Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kuiga mfano bora wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kwa kusimama kidete kutetea Injili ya uhai. Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kuiga mfano bora wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kwa kusimama kidete kutetea Injili ya uhai. 

Mt. Yohane Paulo II Ni Mfano Bora wa Kuigwa Katika Utu na Utakatifu

Papa mekutana na Mahujaji wa Familia ya Mtakatifu Vincenti kutoka Italia; Mahujaji waliofanya hija kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Muungano wa Waathirika wa Ghasia Italia. Ni hija ya kumshukuru Mungu kwa kubahatika kueneza Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na maambukizi ya UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kabla ya Katekesi yake Kuhusu Mtakatifu Yosefu katika Historia ya Wokovu, Jumatano tarehe 24 Novemba 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekutana na kuzungumza na Mahujaji wa Familia ya Mtakatifu Vincenti kutoka Italia; Mahujaji waliofanya hija kama sehemu ya kumbukumbu ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na Muungano wa Waathirika wa Ghasia Italia. Mahujaji wa Familia ya Mtakatifu Vincenti kutoka sehemu mbalimbali za Italia wanafanya hija ya kumshukuru Mungu kwa kubahatika kueneza Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kwa njia ya Ibada ya Medali ya Miujiza ya Bikira Maria, wamewasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema, kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Medali ya Miujiza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, imeitwa hivi kwa ajili ya miujiza mingi sana iliyotendeka kwa njia ya Medali hii.

Inasadikiwa kwamba, Medali hii ilibuniwa na Bikira Maria mwenyewe na inapata chimbuko lake la kihistoria kutoka kwa Mtakatifu Katarina wa Labore, Mtawa wa Shirika la Upendo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo aliyepewa dhamana ya kutengeneza Medali alama ya upendo na ulinzi kutoka kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo katika maisha na utume wake, limepewa dhamana na wajibu wa kuitangaza Medali hii. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza kwa utume wao makini miongoni mwa watu wanaoishi katika upweke, wagonjwa, wafungwa, watu wanaohifadhiwa kwenye Vituo vya wakimbizi na wahamiaji, bila kuwasahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu. Hiki ni kielelezo cha Kanisa linalotoka kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, kwa wale wote waliokata tamaa katika maisha. Baba Mtakatifu anawahimiza kuendeleza utume huu, huku wakitoa nafasi kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia nguvu ya kutangaza kwa ari na moyo mkuu upya wa Injili!

Mama Kanisa kunako mwaka 2020 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Yohane Paulo II alipozaliwa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Katekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane  Paulo II alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mei Mosi, 2011 akamtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari.

Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo! Ni katika muktadha huu, Chama cha Yohane Paulo II cha Bisceglie, Italia, kinafanya hija ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwataka mahujaji hawa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuiga mfano wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Wajitahidi kufahamu na kuupokea upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao, kama chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha. Wajitahidi kujenga na kudumisha ushirika na viongozi wao wa Kanisa, wamtangaze na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda katika medani mbalimbai za maisha.

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza pia na Wanachama wa Muungano wa Waathirika wa Ghasia Nchini Italia ulioanzishwa kunako mwaka 2006 “L' Associazione Italiana Vittime della Violenza, AIVV”. Hawa ni waathirika wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, nyanyaso na ukatili wa majumbani. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ghasia na vurugu nchini Italia. Hawa ni watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi! Ghasia ni tabia chafu sana! Muungano huu kwa njia ya maisha na utume wao unachangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mfano huu, usaidie kuamsha ndani ya watu wengi dhamana na wajibu wa kupyaisha huduma kwa waathirika, ili walindwe, kilio na mahangaiko yao yasikilizwe kwa makini na hatimaye kufanyiwa kazi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amesali pamoja na vikundi hivi na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Vikundi vya Mahujaji
24 November 2021, 14:52