Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni 2021

Baba Mtakatifu Francisko Ujumbe: Kila kitu kuhusu Kristo kinatukumbusha kuwa Yeye anaufahamu vizuri ulimwengu wetu pamoja na hitaji lake la ukombozi, na kinatutaka tushiriki kikamilifu katika utume huu: “Nendeni, basi, katika barabara na njia na kuwaalika wote mnaowakuta” (Mt 22:9). Hakuna aliyetengwa na hilo wala hakuna anayehitaji kujiona mbali na upendo huu mkubwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC.,  - Dar Es Salaam.

Ndugu wapendwa, Mara tunapoonja nguvu ya upendo wa Mungu na tunapotambua uwepo wake wa kibaba katika maisha yetu binafsi na ya jumuiya, hatuwezi kuacha kutangaza na kushirikisha yale tuliyoyaona na kuyasikia. Uhusiano wa Yesu na wafuasi wake na ubinadamu wake, kama tulivyofunuliwa katika fumbo la Umwilisho wake, Injili na Fumbo la Pasaka, unaonesha namna Mungu anavyoupenda ubinadamu wetu na anavyovifanya furaha na uchungu wetu kuwa vyake, pia matumaini yetu na mahangaiko yetu (Rejea Gaudium et spes, 22). Kila kitu kuhusu Kristo kinatukumbusha kuwa Yeye anaufahamu vizuri ulimwengu wetu pamoja na hitaji lake la ukombozi, na kinatutaka tushiriki kikamilifu katika utume huu: “Nendeni, basi, katika barabara na njia na kuwaalika wote mnaowakuta” (Mt 22:9). Hakuna aliyetengwa na hilo wala hakuna anayehitaji kujiona mbali na upendo huu mkubwa.

Uzoefu wa Mitume: Historia ya uinjilishaji ilianza na nia thabiti ya Bwana mwenyewe ya kumwita kila mmoja na kumfanya aingie katika uhusiano wa kirafiki nao. Pia aliwaingiza katika mazungumzo baina yake na hao, kadiri kila mmoja alivyo (rej. Yn 15:12-17). Mitume walikuwa wa kwanza kutuambia sisi hili; walikumbuka hata siku na saa walipokutana na Yesu kwa mara ya kwanza: “ilikuwa mnamo saa kumi hivi jioni” (Yn 1:39). Kwa kuonja urafiki wa Bwana, kumwona alivyowaponya wagonjwa, alivyokula na wakosefu, na kuwapa chakula wenye njaa, akiwapokea waliotengwa, na kuwagusa wanajisi, akijilinganisha na wahitaji na kupendekeza mafundisho ya HERI na kufundisha kwa mamlaka, tunaona kuwa aliwaachia alama isiyofutika, akiamsha mshangao, furaha tele na moyo mkuu wa shukrani. Nabii Yeremia anaieleza hali hii kama mmoja anayetambua fika uwepo wa Bwana katika mioyo yetu, akitusukuma kwenda kwenye utume, bila kujali ugumu wa majitoleo na sintofahamu zinazojitokeza katika utume huo (Rej. 20:7-9). Upendo daima unasonga mbele na unatutaka tushirikishwe ujumbe ulio wa ajabu na uliojaa matumaini. “Tumemwona Masiha” ((Yn 1:41).

Tukiwa pamoja na Yesu, pia tumeona, tumesikia na tumeonja kuwa mambo yanaweza kuwa tofauti. Hata sasa, Yesu amezindua nyakati zijazo, akitukumbusha jambo ambalo daima linasahaulika katika ubinadamu wetu, nalo ni kwamba “tumeumbwa kwa ajili ya lile linaloweza kukamilika katika upendo” (Fratelli tutti, 67). Jumuiya ya kikanisa inastawi daima inapokumbuka kwa moyo wa shukrani kwamba Bwana alitupenda kwanza (Rej. Yn 4:19). “Upendeleo wa upendo wa Bwana kwetu unatushangaza, na mshangao kwa wenyewe hauwezi kuwa mali yetu, wala haufanywi na sisi. Ni kwa namna hii tu mwujiza wa neema, kipaji cha bure, vinaweza kustawi. Wala ari ya umisionari haijawahi kuwepo kama matokeo ya akili zetu au ya mpangilio katika kufikiri. Kuwa katika hali ya umisionari kunaakisi moyo wa shukrani” (Ujumbe kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, 21 Mei 2020). Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi daima. Wakristo wa kwanza walianza maisha yao katika hali ya uadui na walikutana na magumu mbalimbali; hali ya kutengwa na jamiii na kufungwa jela, mambo yaliyoongozana na mapigano ya ndani na ya nje ambayo yalionekana kupingana na kuyakataa yale “waliyoyaona na kuyasikia”. Lakini hayo yote badala ya kuwa vipingamizi vya kuwarudisha nyuma au kuwafanya wajifungie wenyewe, wao yaliyaona kuwa ni fursa kwa utume (umisionari).

