Tafuta

Papa: Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu Katika Historia ya Wokovu

Wainjili wote wanamtambua Yosefu kuwa ni Baba Mlishi wa Kristo Yesu, aliyekuja hapa ulimwenguni kutimiza historia ya Agano Jipya na la milele na kwamba historia ya wokovu inajenga mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kwa Mathayo, historia ya wokovu inapata chimbuko lake kwa Abrahamu, lakini Luka anakwenda mbali zaidi hadi kufikia kwa Adamu! Wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Kwa njia ya maisha na ushuhuda wake awe ni msaada mkubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu amemgusia Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu. Katekesi ya Baba Mtakatifu, Francisko, Jumatano tarehe 24 Novemba 2021 imenogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inayoelezea kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu: 1: 12-16 “Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.”

Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inamwonesha Mtakatifu Yosefu katika historia ya wokovu. Injili zinamwonesha Kristo Yesu kwamba, alidhaniwa kuwa ni Mwana wa Yosefu na Mwana wa Seremala. Mwinjili Mathayo na Luka wanaonesha Ukoo wa Kristo Yesu, huku wakitoa nafasi kwa Mtakatifu Yosefu na kuonesha chimbuko lake katika historia ya wokovu, kwa kusema “Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo” Mt. 1: 16. Mwinjili Luka anaanza mbali zaidi, kule kwa Adamu. Wainjili wote wanamtambua Yosefu kuwa ni Baba Mlishi wa Kristo Yesu, aliyekuja hapa ulimwenguni kutimiza historia ya Agano Jipya na la milele na kwamba historia ya wokovu inayojenga mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Kwa Mwinjili Mathayo, historia ya wokovu inapata chimbuko lake kwa Abrahamu, lakini Mwinjili Luka anakwenda mbali zaidi hadi kufikia asili ya mwanadamu yaani Adamu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu. Mtakatifu Yosefu ni mtu muhimu sana, lakini alijinyenyekesha na kamwe hakupenda kujipatia kipaumbele cha kwanza. Hii inaonesha kwamba, hata katika maisha ya kawaida, kuwa watu muhimu, lakini mara nyingi husahauliwa na kamwe hawapewi kipaumbeke na vichwa vya habari kwenye vyombo vya upashanaji habari. Hata leo hii ndani ya jamii, kuna watu wanashiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto kwa njia ya mifano bora ya maisha! Hawa ni wale wanaowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha kwa kuwajengea tabia njema pamoja na kuwafundisha namna ya kupambana na changamoto za maisha pamoja na kukuza ari na moyo wa sala. Kuna watu wengi wanaosali, wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya  ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Watu wengi wanaweza kujitambua ndani ya maisha na utume wa Mtakatifu Yosefu, aliyetekeleza dhamana na wajibu wake pasi na makuu, katika hali ya kificho, akawa mwombezi, msaada na kiongozi nyakati za shida na magumu ya maisha. Mtakatifu Yosefu anawakumbusha kwamba, wale wote wanaotekeleza nyajibu zao pasi na makuu wanaye mwenza katika historia ya wokovu. Ulimwengu unawahitaji watu kama hawa. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka, Mtakatifu Yosefu anaoneshwa kama mlinzi wa Yesu na Bikira Maria. Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Yosefu ni Mlinzi na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu, kwa sababu Kanisa ni mwendelezo wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu katika historia. Wakati huo huo katika tumbo la Mama Kanisa, limefunikwa na kivuli cha Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu anaendelea na utume wake wa kumlinda Mtoto pamoja na Mama yake! Huu ni wajibu mzito wa Mtakatifu Yosefu wa kuendeleza ulinzi kwa ndugu na jirani kinyume kabisa na ilivyokuwa kwenye Agano la Kale.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Jamii mamboleo inapata katika historia ya Mtakatifu Yosefu maelekezo ya umuhimu wa umoja na mafungamano  ya udugu wa kibinadamu. Agano Jipya linasimulia kuhusu Ukoo wa Kristo Yesu si kwa sababu msingi za kitaalimungu, lakini pia ni kutaka kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, unaotangulia na kuwasindikiza watu katika maisha yao. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ili kuja ulimwenguni ameamua kufuata njia ya mafungamano ya kijamii. Hii ni changamoto pevu kwa watu wengi duniani. Wanajisikia kuwa wapweke, hawana nguvu wala ujasiri wa kusonga mbele na safari ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kuhusu Mtakatifu Yosefu katika historia ya wokovu kwa kusali Sala kwa ajili ya Mtakatifu Yosefu, mwenza wa safari, rafiki na msaada wa daima. Mtakatifu Yosefu uliweza kujenga na kukuza mahusiano ya pekee na Bikira Maria na Mtoto Yesu, tusaidie tuweze kutunza mahusiano na mafungamano katika maisha. Asiwepo hata mmoja anayehisi kutelekezwa, hali inayotokana na upweke. Kila mtu ajitahidi kujipatanisha na historia yake, na wale waliomtangulia na hivyo kutambua pia makosa aliyotenda, lakini kwa njia ya uweza wa Mungu ameweza kusonga mbele na kwamba, ubaya hauwezi kuwa na neno la mwisho. Mtakatifu Yosefu, jioneshe kama rafiki kwa wale wote wenye shida, kama ulivyomlinda Bikira Maria na Mtoto Yesu katika nyakati ngumu, utusaidie hata sisi katika safari yetu. Amina.

Yosefu Mtakatifu
24 November 2021, 16:45

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >