Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema, wakimbizi na wahamiaji ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake: Fondazione Migrantes Baba Mtakatifu Francisko asema, wakimbizi na wahamiaji ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake: Fondazione Migrantes 

Papa Francisko: Wakimbizi na Wahamiaji Ni Hazina, Amana na Utajiri wa Kanisa na Jamii

Papa Francisko amekazia mambo makuu matatu: Uhamiaji, Bara la Ulaya na Ushuhuda wa imani. “Waitalia Ulaya na Utume wa Kikristo” mada hii inaonesha jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika mchakato wa kutaka kufahamu ukweli kuhusu uhamiaji; ili kukoleza ari na mwamko wa kimisionari, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya Barani Ulaya. Upendo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Mfuko wa Wahamiaji “Fondazione Migrantes” wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia umepewa dhamana ya kuratibu shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Kanisa Katoliki nchini Italia mintarafu maisha ya wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Mfuko huu, kuanzia tarehe 9-12 Novemba 2021 unaendesha Kongamano la Kitaifa linalonogeshwa na kauli mbiu “Waitalia Ulaya na Utume wa Kikristo”. Wajumbe wa kongamano hili, Alhamisi tarehe 11 Novemba 2021 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Uhamiaji, Bara la Ulaya na Ushuhuda wa imani. “Waitalia Ulaya na Utume wa Kikristo” mada hii inaonesha jitihada za Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika mchakato wa kutaka kufahamu ukweli kuhusu uhamiaji; ili kukoleza ari na mwamko wa kimisionari, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, dhana ya wahamiaji inawaangalia wengine, lakini hawa ni sehemu ya watu wa Mungu waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, yeye ni mtoto kutoka katika familia ya wakimbizi, waliohamia nchini Argentina na kwamba, yeye pia ni sehemu ya wahamiaji! Baba Mtakatifu anasema, Bara la Ulaya linapaswa kufahamika kuwa ni nyumba ya wote. Kanisa kwa upende wake, linapaswa kuonesha moyo wa sifa na shukrani kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kubadili uso wa miji na Italia katika ujumla wake. Kumbe, ndoto kubwa kwa watu wa Mungu Barani Ulaya ni kuona kwamba, umoja unapewa kipaumbele cha pekee, kwa kutambua na kuthamini amali msingi zinazojitokeza ili kufurahia umoja katika utofauti unoonekana. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma pamoja na maamuzi mbele yanatoweka. Bara la Ulaya linahimizwa kupyaisha wito wake unaojikita katika mshikamano unaosimamiwa na kanuni auni.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ushuhuda wa imani kutoka kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka nchini Italia. Hawa wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, ukarimu na ushirika, kumbukumbu hai na endelevu kutoka kwa familia za Kiitalia. Hii ni amali na utajiri wa jamii unaopaswa kulindwa na kuhifadhiwa, kama sehemu ya mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo. Kumbe, kuna haja ya kujenga majadiliano katika ukweli na uwazi  kati vizazi mbalimbali; kati ya vijana na wazee. Vijana wengi wa Kiitalia wanaohamia sehemu mbalimbali za Ulaya wameonesha ushuhuda angavu wa imani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wazee na vijana hawa watakuza ushuhuda huu wa kiimani, ili kuendeleza tunu msingi na amali za kijamii: kiroho na kiutu! Majadiliano kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee ni fursa ya kitaalimungu inayolidaia Kanisa kuitazama kwa makini, hasa katika kipindi ambamo Mama Kanisa anaendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Wakimbizi na wahamiaji wakiweza kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya nchi zinazowapatia hifadhi ni baraka na utajiri mkubwa unaoiwezesha jamii kukua na kukomaa.

Wakimbizi na wahamiaji ni baraka kwa Kanisa Barani Ulaya, ni kielelezo cha umoja, ukatoliki wa Kanisa na ushuhuda wa utume wa Kanisa, na kwamba, wanaweza kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha; urafiki na kama sehemu ya majadiliano ya kidini na kiekumene yanayofumbatwa katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu amewapongeza watu wa Mungu nchini Italia kwa kujielekeza zaidi katika mchakato wa hija ya Kisinodi inayorutubishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kichungaji. Hizi ni jitihada zinazotekelezwa kwa makusudi ili kuwatambua wakimbizi na wahamiaji kuwa ni amali za kijamii na utajiri, kwa ajili ya kupyaisha maisha na utume wa Kanisa Barani Ulaya. Vijana wa kizazi kipya wanavutwa kuwaona viongozi wa Kanisa wakishirikiana bega kwa bega na wakimbizi pamoja na wahamiaji. Mwenyeheri Giovanni Battista Scalabrini alijitahidi sana kuboresha maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Mtakatifu Francesca Cabrini, Msimamizi wa wakimbizi ayaongoze na kuyalinda Makanisa Barani Ulaya katika mchakato mpya wa kutangaza kwa furaha na kushuhudia kinabii Injili ya Kristo Yesu. Mwishoni, amewashukuru wajumbe kwa mchango wao na kuwataka kuendeleza ari na mwamko huu kwa kujikita katika ubunifu wa kitume. Lengo ni kuziwezesha jumuiya za waamini kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na ukarimu.

Migrantes
11 November 2021, 15:47