Mapungufu na vikwazo vilikuwa ni nafasi za upendeleo na mwafaka kwa kuwapaka wote mafuta ya Roho wa Bwana. Hakuna kitu wala mtu ambaye angetengwa na ujumbe wa ukombozi. Kuhusu hilo tunao ushahidi wa kutosha katika Kitabu cha Matendo ya Mitume, kitabu ambacho wafuasi wa kimisionari wanakisoma daima. Humo tunasoma namna Injili ilivyoenea kote ilikohubiriwa, ikiamsha furaha ambayo Roho Mtakatifu peke yake anaweza kuitoa. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatufundisha kuvumilia magumu kwa ajili ya kumtangaza Kristo, ili kukua katika imani kwamba Mungu anaweza kutenda kazi katika mazingira ya aina yoyote, hata kati ya vikwazo na changamoto na katika uhakika kwamba wote wanaomtumainia Mungu watazaa matunda mema (Rejea Evangelii gaudium, 279).

Hilo linatupata sisi pia: nyakati zetu siyo za urahisi. Balaa hii imetupeleka kwenye maumivu makali, upweke, umaskini na ukosefu wa haki kwa watu wengi. Limetufunulia mtazamo wetu batili wa usalama na kudhihirisha utengano unaokua kimya kimya kati yetu. Wale walio wanyonge wamefikia kujisikia hivyo hata zaidi. Tumeonja kukata tama, kuvunjika moyo na kuchoka; na wala hatujakwepa hali ya uovu ambayo inatupotezea matumaini. Hata hivyo, sisi kwa upande wetu “hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe ni watumishi wema kwa ajili ya Yesu” (2 Kor 4:5). Matokeo yake ni kwamba katika jumuiya na familia zetu tunaweza kusikia ujumbe wenye nguvu kuhusu maisha, ujumbe ambao unasisikika katika mioyo yetu na unalia: “Hayupo hapa, amefufuka” (Lk 24:6). Ujumbe huu wa matumaini unavunja kila aina ya uthubutu na kwa wale wanaoguswa nao unawapa uhuru na ujasiri unaohitajika ili kuinuka na kutafuta njia iwezekanayo kuonesha huruma, kisakramenti cha ukarimu wa Mungu kwetu, ukaribu ambao haumwachi yeyote nje ya njia.

Katika siku hizi za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambapo kuna kishawishi cha kupuuza na kuhalalisha hali ya kutojali na kutoguswa, kwa kisingizio cha kutunza utengano-tahadhari wa kijamii, kuna hitaji la haraka la utume wa huruma, ambao unaweza kuufanya utengano huo uwe fursa ya kukutana, kujaliana na kuinuana. Tuliyoyaona na kuyasikia (Mdo. 4:20), huruma tuliyoionja, vinaweza kuwa chachu na chanzo cha imani, ambacho kinatufanya tuweze kurejesha tena hamasa ya pamoja ya kujenga jamii yenye kutufanya tujisikie nyumbani na mshikamano unaoendana na nyakati zetu, nguvu zetu na raslimali zetu (Fratelli tutti, 36). Neno la Bwana linatusaidia na linatuokoa kila siku na aina ya udhuru unaotuingiza katika hali ya visingizio kwamba “hakuna kinachobadilika, kila kitu kinabaki katika hali hiyo hiyo”. Kwa wale wanaoshangaa kwa nini wanapaswa kuukatia tamaa usalama wao, raha na starehe kama hawawezi kuona matokeo ya maana, jibu letu litabaki daima lile lile kuwa: “Yesu Kristo ameshinda dhambi na mauti, na sasa ni Mwenye enzi” Yesu Kristo ni mzima kweli (Evangelii gaudium, 275) na anatutaka tuwe hai, wamoja, na wenye uwezo wa kutunza na kushirikishana ujumbe huu wa matumaini. Katika mazingira yetu ya sasa kuna hitaji la haraka la wamisionari wa matumaini ambao wakishapakwa mafuta ya Bwana wanaweza kutoa kumbusho la kinabii kwamba hakuna anayejiokoa mwenyewe.

