Tafuta

Papa Francisko: Viongozi na wajumbe wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi COP26, Glasgow usikilize na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini. Papa Francisko: Viongozi na wajumbe wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi COP26, Glasgow usikilize na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini. 

Papa: COP26 Glasgow: Sikilizeni Kilio cha Dunia Mama na Maskini!

Jumuiya ya Kimtaifa tarehe 31 Oktoba 2021 imefungua mkutano wa Kimataifa kuhusu Mabadilio ya Tabianchi COP26 huko Glasgow, Scotland. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuweza kutoa majibu muafaka yatakayokuwa ni chimbuko la matumaini kwa vizazi vijavyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe12 Novemba 2021 ifanya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 31 Oktoba 2021 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Jumuiya ya Kimtaifa imefungua mkutano wa Kimataifa kuhusu Mabadilio ya Tabianchi COP26 huko Glasgow, Scotland. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuweza kutoa majibu muafaka yatakayokuwa ni chimbuko la matumaini kwa vizazi vijavyo! Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kwa sababu hawa ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia!

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linashiriki kikamilifu katika mkutano huu, ili kuyawakilisha Mashirika wanachama wake 162 kwenye mkutano huu. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi sanjari wongofu wa kiikolojia, kwa sababu mazingira ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” Baba Mtakatifu anakazia: Umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu katika Waraka wa “Laudato si”, anapembua kwa kina na mapana kuhusu: Mambo yanayotokea katika mazingira; umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Uumbaji. Anabainisha vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu, baadaye anazama zaidi kufafanua maana ya ikolojia katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa ushauri kuhusu njia za kupanga na kutekeleza na mwishoni anajiekeza zaidi katika elimu ya ikolojia na maisha ya Kikristo! Huu ni mwaliko unahimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na haki jamii, kwa kuwalinda na kuwaendeleza maskini na katika muktadha huu wakimbizi na wahamiaji duniani! Hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi na makazi yao kiasi kwamba, wanapoteza hadhi, utu, heshima, haki na utambulisho wao kama binadamu! Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Jumuiya ya Kimataifa imejikuta ikipambana na vipaumbele vipya, lakini sakata la utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote lazima lipewe kipaumbele cha kwanza. Hii inawezekana kwa kujikita katika uchumi fungamanishi na shirikishi, haki jamii na mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi. Zote hizi ni fursa zinazopaswa kutumiwa kikamilifu katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris wa mwaka 2015 vimetaka kuwepo kwa msaada wa kifedha kutoka vyanzo vilivyo na rasilimali nyingi kifedha kwenda kwa wale wenye uwezo mdogo na walioko hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Itifaki hii inatambua kwamba mchango unaotolewa na nchi moja na nyingine kwenye mabadiliko ya hali ya hewa na uwezo wao wa kuzuia na kukabiliana na athari zake hutofautiana sana. Fedha hizo zinahitajika ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa sababu uwekezaji mkubwa unahitajika katika kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa.  Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linalisema, Mkataba wa Paris umeeleza wajibu wa Nchi tajiri zaidi duniani na kuhimiza michango ya hiari kwa wadau wengine. Nchi hizo Zilizoendelea pia zimepewa jukumu la kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Nchi hizo pia zimepewa jukumu la kuunga mkono mikakati inayoendeshwa na Nchi zinazoendelea pamoja na kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya nchi hizo. Kimsingi juhudi za Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015 zinaongozwa na lengo lake kuu la kufanya kuwepo na mtiririko wa kifedha unaoendana na uzalishaji mdogo wa hewa ya ukaa kwa tabaka la Ozoni pamoja na kukuza uchumi fungamani. Mkataba unasema shughuli za uendeshaji wa wa taratibu za kifedha zinaweza kukabidhiwa kwa taasisi moja au zaidi za kimataifa zilizopo.

Kituo cha Mazingira Duniani (GEF) kimekuwa kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha tangu kuanza kutumika kwa Mkataba huo mwaka 1994. Katika Mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa UNFCCC, COP16, nchi zilianzisha Mfuko wa tabianchi (GCF) na mwaka 2011 kuuteua kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha. Utaratibu wa kifedha unawajibika kwa COP, ambao ndio unafanya maamuzi ya sera zake, programu zitakazopewa kipaumbele na vigezo vya wakataokuwa wanastahili kupata ufadhili. Kumbe, kuna Mfuko Maalum wa Mabadiliko ya Tabianchi (SCCF) na Mfuko wa Nchi masikini zaidi (LDCF). Mifuko yote hiyo inasimamiwa na GEF na Mfuko wa Kukabiliana (AF) ulioanzishwa chini ya Itifaki ya Kyoto kunako mwaka 2001. Caritas Internationalis linasema, ni wajibu wa kimaadili  kwa Nchi tajiri duniani kuchangia katika mchakato wa kuwalinda watu wa Mungu kutoka katika Nchi changa zaidi duniani, kwa sababu wao wamekuwa ni waathirika wakubwa hata kama hawakuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira. Ni wajibu wa Serikali kutunga na kutekeleza sera na sheria zinazozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kudhibiti uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Nchi Tajiri zitekeleze kikamilifu ahadi zake za kuchangia mfuko wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu upewe msukumo wa pekee katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi!

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland unawahusisha Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Viongozi wa Kidini, Viongozi wa Taasisi za Biashara, Asasi za Kiraia pamoja na watu mashuhuri. Pamoja na mambo mengine, COP26 unakusudia kujadili na kutoa maamuzi ya kuharakisha utekelezaji wa maazimio yaliyokwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anatarajia tarehe 2 Novemba 2021 kuhutubia katika mkutano huu. Pamoja na mambo mengine anatarajia kuuelezea ulimwengu hatua ambazo Tanzania imepiga katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto zilizopo na masuala yanayotakiwa kufanyika ili kupiga hatua zaidi katika kufanikiwa kufikia malengo yaliyowekwa na Jumuiya ya Kimataifa. Uingereza ni Rais na nchi mwenyeji wa mkutano wa COP26 Glasgow, Scotland.

Papa COP26
01 November 2021, 13:34