Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu anazaliwa katika mazingira ya upendo unaomwilishwa katika huduma ya udugu na ujirani mwema. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu anazaliwa katika mazingira ya upendo unaomwilishwa katika huduma ya udugu na ujirani mwema.  

Kristo Yesu Anazaliwa Mahali Penye Upendo Na Ujirani Mwema!

Mwenyezi Mungu anazaliwa pale ambapo fadhila ya upendo inamwilishwa na kuwa ni kielelezo cha ujirani mwema, huruma na upendo wa Mungu. Familia zijifunze kudumisha mahusiano mema kifamilia, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kuwalinda na kuwatunza wazee, wagonjwa na maskini na kamwe wasitumbukie katika utamaduni wa kutupa na utandawazi usiojali wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kukutana na kuzungumza na Makardinali, Maaskofu wakuu na familia ya Sekretarieti kuu ya Vatican, Alhamisi, tarehe 23 Desemba 2021 amekutana na kuzungumza pia na wafanyakazi wa Vatican pamoja na familia zao kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2021 na kuwakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kufanya maskani yake pale ambapo kuna upendo wa dhati kwani “Palipo na upendo, hapo Mungu yupo.” Mwenyezi Mungu anazaliwa pale ambapo fadhila ya upendo inamwilishwa na kuwa ni kielelezo cha ujirani mwema, huruma na upendo wa Mungu. Familia zijifunze kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kifamilia, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kuwalinda na kuwatunza wazee, wagonjwa na maskini na kamwe wasitumbukie katika utamaduni wa kutupa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Palipo na upendo ni mahali ambapo matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanamwilishwa kama kielelezo cha imani tendaji. Kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bado watu wengi sehemu mbalimbali za dunia wanaishi katika hofu na wasiwasi mkuu kuhusu hatima ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote wenye shida, magumu na changamoto za maisha, wapate faraja na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Janga la UVIKO-19 limesababisha madhara makubwa katika mahusiano na mafungamano ya kifamilia na kijamii katika ujumla wake. Limesababisha ukosefu mkubwa wa fursa za ajira sanjari na kuporomoka kwa uchumi kitaifa na Kimataifa, bila kusahau madhara makubwa yaliyosababishwa kisaikolojia na waathirika wakuu ni watoto na vijana wa kizazi kipya waliolazimika kukaa kwa muda mrefu kwenye karantini ili kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Kwa wanafunzi wengi, walilazimika kusoma kwa njia ya mitandao, lakini katika yote, kila kundi limeathirika kwa namna moja au nyingine anasema Baba Mtakatifu Francisko. Vatican kwa upande wake, itaendelea kuimarisha fursa za ajira kwa wafanyakazi wake, hata kama kwa sasa kuna matatizo na changamoto zake, zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano, kwa kukutana pamoja na kuheshimu haki msingi za wafanyakazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wawasaidie na kuwaombea katika hija ya maisha ya familia zao. Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali.

Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu katika shida, mahangaiko na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mtakatifu Yosefu katika ukimya wake, alibahatika kuwa na kipaji cha kusikiliza na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, kiasi cha kulinda na kumhifadhi Mtoto Yesu aliyekuwa anakabiliwa na mauaji kutoka kwa Mfalme Herode.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wake. Ikumbukwe kwamba, familia ni mahali muafaka ambapo watu wanaonja wema, huruma, upendo na tunza ya Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha yao kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Si rahisi sana kuweza kutambua mapenzi ya Mungu na kuyatenda kwa ukamilifu, kumbe, waamini wanapaswa kuwa na imani, matumaini, mapendo thabiti na uvumilivu, wanaposali na kumwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili waweze kupata furaha, amani na utulivu wa ndani.

Wafanyakazi Vatican

 

23 December 2021, 15:42