Kama mitume na wakristo wa kwanza nasi pia tunaweza kusema kwa imani yote: “Hatuwezi kukaa kimya juu ya yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo. 4:20). Yote tuliyoyapokea toka kwa Bwana ni kwa ajili ya kuyatumia vizuri na kuwashirikisha wenzetu kwa uhuru. Kama mitume walivyoiona, kuisikia na kuigusa nguvu ya kuokoa ya Yesu (Rej. 1Yn 1:1-14), sisi pia tunaweza kugusa kila siku mwili wa Kristo wenye uchungu na wenye utukufu. Hapo tunatiwa nguvu ya kuwashirikisha wote tunaokutana nao hatima ya matumaini, utambuzi hakika kwamba Bwana yupo upande wetu daima. Kama Wakristo, hatuwezi kumweka Bwana kwa ajili yetu wenyewe: utume wa Uinjilishaji wa Kanisa unakamilika kwa nje katika kuubadili ulimwengu wetu na kuvitunza viumbe.

Mwaliko kwa kila mmoja wetu: Kaulimbiu ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni mwaka huu 2021: “Hatuwezi kukaa kimya juu ya yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo. 4:20) ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kumiliki na kuwapa wengine kile tulicho nacho moyoni mwetu. Utume huu umekuwa daima kitambulisho cha Kanisa, kwani Kanisa lipo kwa ajili ya Uinjilishaji (Mtakatifu Paulo VI, Evangelium nuntiandi, 14). Uhai wa imani yetu unadhofika, unapoteza nguvu ya kinabii na uwezo wake wa kuamsha mshangao na shukrani, tunapojitenga na kujiweka katika vikundi vidogo vidogo. Kwa hali yake, imani inataka uwazi unaokua kiasi kwamba unamkaribisha kila mtu, kila mahali. Wakristo wa kwanza walijiepusha na kishawishi cha kuwa kundi la watu wa tabaka la juu, waliongozwa na Bwana na zawadi yake ya maisha mapya; na kwa hali hiyo wakaenda kwa mataifa na kutoa ushuhuda wa yale waliyoyaona na kuyasikia: habari njema kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia. Walifanya hivyo kwa ukarimu, kwa shukrani na uungwana, kama ilivyo kawaida ya wale ambao wanapanda mbegu wakijua kwamba wengine watafurahia matunda ya jitihada na majitoleo yao. Napenda kufikiri kwamba “hata wale walio dhaifu, wenye mapungufu na wenye kutaabishwa wanaweza kuwa wamisionari kwa namna yao, kwani wema daima unaweza kushirikishwa, hata kama umeambatana na mapungufu mengi” (Christus vivit, 239).

Katika Siku ya Kimisionari Ulimwenguni ambayo tunaiadhimisha kila mwaka Dominika ya tatu (ya pili toka mwishoni) ya Mwezi Oktoba, tunawakumbuka kwa shukrani watu wote, wake kwa waume, ambao kwa ushuhuda wa maisha yao wanatusaidia sisi kupyaisha ahadi zetu za Ubatizo, ili tuwe mitume wa Injili wakarimu na wenye furaha. Tuwakumbuke kwa namna ya pekee wale ambao waliondoka, wakaacha makazi na familia zao, ili kwenda kupeleka Habari njema kwa wale wenye kiu ya ujumbe huo unaookoa. Tunapotafakari ushuhuda wao wa kimisionari tunapata ujasiri wa kumwomba “Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake” (Lk 10:2). Tunafahamu kwamba wito wa umisionari si kitu kilichopitwa na wakati, au kumbukumbu za mambo yanayopendeza ya kale. Leo pia Yesu anaihitaji mioyo yenye uwezo na yenye kuonja wito kama hadithi ya mapenzi ya kweli ambayo inawasukuma waende katika maeneo ya pembezoni mwa dunia, kama wajumbe na wadau wa huruma. Bwana analeta mwito wake kwetu sote, na kwa namna tofauti tofauti. Tunaweza kufikiria maeneo yote ya pembezoni yanayotuzunguka, katika miji yetu, au hata katika familia zetu. Daima, lakini hasa wakati huu wa majanga, ni muhimu kukua siku kwa siku katika uwezo wetu wa kupanua mtazamo wetu, kuwafikia wengine, ambao pengine wapo karibu nasi, lakini si sehemu yetu, na hatuwafikirii (Rej. Fratelli tutti, 97). Kuwa katika umisionari ni kutaka kufikiri namna ambayo Kristo alifikiri, yaani, kuwa na imani naye kwamba wale wanaotuzunguka ni ndugu zetu pia. Tunaomba upendo wake uliojaa huruma uguse mioyo yetu na utufanye sote tuwe mitume wa kweli wa kimisionari. Maria, mfuasi wa kimisionari wa kwanza, awaongezee wabatizwa wote hamu ya kuwa Chumvi na Nuru katika nchi zetu (Rej. Mt. 5:1314).

Imetolewa Roma, Mtakatifu Yohane wa Laterano, 6 Januari 2021, Sherehe ya Tokeo la Bwana.

Ujumbe wa Siku ya kimisionari

 

22 October 2021, 15:19