Tafuta

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus inapania kufuata nyayo za Mtakatifu Barnaba, Mtume ili kukuza Kanisa na kidugu, wakala wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus inapania kufuata nyayo za Mtakatifu Barnaba, Mtume ili kukuza Kanisa na kidugu, wakala wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Barnaba na Paulo, Mitume

Papa Francisko amekaziaa: Umuhimu wa kudumisha ushirika katika utofauti wao; kukuza fadhila ya uvumilivu kwa sababu watu wanataka kuona Kanisa ambalo limejengwa na kusimikwa kwenye fadhila ya uvumilivu. Historia na maisha ya Mtakatifu Barnaba Mtume, aliyebahatika kukutana na Sauli huko Tarso na huo ukawa ni mwanzo wa kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuwasili nchini Cyprus na kupokelewa rasmi na viongozi wa kiserikali na kidini, Alhamisi, tarehe 2 Desemba 2021 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na: Wakleri, watawa, makatekista pamoja na wanachama wa vyama vya kitume nchini Cyprus. Mkutano huu umefanyikia kwenye Kanisa kuu la Bikira wa Neema huko Nicossia. Baba Mtakatifu amewapongeza viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao kwa mchango wao katika shughuli za kichungaji hususan katika sekta ya elimu, mahali muafaka pa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kuendeleza majadiliano pamoja na wanafunzi kujipatia ujuzi na maarifa. Amewashukuru kwa uwepo wao wa karibu kwa watu wa Mungu hasa katika nyakati tete za maisha. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha ushirika katika utofauti wao; kukuza fadhila ya uvumilivu kwa sababu watu wanataka kuona Kanisa ambalo limejengwa na kusimikwa kwenye fadhila ya uvumilivu. Historia na maisha ya Mtakatifu Barnaba Mtume, aliyebahatika kukutana na Sauli huko Tarso na huo ukawa ni mwanzo wa kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Ndiyo maana waamini wanahitaji kuona Kanisa la kidugu, kama wakala wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Hija ya Baba Mtakatifu nchini Cyprus inapania kufuata nyayo za Mtakatifu Barnaba Mtume na Mwinjilishaji hodari aliyefanikiwa kuiona neema ya Mungu, akafurahi na kuwasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Rej. Mdo 11: 23. Baba Mtakatifu anasema, yuko kati yao kwa ajili neema ya Mungu inayotenda kazi nchini Cyprus, ili kufurahi pamoja nao na kamwe wasikate tamaa. Baba Mtakatifu amewasifu na kuwapongeza waamini wa Kanisa la Wamaroniti ambalo limepitia katika changamoto mbalimbali, lakini limeendelea kuwa imara katika imani. Amesikitishwa na madhara makubwa ya machafuko ya kisiasa yanayoendelea kujitokeza nchini Lebanon. Hawa ni watu ambao wamejaribiwa sana kutokana na machafuko sanjari na utofauti wao. Anawaombea ili waweze kupata amani ya kudumu. Sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu zinataja uzuri na ukuu wa Lebanon na kwamba, waamini hawa ni sehemu ya mizizi kutoka Lebanon iliyopandikizwa nchini Cyprus, ili kueneza harufu ya uzuri wa Injili. Hata waamini wa Madhehebu ya Kilatini wanazidi kuongezeka maradufu na hivyo Cyprus kuwa ni daraja linalowakutanisha watu kutoka katika makabila na tamaduni mbalimbali.

Kanisa ni Katoliki liko wazi kwa watu wote, kwani wanakaribishwa na kukutana chini ya mwamvuli wa huruma na upendo wa Mungu na kamwe, pasiwepo na kuta za utengano ndani ya Kanisa Katoliki. Kanisa linapaswa kuwa ni nyumba ya wote, mahali pa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na hatimaye, kuishi katika ushirika unaofumbatwa katika utofauti! Mtakatifu Barnaba ni Mlinzi na Mwombezi wa nchi ya Cyprus, aliyekuwa na imani thabiti, hekima na busara na shuhuda wa waamini waliokuwa wamemwongokea Kristo Yesu katika maisha yao kutoka katika Kanisa la Antiokia. Alikuwa makini na akaguswa na tamaduni za watu wenye ari na mwamko mpya lakini bado imani yao ilikuwa ni dhaifu na Mtakatifu Barnaba akaonesha fadhila ya uvumilivu. Uvumilivu ulimwezesha kusoma alama za nyakati na kuendelea kusoma tamaduni za watu wengine. Uvumilivu ulimsaidia kuwasindikiza Wakristo wapya kwa kuwataka kuzingatia mambo msingi katika maisha,  akawashika mkono na kujadiliana nao kwa unyenyekevu mkuu. Waamini wanahitaji Kanisa ambalo ni vumilivu, tayari kukubali na kupokea upya unaokuja kwa kufanya mang’amuzi ya dhati mintarafu mwanga wa Injili.

