Maadhimisho ya Siku ya 36 Ya Vijana Ulimwenguni: Kijimbo 2021
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, sanjari na Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni inayoadhimishwa mwaka huu katika ngazi ya Kijimbo, Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa 4: 00 asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 6: 00 Mchana kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu “Inuka. Nimekuteua uwe Shahidi wa mambo haya uliyoyaona.” Mdo 26: 16. Siku hii kwa ngazi ya kijimbo inaadhimishwa tarehe 21 Novemba 2021, Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na umuhimu wa kuinuka na kuendelea na safari ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2021 yanaongozwa na ushuhuda wa Mtakatifu Paulo Mtume mbele ya Mfalme Agripa, baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka na kujitambulisha kwake akisema kuwa ni Yesu Mnazareti, kweli mang’amuzi haya yana umiza.
Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua upofu wa maisha yao, kuwa tayari kutubu na kumwongokea Mungu, na hatimaye kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni muda muafaka kwa vijana kuinuka na kuanza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Huu ni wakati wa kuinuka na kuanza kusherehekea Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo! Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufanya hija ya pamoja, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa kwa kujishikamanisha na upendo wa Kristo Yesu unaoganga na kuokoa. Hili ni jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini, dhana inayopewa kipaumbele cha pekee wakati huu wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa vijana.
Huu ni utajiri na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini, mapendo na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake! Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi.
Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma ya Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kipindi cha miaka yote hiyo!