Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni!

Kauli mbiu kwa Mwaka 2021: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Uhusiano na mafungamano ya Kristo Yesu na wafuasi wake na binadamu katika ujumla wake, yamewawezesha kufunuliwa Injili na Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka kielelezo cha ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Uhusiano na mafungamano ya Kristo Yesu na wafuasi wake na binadamu katika ujumla wake, yamewawezesha kufunuliwa Injili na Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia uzoefu wa Mitume wa Yesu wanaoshuhudia upendo, huruma na msamaha ulioneshwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Anaelezea matatizo na changamoto zilizojitokeza kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo katika mwanzo wa safari yao ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo hii, walimwengu wanakabiliwa na changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyefufuka na kutukuzwa ndiye chemchemi ya matumaini ya waja wake. Katika mchakato wa uinjilishaji, Wakristo wanahamasishwa pia kulinda na kutunza mazingira. Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha, mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo vya uinjilishaji.  

Baba Mtakatifu anasema kwamba, upendo na huruma ya Mungu imefunuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, katika Injili na hatimaye katika Fumbo la Pasaka. Wakristo wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kwamba, hakuna mtu anayetengwa na utume huu. Mitume wa Yesu wanashirikisha uzoefu na mang’amuzi ya urafiki wao na Kristo Yesu, uliowawezesha kukumbuka hata ule muda aliowaita kufuatana naye. Waliona na kushuhudia huruma, upendo na msamaha wa Yesu kwa watu waliokuwa na shida mbalimbali za maisha! Akawaponya, akawalisha na kuwasamehe dhambi zao, kielelezo cha upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Ni upendo uliowavuta Mitume kushirikisha mang’amuzi yao. Waamini wanakumbushwa kwamba wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na utimilifu huu unafumbatwa katika upendo unaowawezesha waamini kukubali udhaifu na mapungufu yao pamoja na yale ya jirani zao, tayari kujifunga kibwebwe ili kujenga udugu na urafiki wa kijamii, mwaliko kwa waamini kuwa ni watu wa shukrani.

Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walikumbana na matatizo na changamoto mbalimbali mwanzoni mwa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Walitengwa na kufungwa magerezani; walikumbana na kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii, lakini yote haya yakageuzwa kuwa ni fursa kwa ajili ya utume wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa kupakwa mafuta na Roho Mtakatifu. Ujumbe wa ukombozi uliwaambata na kuwakumbatia wote na wala hakuna aliyetengwa. Kitabu cha Matendo ya Mitume ni ushuhuda wa furaha inayoletwa na Roho Mtakatifu peke yake. Ni kitabu kinachowataka waamini kusimama imara katika imani huku wakimtegemea Kristo Yesu na kwamba, watazaa matunda kwa wakati muafaka! Hata katika ulimwengu mamboleo mambo si shwari sana. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha: mateso, upweke, umaskini na ukosefu wa haki kwa watu wengi duniani. Ni gonjwa ambalo limefunua mapungufu na madhaifu ya binadamu, lakini waathirika wakubwa ni maskini, Watu wamekatishwa tamaa na kukosa matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, bila matumaini maisha yangekosa maana na yangekuwa hayavumiliki. Kumbe, waamini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na sasa anao uwezo wote. Yesu Kristo anaishi kiukweli anawataka wafuasi wake wawe hai, wadumishe udugu wa kibinadamu, huku wakitangaza ujumbe wa matumaini na kwamba wote wanaweza kuokolewa ikiwa wameshikamana kwa sababu hakuna mtu anayeweza kujiokoa binafsi. Lakini pamoja na changamoto zote hizi, waamini wanapaswa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu, ujumbe wa matumaini. Huruma, upendo na msamaha ni sakramenti zinazoonesha ukaribu wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa kuwalinda na kuwatunza. Kanisa linatumwa kuinjilisha pamoja na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kwa asili Kanisa katika maisha yake ya imani na nguvu yake ya kinabii na kwamba, lipo kwa ajili ya kuinjilisha. Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu, kwa ukarimu, sadaka na majitoleo yao. Kwa hakika kila mtu anaweza kuwa ni mmisionari kadiri ya hali na mazingira yake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Duniani ni muda wa shukrani kwa Wakristo ambao wamejisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni kipindi muafaka cha kupyaisha tena ahadi za Ubatizo kwa kuendeleza ukarimu, ili hatimaye, waweze kuwa ni Mitume wa furaha ya Injili. Ni muda wa kuwakumbuka na kuwaombea wale wamisionari ambao wako nje ya nchi na familia zao ili kutangaza na kuzima kiu ya Injili ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Iwe ni nafasi ya kuombea miito mitakatifu kwa kutambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kristo Yesu anataka watu wanaotambua wito kuwa kama ni historia ya upendo inayowahamasisha kutoka na kwenda kuwa ni wajumbe na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Huu ni wito kwa watu wote na hasa wakati huu wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVKO-19. Waamini wafikiri na kutenda kama Kristo Yesu na kuamini kwamba, wale wote wanaowazunguka ni ndugu zao. Huruma na upendo wa Kristo viguse nyoyo za waamini wote ili kweli waweze kuwa ni Mitume Wamisionari.

Siku ya Kimisionari
15 October 2021, 16:25