Mahojiano ya Papa na Jarida La "Paris Watch": Nyanyaso, UVIKO na Katiba ya Kitume!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Serikali mbalimbali duniani kwa upande wake, zinapaswa pia kujizatiti ili kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ambazo zimekithiri katika familia. Kuna makundi ya watu ambayo yamejikita kutengeneza na kuuza picha za utupu, kinyume cha maadili, utu wema na haki msingi za binadamu. Serikali na watunga sheria wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanadhibiti vitendo hivi mapema iwezekanavyo!
Hii ni sehemu ya mahojiano yaliyofanywa kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Mwandishi wa Habari Caroline Pigozzi wa Jarida la “Paris Watch." Baba Mtakatifu anakaza kusema, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni aibu kubwa ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na watu wote wa Mungu ili isitokee tena! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya. Anavishukuru vyama vya kitume na watu wanaojitolea katika kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna mambo mengi yanayoweza kuwakamata na kuwashtua watu, lakini zaidi wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa maisha, anawapenda watu wake upeo na zaidi ya yote, yeye yuko ulimwenguni kati ya viumbe vyake. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha watu wake katika upweke, kwa sababu amejishikamanisha sana na waja wake na upendo wake wa daima, unawawezesha kupata njia mpya. Kumbe, Mwenyezi Mungu anapaswa kutukuzwa milele!
Waamini wanakumbushwa kwamba, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya wema wote, awasaidie waamini kutafakari kuhusu hali tete ya maisha ya mwanadamu, ili hatimaye, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwalinda na kila ubaya! “Tume ya UVIKO-19 ya Vatican” “Vatican COVID-19 Commission” iliundwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 20 Machi 2020 na dhamana hii kukabidhiwa kwa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutokana na wimbi kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Tume ifanye upembuzi yakinifu na wakisayansi ili kuweza kutoa ushauri muafaka kwa Kanisa, kwa kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kipaumbele cha pekee ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utawala bora usaidie kukuza amani, usalama mambo msingi katika kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kitaifa na Kimataifa. Tume ijitahidi kuweka uwiano bora kati ya masuala jamii na ikolojia mintarafu UVIKO-19.
Baba Mtakatifu Francisko tangu alipokabidhiwa dhamana na utume wa kuliongoza Kanisa Katoliki, alishauriwa na Baraza la Makardinali kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa kwa kusoma alama za nyakati. Tangu mwaka 2013 Baba Mtakatifu anajielekeza zaidi katika masuala makuu matatu katika mageuzi haya: maboresho, udogo, ubora, ufanisi na tija kwa kuunganisha baadhi ya Mabaraza ya Kipapa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inaendelea kupewa msukumo wa pekee, ili kuwawezesha watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” unaendelea kuboreshwa zaidi, ili hatimaye, uweze kuchapishwa na kuanza kutekelezwa baada ya kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko.
Kumbe, kuna haja ya kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto mpya zinazoendelea kuibuliwa katika maisha na utume wa Kanisa, kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Baraza la Makardinali wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa mwaka 2013. Na swali kuhusu afya yake, Baba Mtakatifu Francisko amejibu kwa kusema, kwa sasa anaendelea na maisha na shughuli za kila siku. Mahojiano haya yanatarajiwa kuchapishwa kwenye Kitabu kijulikanacho kama “Pourquoi eux” “Kwa nini wao” kinachochapishwa na Kampuni ya Plon na kinatarajiwa kutoka tarehe 18 Novemba 2021. Mwandishi Caroline Pigozzi ataweka mahojiano haya ndani ya Kitabu hiki, ambacho kinajumuisha pia mahojiano yaliyofanywa na baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali, nchi pamoja na viongozi mashuhuri duniani!