni hitaji msingi la kimaadili. Chanjo dhidi ya magonjwa ni nyenzo inayotumika kuzuia magonjwa. Wanasiasa hawana budi kujielekeza zaidi katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuweka sera na mikakati ya kuzuia na kukinga watu dhidi ya maambukizi ya magonjwa. Ukweli na uwazi unapaswa kuzungatia ili kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, amani na utulivu badala ya kusababisha kinzani na mipasuko ya kijamii. Shirika la Afya Duniani, WHO halina budi kuwajibika barabara ili kutoa majibu muafaka dhidi ya UVIKO-19. Kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali, Jumuiya ya Kimataifa iwe na uwezo wa kuzalisha chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa ajili ya wote. 

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi cha mwaka 2021 alibahatika kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali. Tarehe 1 Julai 2021 Papa Francisko alikutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Jumuiya za Kikristo nchini Lebanon. Hii ilikuwa ni Siku ya Sala na Tafakari kwa ajili ya Lebanon ambayo imetumbukia katika hali mbaya ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ni matumaini yake kwamba, Lebanon itaendelea kushikamana na kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mafungamano ya kijamii. Amezungumzia hija zake za kitume nchini Iraq ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ametembelea Hungaria na kushiriki katika maadhimisho ya 52 ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa na kukazia umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga udugu wa kibinadamu. 

Baba Mtakatifu anasema, alipata nafasi ya kushuhudia kwa macho yake mwenyewe mateso, mahangaiko na matamanio ya wakimbizi na wahamiaji kwenye Visiwa vya Lesvos nchini Ugiriki. Ameyapongeza Mataifa ambayo yamekuwa tayari: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Ameonya tabia ya kuwageuza wakimbizi na wahamiaji kuwa ni chanzo cha chokochoko za kisiasa na matokeo yake ni watu kuendelea kupoteza maisha na wengine kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapaswa kuwa na msimamo mmoja kuhusu wakimbizi na wahamiaji, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wana haki na nyajibu zao.  Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto za Kimataifa zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa umoja na ushirikiano, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbata udugu wa kibinadamu na diplomasia ya Kimataifa ambayo inapaswa kuwa ni shirikishi kwa kutambua haki msingi za binadamu. Wakimbizi na wahamiaji wana haki na utambulisho wao. Kumbe, kuna haja ya kuondokana na ukoloni wa kiitikadi unaotaka kuondoa tofauti msingi kati ya mume na mke.

Diplomasia shirikishi ni jukwaa linalopaswa kuwakutanisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili kujadili changamoto, matatizo na fursa za Jumuiya ya Kimataifa kama inavyopaswa kuwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.  Kuna nchi ambazo zinaendelea kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi wengi hasa wakulima wanaotegemea kilimo kwa maisha yao. Utandawazi uiwezeshe Jumuiya ya Kimataifa kupata suluhu za Kimataifa na kuzifanyia kazi. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland kwa mwaka 2021 ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani! Kuna hatua ambayo imepigwa, lakini bado kuna changamoto kubwa. Mkutano wa COP27 unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2022 huko nchini Misri unalenga kuimarisha maazimio yaliyofikiwa huko Glasgow.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa majadiliano yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na vita huko Siria na Yemen; Israeli na Palestina; Libya, Sudan ya Kusini na Ethiopia pamoja na Ukraine, bila kusahau umuhimu wa kudumisha amani na utulivu huko Bosnia-Erzegovina. Myanmar inaonekana kusahaliwa na Jumuiya ya Kimataifa. Vita na kinzani zote hizi ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani, kwani kama anavyosema Mtakatifu Paulo VI huwezi kumpenda mtu ukiwa na silaha za maangamizi mikononi. Mantiki ya matumizi ya silaha yanafifisha umuhimu wa majadiliano na matokeo yake ni matumizi ya silaha.  Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani, kikwazo kikubwa katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mama Kanisa anakazia majadiliano yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu. 

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januari 2022 umenogeshwa na kauli mbiu “Elimu, Kazi Na Majadiliano Kati ya Vizazi: Nyenzo za Ujenzi wa Amani ya Kudumu.” Kanisa Katoliki katika maisha na utume wake, linatambua na kuthamini elimu kama sehemu ya mchakato wa ukuaji wa vijana wa kizazi kipya: kiroho, kimaadili na kijamii. Kanisa linasikitishwa sana kwa baadhi ya maeneo kutumiwa na baadhi ya watu kuwa ni sehemu za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. UVIKO-19 umesababisha madhara makubwa kwa wanafunzi katika ngazi mbalimbali. Jamii inapaswa kupambua athari za matumizi ya mitandao ya kijamii, ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi mbalimbali, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Kazi ni msingi wa haki na mshikamano wa kila jumuiya. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kuhakikisha kwamba, watu wanapata fursa za ajira na wala nafasi zao hazichukuliwi na mashine. Kwa sababu kazi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu hapa duniani, inayomsaidia kukua na kutekeleza malengo yake sanjari na kudumisha amani.

Papa Diplomasia

 

 

12 January 2022, 15:19