Kanisa nchini Cyprus limeonesha kuwa ni Kanisa ambalo linawapokea na kuwalinda watu; linawaendeleza na kuwahusisha kikamilifu katika maisha na utume wake. Huu ni ujumbe murua kwa Kanisa Barani Ulaya ambalo linapambana na mmong’onyoko wa imani. Baba Mtakatifu Francisko anasema huu ni wakati wa uinjilishaji mpya hasa kwa vijana wa kizazi kipya, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa uvumilivu mkubwa katika maisha ya sala, kwa kukutana na mapadre wao; kwa kuheshimiana na kuthaminiana na waamini wa Makanisa mengine. Wakleri kwa namna ya pekee kabisa wanahimizwa na Baba Mtakatifu kuwa wavumilivu kwa waamini wao, kwani wao ni wahudumu wa msamaha na huruma ya Mungu na kamwe wasiwe na haraka ya kutoa hukumu kali, bali watambue kwamba, waamini wao ni “historia takatifu” na wanapaswa kuingizwa ndani ya Kanisa kwa uvumilivu. Hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ambayo inapaswa kumwilishwa kwa njia ya usikivu, kwa kuonesha unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuendelea kuwa wazi kwa binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Barnabas Mtume, alikutana na Paulo wa Tarso aliyekuwa amemwongokea Kristo Yesu hivi punde. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, “Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.” Mdo 9:26. Kwa sababu hapo mwanzoni alilidhulumu Kanisa la Kristo Yesu, lakini Barnaba akamtwaa akampeleka kwa Mitume na kusimulia yote yaliyotokea. Neno la Mungu likaendelea kukua na kukomaa kwa sababu ya neema na udugu wao uliong’ara kwa Amri ya upendo, hata kama katika safari ya maisha yao wakati mwingine walijikuta wakiwa wanasigana, jambo la kawaida kabisa kwa sababu ya watu kuwa na mawazo tofauti. Udugu wa Kikristo katika Kanisa unawawezesha waamini kujadiliana kwa kina na mapana kuhusu dira, vipeo, hisia na mawazo yao katika ukweli na uwazi, ili kwa pamoja waweze kukua, kukomaa na kubadilika. Majadiliano haya si kwa ajili ya mtu kutaka kujikweza bali ni kielelezo cha uhai wa Roho Mtakatifu anayewaongoza katika upendo na ushirika.

Kimsingi waamini wanahitaji Kanisa ambalo ni la kidugu ambalo ni wakala wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni. Cyprus ina waamini wenye historia, madhehebu na mapokeo mbalimbali, kumbe hapa ni mahali pa kushuhudia ushirika na utofauti na wala hakuna sababu ya kuwa na wivu usiokuwa na mashiko wala baadhi ya waamini kutaka kujilinda kupita kiasi. Waamini wajifunze kuheshimiana na kuthaminiana, ili kukuza na kudumisha udugu wa Kikristo, tayari kuvuka: kinzani, mipasuko na migawanyiko, ili kujenga na kudumisha ushirika. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru waamini wote kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu mintarafu njia iliyotengenezwa na watakatifu Paulo na Barnaba, Mitume. Ni matumaini yake kwamba, Kanisa litaendelea kuwa na uvumilivu, kwa kufanya mang’amuzi, kuwasindikiza na kuwahusisha waamini wote kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la kidugu hata katika tofauti zake, bado linaweza kuendelea kuwa na ushirika.

Papa Cyprus Hotuba
02 December 2021, 16:52