Tafuta

Papa Francisko asema, Kanisa Katoliki litaendeleza majadiliano ya kiekumene na Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Mchungaji mkuu Kristo Yesu. Papa Francisko asema, Kanisa Katoliki litaendeleza majadiliano ya kiekumene na Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Mchungaji mkuu Kristo Yesu. 

Kanisa Katoliki Kudumisha Majadiliano ya Kiekumene na Kanisa la Kiorthodox la Urussi

Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev yaliyofanyika katika hali ya udugu wa kibinadamu, wamegusia mambo msingi, nyeti na tete katika maisha na utume wa Kanisa ili hatimaye, waweze kupata majibu kwa ajili ya machangamoto zake: kiroho na kimwili. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni muhimu kwa utume wa Kanisa la Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika mahojiano maalum na waandishi wa habari baada ya hija yake ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki kuhusu mchakato wa majadiliano ya kiekumene alisema, hivi karibuni anatarajia kukutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi nzima na kwamba, yuko tayari kwenda nchini Urussi ili kutekeleza azma hii ya kiekumene, ili wote wawe wamoja chini Kristo Yesu mchungaji mkuu. Angependa kukutana na kuzungumza naye ana kwa ana kama ndugu wamoja. Mpasuko wa Kanisa wengine wameurithi na wengine ni sehemu ya historia, kumbe, kuna haja ya kuanza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja. Baba Mtakatifu anatambua nia njema ya viongozi wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox wanaoendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Patriaki Anathegoras. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 10 Agosti 1964, akachapisha Waraka wake wa kwanza wa kichungaji, unaojulikana kama "Ecclesiam suam” yaani "Kanisa la Bwana.” Huu ni Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Patriaki Cyrill au Kirill wa Moscow na Urussi nzima walikutana na kuzungumza kwa mara ya kwanza tarehe 12 Februari 2016, huko Cuba, wakati Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Mexico. Patriaki Cyrill wa Moscow alikuwa nchini Cuba kwa ziara ya kitume. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk ambaye pia ni Mjumbe wa Sinodi Takatifu na Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya nje ya Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow nzima tarehe 22 Desemba 2021, amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev yaliyofanyika katika hali ya udugu wa kibinadamu, wamegusia mambo msingi, nyeti na tete katika maisha na utume wa Kanisa katika ujumla wake, ili hatimaye, waweze kupata majibu muafaka kwa ajili ya shida na machangamoto zake: kiroho na kimwili.

Patriaki Cyrill au Kirill wa Moscow na Urussi nzima alizaliwa tarehe 20 Novemba 1946 na hivi karibuni tu, amefanya kumbukizi la miaka 75, tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumpongeza na kumtakia heri na neema katika maisha na utume wake. Kwa upande wake, Askofu mkuu Hilarion Alfeyev amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Patriaki Cyrill wa Moscow na Urussi nzima salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko kusherehekea kumbukizi la Miaka 85 tangu kuzaliwa kwake hapo tarehe 17 Desemba 1936. Baba Mtakatifu amekumbushia pia majadialino ya kiekumene na hatimaye, tamko lililotolewa na viongozi hawa wawili nchini Cuba baada ya kukutana kwa pamoja, tarehe 12 Februari 2016.

Kanisa la Kiorthodox

 

22 December 2021, 14:44